Shekhe Mkuu wa Tanzania ambaye pia
ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir Bin Ally amewataka Watanzania
kumwomba Mungu ili awapatie kiongozi bora katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu.
Shekhe Zubeir aliyasema hayo jana
kwenye mkutano mkuu wa Bakwata uliompitisha kuwa Mufti wa Tanzania
kwa kura za wajumbe wote 310 baada ya mtu aliyeingia naye katika
ushindani huo kujitoa.
Katika kinyang’anyiro hicho Shekhe
Aboubakar alikuwa na wenzake watatu ambao ni Shekhe Khamis Mtupa,
Shekhe Hassan Kiburwa kutoka mkoa wa Kigoma na Shekhe Ally Mkoyogole
kutoka Dar es Salaam.
Tume ya dini iliyaondoa majina ya
mashekhe wawili na kuwabakiza Mufti na Shekhe Mkoyogole ambaye naye
aliamua kwa hiyari yake kujitoa ndipo wajumbe wakapiga kura za ndiyo.
Katika hotuba yake Mufti aliwataka
Watanzania kumwomba Mungu ili ailinde nchi ya Tanzania katika
kipindi cha uchaguzi mkuu wa Madiwani, wabunge na Rais lakini akataka
waislamu wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi
mkuu.
Aidha aliwaagiza mashekhe wote wa
Mikoa, Wilaya na kata kuomba dua kwa Mungu katika kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mkuu ili Mungu aendelee kuidumisha amani ya nchi.
“Kama watu hawaombi Mungu
anawaachia tu lakini wakiomba yeye atatenda tena atatenda yaliyomema
zaidi,” alisema Shekhe Aboubakar.
Kiongozi huyo aliwashukuru waislamu
kwa kumwamini na kumpa kazi ya kuwatumikia na kuahidi kushirikiana
nao kwa ajili ya kulijenga baraza la Waislamu nchini (Bakwata) na
kuwa pamoja katika masuala yote ya maendeleo ya baraza.
Ahadi nyingine kwao ni kuwa hatakuwa
mtu wa ofisini na badala yake atatenga muda wa kutembelea mikoa na
wilaya ili kuimarisha dini ya Kiislamu.
“Ninaliagiza baraza kulinda amani
ya nchi na utulivu na kujiepusha na viashirio na kila jambo
linalovuruga amani ya nchi hii huku akisema kuwa Uislamu ndiyo kitovu
cha amani,” alisema Shekhe Mkuu.
Katika hatua nyingine Mufti huyo
alimshukuru Shekhe Ally Mkoyogole kwa kumwamini na kumwachia nafasi
hiyo na kusema kuwa huo ndiyo ucha Mungu wa kweli.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye
alikuwa ni mgeni rasmi Chiku Galawa, aliwataka waislamu kuwakumbusha
vijana wao katika kusoma elimu ya dini pamoja na elimu nyingine ili
wasipitwe na fursa zilizopo.
Galawa alisema kuwa Quruan inawagiza
waislamu kusoma zaidi na kutenda mema lakini wanapaswa kufanya hivyo
kwa kuonyesha kwa vitendo kile wanachokisoma ili kuleta mabadiriko
nchini.
Hata hivyo alionyesha masikitiko
kuwa alipokea majina mengi kwa vijana waliokamatwa na madawa ya
kulevya lakini asilimia 90 ya majina hayo yalikuwa ni ya Kiislamu
jambo alilosema linapaswa kutolewa elimu kwa vijana.
Katibu Mkuu wa Bakwata Seleman
Lolila aliwataja wajumbe waliostahili katika Mkutano huo ni Mashekhe
wa Mikoa na wilaya, Wenyeviti na Makatibu wa halmashauri za Bakwata
mikoa na wilaya na Katibu Mkuu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake