ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 10, 2015

BAKWATA YAMCHAGUA SHEKHE ABOUBAKAR ZUBEIR BIN ALLY KUWA MUFTI WA TANZANIA



Shekhe Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir Bin Ally amewataka Watanzania kumwomba Mungu ili awapatie kiongozi bora katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Shekhe Zubeir aliyasema hayo jana kwenye mkutano mkuu wa Bakwata uliompitisha kuwa Mufti wa Tanzania kwa kura za wajumbe wote 310 baada ya mtu aliyeingia naye katika ushindani huo kujitoa.

Katika kinyang’anyiro hicho Shekhe Aboubakar alikuwa na wenzake watatu ambao ni Shekhe Khamis Mtupa, Shekhe Hassan Kiburwa kutoka mkoa wa Kigoma na Shekhe Ally Mkoyogole kutoka Dar es Salaam.

Tume ya dini iliyaondoa majina ya mashekhe wawili na kuwabakiza Mufti na Shekhe Mkoyogole ambaye naye aliamua kwa hiyari yake kujitoa ndipo wajumbe wakapiga kura za ndiyo.

Katika hotuba yake Mufti aliwataka Watanzania kumwomba Mungu ili ailinde nchi ya Tanzania katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa Madiwani, wabunge na Rais lakini akataka waislamu wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu.

Aidha aliwaagiza mashekhe wote wa Mikoa, Wilaya na kata kuomba dua kwa Mungu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili Mungu aendelee kuidumisha amani ya nchi.

“Kama watu hawaombi Mungu anawaachia tu lakini wakiomba yeye atatenda tena atatenda yaliyomema zaidi,” alisema Shekhe Aboubakar.

Kiongozi huyo aliwashukuru waislamu kwa kumwamini na kumpa kazi ya kuwatumikia na kuahidi kushirikiana nao kwa ajili ya kulijenga baraza la Waislamu nchini (Bakwata) na kuwa pamoja katika masuala yote ya maendeleo ya baraza.

Ahadi nyingine kwao ni kuwa hatakuwa mtu wa ofisini na badala yake atatenga muda wa kutembelea mikoa na wilaya ili kuimarisha dini ya Kiislamu.

Ninaliagiza baraza kulinda amani ya nchi na utulivu na kujiepusha na viashirio na kila jambo linalovuruga amani ya nchi hii huku akisema kuwa Uislamu ndiyo kitovu cha amani,” alisema Shekhe Mkuu.

Katika hatua nyingine Mufti huyo alimshukuru Shekhe Ally Mkoyogole kwa kumwamini na kumwachia nafasi hiyo na kusema kuwa huo ndiyo ucha Mungu wa kweli.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye alikuwa ni mgeni rasmi Chiku Galawa, aliwataka waislamu kuwakumbusha vijana wao katika kusoma elimu ya dini pamoja na elimu nyingine ili wasipitwe na fursa zilizopo.

Galawa alisema kuwa Quruan inawagiza waislamu kusoma zaidi na kutenda mema lakini wanapaswa kufanya hivyo kwa kuonyesha kwa vitendo kile wanachokisoma ili kuleta mabadiriko nchini.

Hata hivyo alionyesha masikitiko kuwa alipokea majina mengi kwa vijana waliokamatwa na madawa ya kulevya lakini asilimia 90 ya majina hayo yalikuwa ni ya Kiislamu jambo alilosema linapaswa kutolewa elimu kwa vijana.

Katibu Mkuu wa Bakwata Seleman Lolila aliwataja wajumbe waliostahili katika Mkutano huo ni Mashekhe wa Mikoa na wilaya, Wenyeviti na Makatibu wa halmashauri za Bakwata mikoa na wilaya na Katibu Mkuu.

No comments: