Advertisements

Wednesday, September 2, 2015

AFRIKA KUZINGATIA VIPAUMBELE VYAKE WAKATI WA UTEKELEZAJI WA MALENGO MAPYA YA MAENDELEO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akizungumza siku ya Jumanne, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio lanalowasilisha kwa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali Malengo na Ajenda mpya za Maendeleo Endelevu ( Ajenda 2030) Anaonekana pia Rais wa Baraza Kuu la 69, Bw. Sam Kutess
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akiwa na Afisa Mkuu Siongelael Shilla wakati wa upitishaji wa Azimio namba A/69/L.85 kuhusu Ajenda 2030 ambapo baada ya kupitishwa kwa kauli moja azimio hilo wazungumzaji wanaowakilisha makundi ya kikanda walipata fursa ya kuelezea misimamo yao juu ya baadhi ya mambo ambayo walikuwa wakitofautiana kimtizamo na kimsimamo.

Na MwandishiMaalum, New York
Afrika, imesisitiza na kubainisha kwamba itatekeleza malengo mapya ya maendeleo endelevu kwa kuzingatia maslahi, vipaumbele, sera, mila na tamaduni ambazo nchi za Afrika zimejiwekea.

Aidha Afrika inasema kuwa, utekelezaji wa malengo hayo pia utazingatia sheria za kimataifa na ambazo nchi za Afrika zimeridhia na sivinginevyo.

Hayo yameelezwa na Balozi Fode Seek,Mwakilishi wa Kudumu wa Senegal katika Umoja wa Mataifa ambaye ni Mwenyekiti wa nchi za Afrika kwa mwezi Septemba.

Alikuwa akizungumza kwa niaba ya nchi za Afrika wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokutana siku ya jumanne, kupitisha Azimio namba A/69/L.85 ambalo linawasilisha ajenda ya Maendeleo Endelevu (ajenda 2030) itakayotekelezwa kwa miaka 15 ijayo.

Ajenda 2030 inachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayofikia ukingoni mwishoni mwa mwaka huu.

Kupitishwa kwa azimio hilo la ajenda 2030, inayojumuisha malengo 17 na ambalo sasa litawasilishwa baadaye mwezi huu wa Septemba kwa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali tayari kwa kuridhiwa na kuanza utekelezaji wake mwakani, kunakamilisha mchakato uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili ya majadiliano yaliyozaa malengo mapya na ajenda mpya.

“Afrika itashirikiana na wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa malengo haya yanayolenga katika kuondoa umaskini, kuboresha huduma za jamii, upatikanaji wa fursa za maendeleo na ajira na bila ya kumwacha yoyote nyuma. Lakini tutatekeleza kwa kuzingatia mipango yetu, vipaumbele vyetu, sera zetu na kwa maslahi ambayo kila nchi itaona inafaa kutokana mazingira na uwezo wa nchi yenyewe” akasema Balozi. Seek

Baadhi ya mambo ambayo Afrika inasema kimsingi haikubaliani katika ujumla wake na ambayo kwa utekelezaji wake utazingatia utashi wa kila nchi, kuzingatia Imani za kidini, mila na tamaduni na sheria za nchi husika ni pamoja na tafsri sahihi ya neno familia ambalo Afrika na baadhi ya nchi nyingine inasema familiani Baba, Mama na watoto na tafsiri inayopigiwa chapuo na baadhi ya nchi za magharibi.

Jambo jingine ambalo Afrika na Nchi nyingine imetoa msimamo, linahusu tafsiri ya jinsia ambayo kwa Afrika inaami ni kwamba jinsia ni ya kike na kiume.

Utolewaji na upatikanaji wa huduma za afya, elimu na mafunzo yanayoambatana na eneo hilo hususani uzazi wa mpango,ambalo Afrika na mataifa mengine yanayoendelea yanasisitizia kuwa utekelezaji wake usiwe wa shurutisho na ufanyike kwa kuzingatia mila na desturi za nchi husika.

Mbali ya msemaji huyo kwa niaba ya nchi za Afrika kuanisha baadhi ya maeneo ambayo Afrika itayatekeleza pasipo kushurutishwa.Wazungumzaji zaidi ya 30 wakiwakilisha makundi ya kikanda na baadhi wakizungumza kwa niaba ya nchi zao walichangia maoni yao kuhusu ajenda 2030.

Mwakilishi wa Kudumu wa Afrika ya Kusini Balozi Kingsley Mamabolo ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la G77& China. Akizungumza kwa niaba ya kundi hilo anasema.Haikuwa kazi nyepesi kufikia makubaliano yaliyopelekea kupitishwa kwa kauli moja Malengo na Ajenda 2030

“Ajenda hii ambayo tumeipitisha kwa kauli moja, hatuwezi kusema kwamba haina mapungufu. lakini tumefika hapa tulipo baada ya majadilliano marefu na magumu na kukubaliana kutokukubaliana”.

Na akaongeza Ajenda 2030 ina mambo mengi yakiwamo malengo 17 na viashiria 169. Lakini jambo moja la msingi na muhimu ni kwamba,utekelezaji wake utategemea kila nchi inavyopanga vipaumbele vyake na sera zake” akasema Balozi Mamabolo.

Awali akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa Azimio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema. Agenda 2030 ni makubaliano ambayo kila nchi inapashwa kujivunia na kwamba utekelezaji wake utahitaji ushirikiano wa karibu baina ya wadau mbalimbali.

Akasema Agenda 2030 itapitishwa na Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa mbalimbali duniani akiwamo Baba Mtakatifu Francis.

No comments: