ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 10, 2015

Simba yakwea pipa 'kukwepa ndumba'

Kikosi cha Simba kinatarajia kutua Tanga leo kwa usafiri wa ndege kwa ajili ya mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya African Sports, huku uvumi wa imani za kishirikina ukikizunguka.

Simba itawavaa African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jumamosi, ikitokea moja kwa moja Unguja, Zanzibar ilikokuwa imeweka kambi.

Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, maamuzi ya kuisafirisha timu hiyo kwa kutumia usafiri wa anga, ni kwa lengo la kukwepa ‘juju’ kutoka kwa wapinzani wao.

Imedaiwa kuwa ‘wataalamu’ wa Simba wamebaini kuwa kushindwa kupata ushindi kwa miaka minne kwenye Uwanja wa Mkwakwani kunatokana na uchawi wanaowekewa katika daraja la Mto Wami, ambao huwanasa wachezaji kila wanapopita katika daraja hilo lililosifika zamani kwa kuwa na mamba wengi.

“Watatukosa mwaka huu, wao watatusubiri njiapanda, sisi tunapita angani,” alisema mtu wa ndani wa Simba ambaye jina lake tunalihifadhi.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Muingereza, Dylan Kerr, ambaye haamini “mambo hayo”, alisema juzi kwamba kikosi chake kimepanga kufanya vizuri katika msimu ujao na kazi hiyo ataianza keshokutwa kwa kusaka ushindi wa ugenini.
Kerr alisema kwamba amejipanga kuanza kwa kuweka historia ya kuwafunga wenyeji ambao wamerejea Ligi Kuu msimu huu.

Kerr akiwa na msaidizi wake, Selemani Matola, wameiongoza timu hiyo katika mechi 12 za kirafiki huku mbili zikiwa za kimataifa na kati ya hizo wameshinda 10, kipigo kimoja na sare moja.

Baada ya mechi ya Jumamosi, Simba itabaki jijini humo kwa ajili ya kusubiri mechi yake ya pili dhidi ya Mgambo Shooting itakayofanyika Jumatano Septemba 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani pia.

REKODI MBOVU
Simba imekuwa na rekodi mbovu kwenye Uwanja wa Mkwakwani ikiwa haijafunga goli lolote tangu 2011. Tangu wakati huo Wekundu wa Msimbazi hawajawahi kushinda kwenye uwanja huo na wamekuwa wakiambulia sare na vipigo tu.

Mchezaji wa mwisho wa Simba kufunga goli Mkwakwani ni marehemu Patrick Mafisango alipofanya hivyo Agosti 24, 2011, akifunga goli dakika ya 24 lililoipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Ligi Kuu msimu wa 2011/12. Kiungo huyo Mkongomani aliyechukua uraia wa Rwanda alifariki dunia miezi tisa baadaye kwa ajali ya gari Mei 17, 2012 jijini Dar es Salaam.

Tangu wakati huo, si kwamba tu haijashinda tena kwenye uwanja huo, bali hakuna mchezaji yoyote wa timu hiyo aliyefunga goli Mkwakwani.

Rekodi za Simba kwenye uwanja wa Mkwakwani zinaonyesha kuwa msimu wa 2012/13 ilitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal, pia dhidi ya Mgambo Shooting.

Msimu wa 2013/14 ilitoka tena bila kufungana dhidi ya Coastal, lakini ikatandikwa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting.

Msimu uliomalizika wa 2014/15 ilitoka sare pia ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union, lakini ikaambulia kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting.
CHANZO: NIPASHE

No comments: