Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akihutubia wakazi wa Mafinga, Iringa wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Wambi jana. Picha na Adam Mzee wa CCM.
Mbarali. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana alikabiliana na wafuasi wa Chadema katika ziara yake ya kampeni, akawaahidi mabadiliko wanayohitaji ya kuufanya Mkoa wa Mbeya kuwa kitovu cha mabadiliko.
Magufuli aliyewasili katika Uwanja wa Ndege wa Songwe, mkoani Mbeya saa tatu asubuhi na kuanza safari ya kwenda Mbarali, alisema hayo aliposimama katika eneo la Soweto na Uyole na kuzungumza na wananchi, wakiwamo wafuasi wa CCM na Chadema.
Miongoni mwa watu hao, wafuasi wa Chadema walikuwa wakimshangilia mgombea huyo kwa kuonyesha vidole viwili juu, huku wengine wakizungusha mikono kama ishara ya mabadiliko inayotumiwa na chama hicho na kuimba Lowassa! Lowassa! Lowassa!
Baada ya kuona hivyo, Dk Magufuli aliwaomba wana-Chadema hao wamchague ili afanye mabadiliko bila kujali itikadi za vyama vyao.
Alisema akichaguliwa kuwa rais ataufanyia mabadiliko mji wa Mbeya kuwa M4C, “Sasa itakuwa Mbeya for Change kuwa kituo cha mabadiliko”
“Nikiwa rais, nitakuwa rais wa wote, nitakuwa Rais wa CCM, CUF, Chadema na hata wasio na vyama.
“Chadema oyeeeee, people,s....” Dk Magufuli aliwasalimia wananchi hao kwa salamu inayotumiwa na Chadema, nao wakamwitikia kwa sauti ya juu, ‘power’.
Alisema anatambua kuwa Mbeya kuna wafuasi wa Chadema na kuwataka wafuasi hao kumpa kura ili awaletee maendeleo. Alisisitiza kuwa Serikali yake itahakikisha vijana wote wanapata ajira ili waweze kujitegemea.
“Chadema mnasema people’s power, basi mnipe hiyo power ili niwaletee maendeleo,” alisema mgombea huyo na kuendelea na safari yake kwenda Mbarali, eneo ambalo lilisalia wakati alipofanya ziara katika mkoa wa Mbeya kwa mara ya kwanza.
Mgombea ubunge wa jimbo la Mbarali, Haroon Primohamed alimwomba Dk Magufuli kutatua mgogoro wa ardhi uliopo katika eneo hilo na kushughulikia kwa haraka mgogoro kati ya wananchi wa vijiji 21 na Tanapa.
Malecela aibuka Mbarali
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela jana aliibukia katika Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya na kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli ili awe rais wa awamu ya tano.
Malecela ambaye pia ni makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, alisema wapinzani ni walaghai na wameshindwa katika uchaguzi wa miaka ya nyuma kutokana na kutokuwa na sera imara zenye mwelekeo wa kuwakomboa wananchi kutoka katika umaskini.
Aliwataka wakazi wa Mbarali kuichagua CCM ili kuwadhihirishia wapinzani kwamba CCM aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere bado iko imara na mwaka huu itashinda.
“Upinzani unaundwa na makundi mawili, kuna kundi la wapinzani tunaowafahamu na walioshindwa tangu mwaka 1992 na kundi la waasi na waroho wa madaraka waliotoka CCM. Wote hawa ni walaghai msiwachague,” alisema Malecela.
Alisisitiza kuwa Dk Magufuli ndiye aliyeshinda kwenye kura za maoni ndani ya CCM, lakini wenye uchu wa madaraka waliona wameonewa wakakihama chama.
“Mimi pia niliwahi kugombea urais, sikuchaguliwa. Lakini sijawahi kufikiria kukihama chama kwa sababu najua utaratibu,” alisema Malecela.
Mgogoro wa ardhi
Akihutubia wakazi hao, Dk Magufuli aliahidi kurudisha ekari 1,800 za ardhi alizopewa mwekezaji kinyume cha taratibu ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa mashamba ya Kapunga yaliyopo wilayani humo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Igulusi, Chimala na Rujewa, jimbo la Mbarali, Dk Magufuli alisema anaufahamu mgogoro huo ambao unamhusisha mwekezaji aliyepewa ekari 6,800 badala ya ekari 5,000 alizotakiwa kupewa.
“Ninaifahamu sheria ya vijiji, namba 5 ya mwaka 1999, ninaifahamu sheria ya ardhi, namba 4 ya 1999 na sheria ya matumizi bora ya ardhi ya mwaka 2007. Ninaomba mnichague niwe rais ili nimalize tatizo hili kwa sababu ardhi ni miliki ya rais, siwezi kushindwa,” alisema.
Mgombea huyo alisema aliyechelewesha mashamba hayo kurudishwa kwa wananchi ni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Modestus Kilufi kwa sababu alishindwa kusimamia kikamilifu mchakato wa kumaliza mgogoro huo.
Kilufi ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM, alikihama chama chake na kwenda ACT - Wazalendo. Anagombea ubunge tena katika jimbo la Mbarali kupitia chama chake kipya.
“Mbunge wenu ndiyo alikuwa kikwazo, akiambiwa peleka ‘document’ (nyaraka) wizara ya ardhi, yeye anakaa nazo. Safari hii msifanye makosa kumchagua tena, mchagueni Haroon Primohamed kwa sababu ni mchapakazi,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli ambaye baadaye alifanya mkutano Mafinga, mkoani Iringa aliwaomba wananchi wa Mbarali wamwamini kwa sababu anakusudia kumaliza matatizo ya ardhi nchini, pamoja na matatizo mengine yanayowakabili Watanzania.
“Nikiwa Rais sitawabagua watu, hizo bendera ni rangi tu, kwangu ni kazi tu,” alisema Dk Magufuli wakati akizungumza na wananchi wa Chimala, eneo lililokuwa na bendera za CCM na Chadema.
Katika mkutano wake rasmi uliofanyika Rujewa, Dk Magufuli aliwaambia wakazi wa eneo hilo kwamba atahakikisha pia vijiji 21 vilivyochukuliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwenye hifadhi ya Ruaha, vinabaki kwa wananchi.
“Mtu yoyote asiwasumbue wananchi wanaoishi kwenye vijiji 21 vilivyochukuliwa na Tanapa. Atakayethubutu kuwasumbua, nikichaguliwa kuwa Rais hana kazi,” alisisitiza mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi.
“Dk Magufuli ameniahidi kwamba akishinda urais atarudisha zile ekari zilizochukuliwa na mwekezaji. Ninawaomba mumchague ili amalize tatizo hili, nadhani mnajua jinsi alivyo mchapakazi,” alibainisha mgombea ubunge Primohamed.
Mkazi wa Rujewa, Augustino Mwambela aliiitaka Serikali kuboresha scheme za umwagiliaji ili waweze kuzalisha kwa wingi. Alisema wanazalisha kidogo kwa sababu maji kwa ajili ya kilimo cha mpunga bado ni tatizo.
“Tunaomba Magufuli atusaidie kupata mashamba yetu aliyopewa mwekezaji. Pia, kilimo cha umwagiliaji ni muhimu kwa sababu scheme tunazotumia hazina maji ya kutosha,” alisema mkulima huyo.
MWANANCHI
7 comments:
Kichwa habari hakiendani na halisi iyotokea
Mnaibeba sana CCM
Magufuli alizomewa tena sana Kama livyozomewa jk Dodoma na wajumbe WA CCM
Ilikuwa Lowassa Lowassa Lowassa
Alifyata Naye akasema chadema oyeeeeeeeeeeeeeeeee
Chezea nguvu ya umma
Mzee John Malechela una matatizo bora ukapumzike! Waachie wenye nafasi wafanye kazi.
Tanzania ya leo tunahitaji kiongozi anaefahamu nini maana ya siasa na upizani wake . Siasa sio uadui kama wanavyoichukulia watu wa chadema na ukawa. Hata hao wafuasi wa chadema wa mbeya walijipanga kwa ajili ya kufanya fujo lakini walishangazwa na ustaarabu wa magufuli . Kwa kiasi fulani walipigwa na butwaa sana kiasi kwamba kutoamini macho yao jinsi magufuli alivyobadilishana mawazo kwa njia ya amani kabisa. Magufuli ni msomi wa kiwango cha PHD ni mchapa kazi, mzalendo hasa kwa nchi yake kwa hivyo tunaimani watanzania tumepata mtu sahii wa kutuvusha katika safari yetu ya mabadiliko ya kweli.
Nyinyi jipeni matumaini tu kiboko yake mtakiona tarehe 10/25.
uozo ukizidi lazima uondoke.....kwahiyo ndiyo maano wanahama
Ushamba na uzanduki mliouonyesha kwenye msafara wa mgombea wa CCM umedhirisha kweli kuwa nyinyi siyo wanasiasa bali ni kundi la wahuni tu. Kwa mwelekeo kama huu sioni vipi wapiga kura watataka kupoteza muda wao adimu kwenda kuwapigieni kura. Wenzenu watakavyozidi kujijenga kwa wananchi kazi yenu itabaki kufanya fujo tu na kulalamika kuwa mnaonewa kumbe uozo uko ndani yenu ninyi wenyewe.
Unaweza kununu baadhi ya watu nasio chama chote,watu wenye tamaa ya pesa ndio walio mkalibisha hapo.itifaki haikufatwa na chadema.akiukosa uraisi patachimbika,si mbali tarehe 25/10.
Post a Comment