ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 9, 2015

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AFUNGUA KONGAMANO LA UWEKEZAJI UKANDA WA ZIWA TANGANYIKA, MJINI KIGOMA LEO.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia moja ya jiwe lenye Madini huku akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Aifola Investiment Co. Ltd, Zubery Mabie, kuhusu upatikanaji wa madini na utengenezaji wa Unga wa 'Lime Powder', wakati Makamu alipokuwa akitembelea Mabanda ya maonesho kwenye ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, lililofanyika leo Sept 9, 2015 kwenye Hoteli ya Tanganyika Mjini Kigoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wauza Samaki wa Mapambo, Nunu Mrisho, kuhusu upatikanaji wa Samaki hao na soko lake , wakati Makamu alipokuwa akitembelea Mabanda ya maonesho kwenye ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, lililofanyika leo Sept 9, 2015 kwenye Hoteli ya Tanganyika Mjini Kigoma.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati akifungua rasmi Kongamano la Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, lililofanyika leo Sept 9, 2015 kwenye Hoteli ya Tanganyika Mjini Kigoma.
 Sehemu ya washiriki wa Kongamano hilo wakimsikiliza Makamu wa Rais Dkt. Bilal, alipokuwa akihutubia kwenye ufunguzi wa Kongamano hilo.
 Mwakilishi wa Umoja wa wafanyabishara wa Burundi, akizungumza.
 Waziri wa Nchi- Uwekezaji na Uwezeshaji, Eng. Christopher Chiza, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu wa Rais Dkt. Bilal ili kufungua Kongamano hilo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Balozi waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Makatibu Wakuu waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Viongozi wa Halmashauri wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Kigoma waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo waliohudhuria Kongamano hilo baada ya ufunguzi, uliofanyika leo Sept 9, 2015. Picha na OMR



HOTUBA YA MHE. Top of Form

Bottom of Form
DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO
LA UWEKEZAJI UKANDA WA ZIWA TANGANYIKA TAREHE 09 SEPTEMBA 2015
 

Mhe.  Mizengo Kayanza Peter Pinda
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mhe. Eng. Cristopher Chiza
Waziri wa Nchi - Uwekezaji na Uwezeshaji;

Waheshimiwa Mawaziri;

Wakuu wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma;

Waheshimiwa Mabalozi;

Washiriki;

Wageni Waalikwa;

Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana;

Awali ya yote napenda kushukuru kupata fursa ya kushiriki nanyi kwenye Kongamano hili, linaloangazia fursa za uwekezaji na utanuaji maendeleo kwa ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Nimefurahi kuwa nanyi hapa Kigoma na nafarijika zaidi kuona namna mlivyojitokeza katika kongamano hili ukilinganisha na lile lililofanyika mwaka jana mjini Sumbawanga ambapo pia nilipata fursa ya kuhudhuria.

Pili, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wenyeji wetu kwa mapokezi mazuri. Nimefurahishwa na maandalizi mazuri ya Kongamano hili kwenye mazingira mazuri ambayo yanaonesha umakini katika uandaaji. Nadhani washiriki wote mtakubaliana nami kwenye hili. Asanteni sana.

Ninawashukuru pia Mabalozi kutoka nchi mbalimbali walioshiriki. Hali kadhalika nawashukuru wageni wetu kutoka nchi za nje kama vile Marekani, Jumuiya ya Ulaya na Burundi.  Na washiriki wengine kutoka taasisi na sehemu mbalimbali kwa kushiriki Kongamano letu, hii inadhihirisha umuhimu wa shughuli yenyewe na inatuhakikishia mafanikio chanya siku zijazo.

Tatu, napenda kuwashukuru Wananchi wa Kigoma na hasa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma  Lt. Col. (Mst.) Issa S. Machibya  kwa ukarimu wao na kukubali kutupokea kwenye Kongamano hili. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba Kongamano hili kufanyika katika mkoa wenu ni mafanikio makubwa ya kuutangaza mji wenu Kigoma/Ujiji.




Waheshimiwa,
Mabibi na Mabwana;
Katika msafara wangu nimefuatana na Maafisa kadhaa Waandamizi wa Serikali ambao wako hapa kusikiliza, kuzungumza na kuchangia hoja mbali mbali kwenye sekta ya Uwekezaji na Mazingira ya Biashara katika Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Ninawaomba washiriki wote kuitumia fursa hiyo ya kupata habari muhimu wakiwa hapa ili kufanikisha malengo yenu ya Uwekezaji katika Ukanda huu.

Ninaelewa baadaye mtapata fursa ya kufanya mazungumzo ya mtu mmoja mmoja na wenzenu kutoka Ukanda huu. Mtapata maelezo ya kutosha kuhusu fursa za Uwekezaji nchini na maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZA) kuhusu fursa na mazingira ya biashara katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Hali hiyo itaifanya kazi yangu iwe rahisi. Nachukua fursa hii kuwaeleza kwa kifupi kwa nini Ukanda huu ni eneo muhimu la kimkakati kwa uwekezaji nchini.

Waheshimiwa,
Mabibi na Mabwana;
Ukanda wa Ziwa Tanganyika unajumuisha mikoa mitatu (Rukwa, Kigoma na Katavi), sina shaka ukanda huu ni mahali muafaka pa kuwekeza katika nchi yetu. Ukanda huu ulikuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi na ukombali na Makao makuu ya nchi Dodoma na hata kutoka kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.
 
Miundombinu ya usafiri wa Barabara, Reli, Maji na Anga ulikuwa hafifu hali ambayo iliathiri kwa kiasi kikubwa maendelo ya ukanda huu. Lakini kwa sasa Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye Barabara, Viwanja vya ndege, Bandari na Reli, hivyo kuufanya Ukanda huu ufunguke.

Uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami unaendelea, ujenzi wa barabara ya  Tunduma hadi Sumbawanga, kutoka Sumbawanga hadi Kasanga kupitia Matai, kutoka Sumbawanga hadi Tabora kupitia Namanyere na Mpanda, pia barabara ya Mpanda hadi Tabora kupitia Koga, kutoka daraja la Mto Malagarasi hadi Tabora kupitia Kaliua na Urambo, kutoka Mpanda kupitia Uvinza hadi Kanyani, Wilaya ya Kasulu. Barabara kutoka Kigoma hadi mpaka wa Burundi na kutoka Kigoma kupitia Kidahwe hadi Uvinza.

Ukamilikaji wa barabara hizo unaufanya ukanda huu ufunguke na kuwezesha kufikika kwa urahisi kutoka kwenye miji mikubwa ya Mbeya, Dar es salaam na Dodoma, na pia kwa nchi jirani za  Afrika ya Kati na Kusini kama vile Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Rwanda, Burundi na Afrika ya Kusini. Hali ya maji kwa sasa inaridhisha, umeme upo wa kutosha kwa matumizi ya nyumbani hata hivyo kuna juhudi mbalimbali kuuongeza ukidhi kwenye shughuli za viwanda. Sehemu za Mkoa wa Rukwa zimeunganishwa na Shirika la Umeme la Zambia “Zambian Electricity Supply Company (ZESCO)”. Kwa upande wa Kigoma na Katavi bado wanatumia umeme wa jenereta hata hivyo kuna juhudi za ujenzi wa umeme wa jua katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kuunganisha na umeme wa gridi ya Taifa kutokea Tabora.





Waheshimiwa,
Mabibi na Mabwana;
Ninaweza kuendelea tena na tena kuelezea fursa na hatua zilizochukuliwa na Serikali. Lakini ni vyema kusema tu kuwa kwa sasa mazingira ya biashara yameboreshwa sana na yameanza kuvutia wawekezaji wengi kiasi kwamba shughuli za uwekezaji zimeongezeka kwenye sekta za Kilimo, Madini na Umeme katika kipindi cha miaka mine iliyopita. 

Kuna wawekezaji ambao wanasema kuwa ukanda huu ni eneo ambalo wawekezaji wanaliangalia kwa jicho la kimkakati kwa sasa. Hii inatokana na ukweli kuwa madini mengi yanapatikana katika Ukanda huu kama vile Dhahabu, Nickel, Makaa ya Mawe, Chokaa, Shaba na Madini ya Vito. Hivyo mtu anaweza kuchagua eneo lo lote analopenda katika ukanda huu ambao una watu wapatao 3,697,073 kutokana na sensa ya mwaka 2012. Kulingana na takwimu za Shirika la Takwimu za mwaka 2013 pato la mkaaji wa ukanda huu anapata wastani wa Tshs. 910,963 kwa mwaka.

Uanzishwaji wa Eneo Maalum la Kiuchumi Kigoma (Kigoma Special Economic Zone “KiSEZ”) ni hatua nyingine ya Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji katika viwanda, biashara na huduma za kiuchumi katika “kuunganisha fursa zilizopo na masoko ya ndani na nje ya nchi”. Hali hiyo imelenga katika kuufanya mji wa Kigoma/Ujiji kuwa kituo kikuu cha biashara katika eneo la Maziwa Makuu. Kuwekeza kwenye eneo hili kunamfanya mwekezaji kupata faida ya kiushindani  katika shughuli za viwanda na biashara kwenye eneo lote la Maziwa Makuu.

Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Kwa sasa napenda kuwakaribisha nyote na biashara zenu kuwekeza katika Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Kuna fursa nyingi ambazo watoa mada watabainisha na mtapata fursa ya kuwasiliana mmoja mmoja na kila Mkoa au kila Halmashauri au kila Mfanyabiashara.

Ukanda unategemea zaidi kilimo na zaidi mazao ya chakula kama vile mpunga, ndizi, mahindi, viazi, maharage, na karanga ambapo mazao ya biashara ni kahawa, tumbaku, alizeti, mawese. Mazao hayo ndiyo yanaendesha maisha ya watu wa ukanda huu shughuli zingine ni uvuvi na biashara. Hata hivyo kilimo ni cha hali ya chini sambamba na uvuvi. Ninawaalika kuwekeza kwenye eneo hilo kuboresha sekta ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi. Ukanda huu umejaliwa mito na maziwa yenye maji baridi na safi, hivyo umwagiliaji unaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Nimesikia kuna baadhi yenu mnataka kuwekeza kwenye nishati, ninawakaribisha. Kama nilivyosema hapo awali Ukanda huu unahitaji umeme mwingi zaidi ili kuweza kuimarisha sekta ya viwanda hasa viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo na uvuvi.

Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Ninafahamu kuwa baadhi yenu mnataka kuwekeza kwenye utalii. Ukanda huu bado haujapiga hatua nzuri kwenye sekta ya utalii, hivyo ni fursa nzuri kwa sasa kuwekeza kwani hili ni eneo lililojaliwa aina mbali mbali ya wanyamapori wanaopatikana kwenye mbuga na maeneo mengine ya hifadhi kama vile Hifadhi za Taifa za Mahale, Gombe na Katavi au pori la Moyowosi na Ugalla. Katika mbuga hizo kuna wanyama kama vile tembo, twiga, mamba, nyati, kiboko na sokwe mtu. Aidha, kuna ndege na mimea ya aina yake. Wawekezaji wanaweza kuwekeza kwenye hoteli na  huduma mbali mbali za kitalii.

Kama nilivyosema awali, eneo la viwanda ni muhimu kuangaliwa kwa mapana yake, ukanda huu una maliasili nyingi kama vile madini na mazao mbali mbali. Hali hiyo inaufanya Ukanda uwe na mali ghafi ya kusaidia kuanzishwa kwa viwanda vya uchakataji wa mazao mbali mbali kama vile mazao ya alizeti, mchikichi, mahindi, mpunga, mazao ya mifugo na madini.  

Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Tanzania kwa sasa inatoa huduma bora za kiushindani kupitia sheria mbali mbali kama vile sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997, sheria ya Maeneo Uchakataji kwa ajili ya kuuza nje ya mwaka 2002, sheria ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya mwaka 2006, sheria ya Madini ya mwaka 1998 na sheria ya mafuta ya Nishati ya mwaka 1981.

Serikali imejikita katika kutekeleza Mpango wa Kuboresha na Kuimarisha Mazingira ya Biashara (Business Environment Strengthening for Tanzania “BEST”). Lengo kubwa la mradi huo ambao ulianza Desemba, 2003, ni kupunguza urasimu wa Serikali na kuboresha huduma kwa sekta binafsi ikiwemo na mashauri ya kibiashara.

Tanzania ni nchi inayotoa motisha nzuri kwa wawekezaji. Pengine ni moja ya nchi zinazotoa motisha bora kuliko nchi nyingi katika Afrika. Nina imani kuwa Wakurugenzi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZA) na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Nchini watakuwa wako hapa pamoja nasi. Nina hakika watazungumza kwa kina kwenye mawasilisho yao kuhusu jambo hilo.

Ni dhahiri kuwa, Ukanda wa Ziwa Tanganyika ndiyo lango kwa nchi nne zinazopakana na Ukanda huo. Ukanda huu unatoa njia fupi ambayo ni ya asili kwa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, na Zambia. Hivyo kuwekeza katika Ukanda huu unatoa fursa ya kuyafikia masoko ya nchi hizo kwa urahisi zaidi.

Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Nimezungumza kwa kirefu kuliko nilivyotarajia. Naomba nihitimishe kwa kusema yafuatayo. Kwanza, Ukanda wa Ziwa Tanganyika uko tayari kufanya biashara nanyi. Pili, katika ukanda huu kuna kila kitu kinachohitajika katika uwekezaji: mazingira mazuri ya biashara, hali ya amani na utulivu, serikali inayojali wawekezaji, mali asili, wafanyakazi wanaojituma, soko la kutosha, hali nzauri ya kijiografia na kadhalika.

Lakini, kitu cha muhimu, kuwepo kwangu na kuwepo kwa Waziri Mkuu na Serikali yote kwa ujumla ni kuwahakikishia kuwa tuko makini na tumejipanga kikamilifu kufanya biashara nanyi. Serikali hii ni ya kuwawezesha wadau na imedhamiria katika  “kuunganisha fursa zilizopo na masoko ya ndani na nje ya nchi” kama kauli mbiyu ya kongamano inavyosema.
Ninaimani kuwa hakuna sababu ya kusita kuwekeza na kufanya biashara katika Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika.

Ninawashukuru sana na ninawatakia mafanikio katika mazungumzo yenu. Karibuni sana Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
 

No comments: