Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia
moja ya jiwe lenye Madini huku akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa
Kampuni ya Aifola Investiment Co. Ltd, Zubery Mabie, kuhusu upatikanaji
wa madini na utengenezaji wa Unga wa 'Lime Powder', wakati Makamu
alipokuwa akitembelea Mabanda ya maonesho kwenye ufunguzi wa Kongamano
la Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, lililofanyika leo Sept 9, 2015 kwenye
Hoteli ya Tanganyika Mjini Kigoma.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wauza Samaki wa
Mapambo, Nunu Mrisho, kuhusu upatikanaji wa Samaki hao na soko lake ,
wakati Makamu alipokuwa akitembelea Mabanda ya maonesho kwenye ufunguzi
wa Kongamano la Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, lililofanyika leo Sept 9,
2015 kwenye Hoteli ya Tanganyika Mjini Kigoma.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akihutubia wakati akifungua rasmi Kongamano la Uwekezaji wa Ziwa
Tanganyika, lililofanyika leo Sept 9, 2015 kwenye Hoteli ya Tanganyika
Mjini Kigoma.
Sehemu
ya washiriki wa Kongamano hilo wakimsikiliza Makamu wa Rais Dkt. Bilal,
alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa Kongamano hilo.
Mwakilishi wa Umoja wa wafanyabishara wa Burundi, akizungumza.
Waziri
wa Nchi- Uwekezaji na Uwezeshaji, Eng. Christopher Chiza, akizungumza
kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu wa Rais Dkt. Bilal ili
kufungua Kongamano hilo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Balozi
waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9,
2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Makatibu Wakuu
waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9,
2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Viongozi wa
Halmashauri wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma waliohudhuria Kongamano hilo
baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Kamati ya Ulinzi
na Usalama wa Mkoa wa Kigoma waliohudhuria Kongamano hilo baada ya
ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na baadhi ya
washiriki wa Kongamano hilo waliohudhuria Kongamano hilo baada ya
ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015. Picha na OMR
HOTUBA YA MHE.
DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA
RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO
LA
UWEKEZAJI UKANDA WA ZIWA TANGANYIKA TAREHE 09 SEPTEMBA 2015
Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania;
Mhe. Eng. Cristopher Chiza
Waziri wa Nchi - Uwekezaji na
Uwezeshaji;
Waheshimiwa Mawaziri;
Wakuu wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na
Kigoma;
Waheshimiwa Mabalozi;
Washiriki;
Wageni Waalikwa;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote napenda kushukuru
kupata fursa ya kushiriki nanyi kwenye Kongamano hili, linaloangazia fursa za
uwekezaji na utanuaji maendeleo kwa ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Nimefurahi
kuwa nanyi hapa Kigoma na nafarijika zaidi kuona namna mlivyojitokeza katika
kongamano hili ukilinganisha na lile lililofanyika mwaka jana mjini Sumbawanga
ambapo pia nilipata fursa ya kuhudhuria.
Pili, napenda kuchukua fursa hii
kuwashukuru wenyeji wetu kwa mapokezi mazuri. Nimefurahishwa na maandalizi
mazuri ya Kongamano hili kwenye mazingira mazuri ambayo yanaonesha umakini
katika uandaaji. Nadhani washiriki wote mtakubaliana nami kwenye hili. Asanteni
sana.
Ninawashukuru pia Mabalozi kutoka
nchi mbalimbali walioshiriki. Hali kadhalika nawashukuru wageni wetu kutoka
nchi za nje kama vile Marekani, Jumuiya ya Ulaya na Burundi. Na washiriki wengine kutoka taasisi na sehemu
mbalimbali kwa kushiriki Kongamano letu, hii inadhihirisha umuhimu wa shughuli
yenyewe na inatuhakikishia mafanikio chanya siku zijazo.
Tatu, napenda kuwashukuru Wananchi
wa Kigoma na hasa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
Lt. Col. (Mst.) Issa S. Machibya kwa
ukarimu wao na kukubali kutupokea kwenye Kongamano hili. Ni ukweli ulio dhahiri
kwamba Kongamano hili kufanyika katika mkoa wenu ni mafanikio makubwa ya
kuutangaza mji wenu Kigoma/Ujiji.
Waheshimiwa,
Mabibi
na Mabwana;
Katika msafara wangu nimefuatana na
Maafisa kadhaa Waandamizi wa Serikali ambao wako hapa kusikiliza, kuzungumza na
kuchangia hoja mbali mbali kwenye sekta ya Uwekezaji na Mazingira ya Biashara
katika Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Ninawaomba washiriki wote kuitumia fursa
hiyo ya kupata habari muhimu wakiwa hapa ili kufanikisha malengo yenu ya
Uwekezaji katika Ukanda huu.
Ninaelewa baadaye mtapata fursa ya
kufanya mazungumzo ya mtu mmoja mmoja na wenzenu kutoka Ukanda huu. Mtapata
maelezo ya kutosha kuhusu fursa za Uwekezaji nchini na maelezo kutoka kwa
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZA) kuhusu
fursa na mazingira ya biashara katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Hali hiyo
itaifanya kazi yangu iwe rahisi. Nachukua fursa hii kuwaeleza kwa kifupi kwa nini
Ukanda huu ni eneo muhimu la kimkakati kwa uwekezaji nchini.
Waheshimiwa,
Mabibi
na Mabwana;
Ukanda wa Ziwa Tanganyika
unajumuisha mikoa mitatu (Rukwa, Kigoma na Katavi), sina shaka ukanda huu ni
mahali muafaka pa kuwekeza katika nchi yetu. Ukanda huu ulikuwa nyuma
kimaendeleo kwa miaka mingi na ukombali na Makao makuu ya nchi Dodoma na hata kutoka
kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.
Miundombinu ya usafiri wa Barabara,
Reli, Maji na Anga ulikuwa hafifu hali ambayo iliathiri kwa kiasi kikubwa
maendelo ya ukanda huu. Lakini kwa sasa Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa
kwenye Barabara, Viwanja vya ndege, Bandari na Reli, hivyo kuufanya Ukanda huu ufunguke.
Uboreshaji wa miundombinu ya
barabara kwa kiwango cha lami unaendelea, ujenzi wa barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, kutoka Sumbawanga hadi
Kasanga kupitia Matai, kutoka Sumbawanga hadi Tabora kupitia Namanyere na Mpanda,
pia barabara ya Mpanda hadi Tabora kupitia Koga, kutoka daraja la Mto Malagarasi
hadi Tabora kupitia Kaliua na Urambo, kutoka Mpanda kupitia Uvinza hadi Kanyani,
Wilaya ya Kasulu. Barabara kutoka Kigoma hadi mpaka wa Burundi na kutoka Kigoma
kupitia Kidahwe hadi Uvinza.
Ukamilikaji wa barabara hizo unaufanya
ukanda huu ufunguke na kuwezesha kufikika kwa urahisi kutoka kwenye miji
mikubwa ya Mbeya, Dar es salaam na Dodoma, na pia kwa nchi jirani za Afrika ya Kati na Kusini kama vile Malawi,
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Rwanda, Burundi na Afrika
ya Kusini. Hali ya maji kwa sasa inaridhisha, umeme upo wa kutosha kwa matumizi
ya nyumbani hata hivyo kuna juhudi mbalimbali kuuongeza ukidhi kwenye shughuli
za viwanda. Sehemu za Mkoa wa Rukwa zimeunganishwa na Shirika la Umeme la
Zambia “Zambian Electricity Supply Company (ZESCO)”. Kwa upande wa Kigoma na
Katavi bado wanatumia umeme wa jenereta hata hivyo kuna juhudi za ujenzi wa
umeme wa jua katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kuunganisha na umeme wa gridi
ya Taifa kutokea Tabora.
Waheshimiwa,
Mabibi
na Mabwana;
Ninaweza kuendelea tena na tena
kuelezea fursa na hatua zilizochukuliwa na Serikali. Lakini ni vyema kusema tu
kuwa kwa sasa mazingira ya biashara yameboreshwa sana na yameanza kuvutia
wawekezaji wengi kiasi kwamba shughuli za uwekezaji zimeongezeka kwenye sekta
za Kilimo, Madini na Umeme katika kipindi cha miaka mine iliyopita.
Kuna wawekezaji ambao wanasema kuwa
ukanda huu ni eneo ambalo wawekezaji wanaliangalia kwa jicho la kimkakati kwa
sasa. Hii inatokana na ukweli kuwa madini mengi yanapatikana katika Ukanda huu
kama vile Dhahabu, Nickel, Makaa ya Mawe, Chokaa, Shaba na Madini ya Vito.
Hivyo mtu anaweza kuchagua eneo lo lote analopenda katika ukanda huu ambao una
watu wapatao 3,697,073 kutokana na sensa ya mwaka 2012. Kulingana na takwimu za
Shirika la Takwimu za mwaka 2013 pato la mkaaji wa ukanda huu anapata wastani wa Tshs. 910,963 kwa mwaka.
Uanzishwaji wa Eneo Maalum la
Kiuchumi Kigoma (Kigoma Special Economic Zone “KiSEZ”) ni hatua nyingine ya
Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji katika viwanda, biashara na
huduma za kiuchumi katika “kuunganisha fursa zilizopo na masoko ya ndani na nje
ya nchi”. Hali hiyo imelenga katika kuufanya mji wa Kigoma/Ujiji kuwa kituo
kikuu cha biashara katika eneo la Maziwa Makuu. Kuwekeza kwenye eneo hili
kunamfanya mwekezaji kupata faida ya kiushindani katika shughuli za viwanda na biashara kwenye
eneo lote la Maziwa Makuu.
Waheshimiwa;
Mabibi
na Mabwana;
Kwa sasa napenda kuwakaribisha nyote
na biashara zenu kuwekeza katika Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Kuna fursa
nyingi ambazo watoa mada watabainisha na mtapata fursa ya kuwasiliana mmoja
mmoja na kila Mkoa au kila Halmashauri au kila Mfanyabiashara.
Ukanda unategemea zaidi kilimo na
zaidi mazao ya chakula kama vile mpunga, ndizi, mahindi, viazi, maharage, na
karanga ambapo mazao ya biashara ni kahawa, tumbaku, alizeti, mawese. Mazao
hayo ndiyo yanaendesha maisha ya watu wa ukanda huu shughuli zingine ni uvuvi na
biashara. Hata hivyo kilimo ni cha hali ya chini sambamba na uvuvi. Ninawaalika
kuwekeza kwenye eneo hilo kuboresha sekta ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi.
Ukanda huu umejaliwa mito na maziwa yenye maji baridi na safi, hivyo
umwagiliaji unaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Nimesikia kuna baadhi yenu mnataka
kuwekeza kwenye nishati, ninawakaribisha. Kama nilivyosema hapo awali Ukanda
huu unahitaji umeme mwingi zaidi ili kuweza kuimarisha sekta ya viwanda hasa
viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo na uvuvi.
Waheshimiwa;
Mabibi
na Mabwana;
Ninafahamu kuwa baadhi yenu mnataka
kuwekeza kwenye utalii. Ukanda huu bado haujapiga hatua nzuri kwenye sekta ya
utalii, hivyo ni fursa nzuri kwa sasa kuwekeza kwani hili ni eneo lililojaliwa
aina mbali mbali ya wanyamapori wanaopatikana kwenye mbuga na maeneo mengine ya
hifadhi kama vile Hifadhi za Taifa za Mahale, Gombe na Katavi au pori la
Moyowosi na Ugalla. Katika mbuga hizo kuna wanyama kama vile tembo, twiga,
mamba, nyati, kiboko na sokwe mtu. Aidha, kuna ndege na mimea ya aina yake.
Wawekezaji wanaweza kuwekeza kwenye hoteli na
huduma mbali mbali za kitalii.
Kama nilivyosema awali, eneo la
viwanda ni muhimu kuangaliwa kwa mapana yake, ukanda huu una maliasili nyingi
kama vile madini na mazao mbali mbali. Hali hiyo inaufanya Ukanda uwe na mali
ghafi ya kusaidia kuanzishwa kwa viwanda vya uchakataji wa mazao mbali mbali
kama vile mazao ya alizeti, mchikichi, mahindi, mpunga, mazao ya mifugo na
madini.
Waheshimiwa;
Mabibi
na Mabwana;
Tanzania kwa sasa inatoa huduma bora
za kiushindani kupitia sheria mbali mbali kama vile sheria ya Uwekezaji ya
mwaka 1997, sheria ya Maeneo Uchakataji kwa ajili ya kuuza nje ya mwaka 2002,
sheria ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya mwaka 2006, sheria ya Madini ya mwaka 1998
na sheria ya mafuta ya Nishati ya mwaka 1981.
Serikali imejikita katika kutekeleza
Mpango wa Kuboresha na Kuimarisha Mazingira ya Biashara (Business Environment
Strengthening for Tanzania “BEST”). Lengo kubwa la mradi huo ambao ulianza Desemba,
2003, ni kupunguza urasimu wa Serikali na kuboresha huduma kwa sekta binafsi
ikiwemo na mashauri ya kibiashara.
Tanzania ni nchi inayotoa motisha
nzuri kwa wawekezaji. Pengine ni moja ya nchi zinazotoa motisha bora kuliko
nchi nyingi katika Afrika. Nina imani kuwa Wakurugenzi wa Maeneo Maalum ya
Kiuchumi (EPZA) na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Nchini watakuwa wako hapa
pamoja nasi. Nina hakika watazungumza kwa kina kwenye mawasilisho yao kuhusu
jambo hilo.
Ni dhahiri kuwa, Ukanda wa Ziwa
Tanganyika ndiyo lango kwa nchi nne zinazopakana na Ukanda huo. Ukanda huu unatoa
njia fupi ambayo ni ya asili kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Rwanda, Burundi, na Zambia. Hivyo kuwekeza katika Ukanda huu unatoa fursa ya kuyafikia
masoko ya nchi hizo kwa urahisi zaidi.
Waheshimiwa;
Mabibi
na Mabwana;
Nimezungumza kwa kirefu kuliko
nilivyotarajia. Naomba nihitimishe kwa kusema yafuatayo. Kwanza, Ukanda wa Ziwa
Tanganyika uko tayari kufanya biashara nanyi. Pili, katika ukanda huu kuna kila
kitu kinachohitajika katika uwekezaji: mazingira mazuri ya biashara, hali ya
amani na utulivu, serikali inayojali wawekezaji, mali asili, wafanyakazi
wanaojituma, soko la kutosha, hali nzauri ya kijiografia na kadhalika.
Lakini, kitu cha muhimu, kuwepo
kwangu na kuwepo kwa Waziri Mkuu na Serikali yote kwa ujumla ni kuwahakikishia
kuwa tuko makini na tumejipanga kikamilifu kufanya biashara nanyi. Serikali hii
ni ya kuwawezesha wadau na imedhamiria katika “kuunganisha fursa zilizopo na
masoko ya ndani na nje ya nchi” kama kauli mbiyu ya kongamano inavyosema.
Ninaimani kuwa hakuna sababu ya
kusita kuwekeza na kufanya biashara katika Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika.
Ninawashukuru sana na ninawatakia mafanikio
katika mazungumzo yenu. Karibuni sana Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
ASANTENI
KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake