ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 10, 2015

FAHAMU URAFIKI WA GWAJIMA NA LOWASA SOMA HAPA LIVE!!


SASA NIMEELEWA KWA NINI LOWASSA, GWAJIMA NI MARAFIKI
NA LUQMAN MALOTO 
Jua lilikuwa limeshamezwa na mwangaza wa jioni ulikuwa unatoweka. Naam usiku ulikuwa unaingia. Abiria walikuwa wengi kuliko idadi ya daladala. Mimi nguvu sina, kwa hiyo nilijikalia pembeni nikitazama purukushani za wenye ubavu wao katika kugombea gari.
Mara ikaja bajaji, ikaita bukubuku. Nami kwa mikogo nikaenda kupanda. Nilijua huko hatutagombana, na kweli hatukupigana. Nilijiweka pembeni, wakapanda wengine wawili nyuma, mmoja akaungana na dereva mbele kisha safari ilianza.
Ukimya ulikuwa mkubwa mwanzoni mwa safari, muungurumo wa bajaji na magari yaliyokuwa yanatupita na mengine tukipishana nayo, ndiyo sauti pekee zilizokuwa zinatawala masikio yetu. Kila mmoja alikuwa anawaza la kwake.
Abiria aliyekuwa ameketi kushoto kabisa, yaani kwenye mlango wa kuingilia, alianza kuuliza: “Watu wa bajaji na bodaboda inaonekana ni waaminifu sana kwa Edward Lowassa”
Dereva wa bajaji akajibu: “Kinoma blaza, Mamvi ndiyo mpango mzima. Hapa huniambii kitu. Yule jamaa mchapakazi halafu ndiye kiboko ya uamuzi. Yule ndiye mzee wa maamuzi magumu. Hapa ukinikata damu inatoka Lowassa, nampenda yule jamaa mpaka kufa.”
Abria aliyekuwa amekaa katikati siti ya nyuma alisema: “Dereva unaongea sana, swali fupi jibu refu kweli. Ulipaswa tu kujibu ndiyo au hapana na jibu lingetosha.”
Mimi nilikuwa kimya, nikisikiliza mazungumzo. Nilipoinua macho mbele juu ya kichwa cha dereva, niliona kipeperushi chenye picha ya Lowassa na bendera ya Chadema, kilichoandikwa: “Lowassa Ulipo Tupo.”
Hapo nikajua kumbe sababu ya jamaa wa kwanza kuuliza lile swali ni baada ya kuona kile kipeperushi. Nilikaa kimya wakati wenye sauti zao wanaendelea kujibishana. Hofu yangu ni mimi kuingilia ubishi, wengine tuna damu mbaya. La mwingine litahamishiwa kwangu. Yangu yalikuwa macho tu!
Dereva wa bajaji akasema: “Blaza hii ndiyo staili yangu ya kuongea, usinipangie kabisa. Ukitaka kujua kama mimi ni mkorofi mseme vibaya Lowassa hapa kwenye bajaji yangu, nakutoza hela halafu nakushusha.”
Ule mkwara ulizidi kunifanya niufyate zaidi. Kushushwa tena kwenye bajaji! Dereva wa bajaji alionekana mbabe sana. Ila kweli ni mwenye mbavu nene, kifua kipana kama tembo. Alijidaia nguvu zake.
Pamoja na uoga ila nilichokoza: “Je, tukikuchangia?” 
Yule abiria wa mlangoni akaja juu: “Hakuna kumchangia wala nini, mimi mwenyewe namkabili halafu namshusha kwenye bajaji yake, naendesha mwenyewe.”
Dereva akasimamisha bajaji, akasema: “Anayejifanya mjanja ashuke, na kama wote mnaleta zenu za kuleta, wote pigeni chini. Siendeshi tena bajaji.”
Nikamuuliza dereva: “Kaka hata mimi TeamLowassa mwenzako?”
Dereva akasema: “Kumbe kuna TeamLowassa humu ndani, bahati yenu.” Akawasha bajaji safari ikaendelea.
Jamaa aliyeanzisha mazungumzo akaongea: “Tatizo lako dereva ni mapepe sana. Mimi mwenyewe ni TeamLowassa nashangaa swali dogo unapaniki. Nimekuuliza mnampenda Lowassa ili tuungane na rais wetu wana mabadiliko.”
“Aah, sorry blaza, ila kiukweli mimi kwa Lowassa nipo tayari kugombana na mtu yeyote. Nampenda sana yule jamaa. Kwanza ni mweupe halafu nywele zake dah! Atakuwa bonge la rais. Si unajua hata Nelson Mandela alikuwa na nywele nyeupe. Hata Mwalimu Nyerere alipozeeka alikuwa na nywele nyeupe kama Lowassa.”
Muda wote, yule jamaa aliyekuwa ameketi mbele na dereva alikuwa hajazungumza chochote. Kipindi abiria wengine tunakubaliana na dereva kuwa Lowassa ndiye rais anayewafaa Watanzania, ikabidi na yeye atie neno:
“Ila sasa hivi nimegundua sababu ya Lowassa na Gwajima kuwa marafiki.”
Sentensi ya abiria mwenzetu ilituchanganya kidogo. Tukawa kimya tukitafakari mantiki ya maneno yake. Dereva kwa mara nyingine akavunja ukimya kwa sauti ya juu.
Akasema: “Gwajima mzee wa maharage ya wapi! Mjinga mmoja, asiyefaa mmoja! Lazima awe rafiki wa mzee wa maamuzi magumu kwa sababu hata Gwajima naye ni noma, haogopi mtu. Wote marafiki wale, napenda urafiki wao.”
Abiria wa mbele akasema: “Wenyewe wanasema niambie rafiki yako nikujue wewe ni nani, sasa nakubali kuwa Gwajima na Lowassa ni marafiki.”
Binafsi niliona yule abiria mwenzangu ana kitu zaidi. Ikabidi nimuulize aweze kufafanua maana yake katika urafiki wa Gwajima na Lowassa. Naye akanijibu kwa kuniuliza:
“Unakumbuka kama Gwajima aliwahi kuutangazia umma wa Watanzania kuwa anataka kumfufua marehemu Amina Chifupa?”
Nikamuitikia kuwa nakumbuka halafu nikamtazama ili aendelee. Wakati huo dereva alikuwa akiendesha, abiria wengine walikuwa kimya. Wote tulitaka kusikiliza kitu kutoka kwa yule mwenzetu.
“Na unakumbuka kuwa Gwajima aliwahi kutangaza kuwa atamfufua aliyepata kuwa waziri mkuu maarufu kabisa hapa nchini Edward Moringe Sokoine?”
Kwa mara nyingine nikamuitikia yule abiria mwenzangu. Sikuishia hapo, nikatupa swali kwa wenzangu kama nao wanakumbuka au peke yangu ndiye niliyekuwa na kumbukumbu. Dereva akanijibu: 
“Gwajima noma blaza, kumbe aliwafufua hadi hao!”
Abiria wa katikati akamwambia dereva wa bajaji: “Hivi wewe wakati Amina Chifupa anafariki dunia wewe ulikuwa umeshakuja mjini? Usituletee maneno yako hapa, kama hujui kaa kimya.”
Dereva akawa mkali tena: “Halafu wewe blaza ndiyo maana muda ule nilitaka kuwashusha kwa sababu ya maneno yako ya jeuri. Safari hii nakushusha peke yako, wengine nawaacha.”
Ikabidi nimtulize kidogo dereva apunguze jazba, nilipofanikiwa hilo nilimgeukia yule abiria mwenzangu nikamuomba aendelee na habari yake ya urafiki wa Lowassa na Gwajima.
Yule abiria mwenzangu akaendelea: “Maana yangu inaonekana Lowassa na Gwajima wanapenda sana kufufua wafu. Si unaona sasa hivi Lowassa anatangaza kumleta nchini aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, marehemu Daud Balali?”
Katika wale abiria tuliokuwa kwenye bajaji, mimi ndiye nilikuwa kiherehere sana. Pengine ndiye nilikuwa namwelewa abiria mwenzangu kwa urahisi zaidi, kwa hiyo nilitaka apewe uwanja mkubwa zaidi aweze kufunguka.
Naye hakuwa na hiyana akasema: “Ndege wanaofanana huruka pamoja, kwa hiyo Gwajima na Lowassa wanafanana kwa mipango yao ya kimaisha. Hawa jamaa ni marafiki kwelikweli. Si unajua Gwajima aliwahi kufikishwa mpaka mahakamani kwa tabia yake ya kusema anafufua misukule?”
Alipokuwa anazungumza macho yake yalikuwa mbele lakini alipoweka kituo hapo, aligeuka na kutazama nyuma, macho yangu na yake yalikutana. Nikatikisa kichwa kama ishara kuwa namuelewa sana, nikamwambia aendelee:
“Gwajima alipokuwa anatangaza kuwa atamfufua Amina Chifupa na baadaye Sokoine, alikuwa na maana ya kutaka kupata wafuasi wengi kwenye kanisa lake la Ufufuo na Uzima. 
“Ukija kwa Lowassa na yeye amekuja na staili ya kutaka kumleta Balali ili apate kura nyingi za urais. Sasa hapa sijui, labda alipewa utaalam na rafiki yake Gwajima lakini kiukweli hawa jamaa wamekuwa na staili zinazofanana.”
“Dereva shusha hapo,” yule abiria wa katikati alimuomba dereva kuonesha kuwa yeye alikuwa amefika.
Wakati yule abiria anatoa pesa amlipe dereva wa bajaji akasema: “Kaka somo lako nimelielewa kuliko wote. Mimi naamini hata mawazo ya kumtoa Babu Seya yametokana na Gwajima. Mimi sijawahi kuona katika maisha yangu kuona mgombea urais ilani yake inakuwa kuwatoa jela wafungwa waliohukumiwa kwa mujibu wa sheria.”
Baada ya kulipa nauli, safari iliendelea, mpaka niliposhuka nilikuwa nimevuna maneno mengi ya maana kutoka kwa yule abiria wa mbele. Jambo ambalo nilisahau kumuuliza ni kuhusu chama chake na mgombea urais atakayempigia kura.
By Luqman Maloto

5 comments:

Anonymous said...

Nice ferry tell, kama lowassa anaongea kuwafufua wafu na kuwaachia wahalifu ni sera au maneno yake. Swali la msingi kama unakereketwa na hayo maneno ni kumkabili yeye na kumuuliza kwa nini na vipi atafanya hivyo. Kwa uhakika atakuwa na majibu ya hoja zake. Sasa kuyakubali au kuyakataa majibu yake itabaki ni uamuzi wako wewe binafsi.
Story nzuri ila haiisaidii himaya iliyo kwenye utawala sasa hivi kubaki hapo walipo baada ya October 25.
Balali kutoweka kwake ilikuwa ni kuficha udhalimu au ubadhirifu mkubwa wa pesa za umma ulofanywa wakati Kikwete anaelekea kuchukua urais, ama kwa babu seya, sheria haikutumika kwa uwazi na haki, mahakama ilitakiwa ipate ushahidi usio na shaka hata kidogo ili kumuhukumu kifungo cha maisha seya na watoto wake. Kifungo chake kina shinikizo la mtu binafsi mwenye nguvu/madaraka nchini hivyo seya hakutendewa haki. Sehemu ndogo tu ya point hii ni pale mahakama ilipo amua kumuachia huru mtoto wa mwisho wa seya for tbe instructions or sense of guilty ya mshinikizaji wa seya's family na kuendelea kuwakandamiza seya na papii jela. Hii si habari inayo hitaji kuwa na nguvu za utume kuijua.
Kama lowassa atawapa haki ya kusikilizwa tena seya na walofungwa wengine kwa sababu za kidhalimu na si kuvunja sheria atakuwa ndio amewapa haki watu hao na amesimamia rule of law. (utawala wa sheria) sio shinikizo. Similar story will be kwa wale mashehe wa Zanzibar.

Anonymous said...

The comment is too long to read.

Anonymous said...

Ferry tell ndio mnyama gani? There's no such thing as ferry tell in the English language! Kwa nini unachombeza vimaneno vya Kingereza wakati hujui hata vina maana gani?

Anonymous said...

Yameandikwa maneno ya maana. Yanawashika ninyi mliopewa kazi ya kubana nanihii zenu kwa imani EL hatatoboa on October 25.
Kazi mnayo, hakikisheni tu mmeweka appointments kumuona urologist wenu next day baada ya uchaguzi kwa kuwa hali za nanihii zenu hazitakuwa nzuri kwa kuzibana kila ukweli wa EL kutoboa unapo andikwa.

Anonymous said...

Cha ajabu kitu gani mbona JK ana marafiki waganga