ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 23, 2015

Simba, Yanga za karne ya 21.

Tangu 2000, Simba imeifunga Yanga mara 11, Yanga ikishinda mechi tano tu, huku wachezaji waliowahi kufunga mabao katika mechi kati ya miamba hao waliosalia vikosini humo ni watatu tu.
Wakati mechi ya watani wa jadi ikitarajiwa kuchezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu ya Simba inaongoza kwa kuifunga Yanga mara nyingi zaidi kwenye karne ya 21.

Kwa mujibu wa rekodi zetu tangu kuingia mwaka 2000, Simba imeifunga Yanga mara 11, sare mara 15, huku Yanga ikishinda mechi tano tu.

Rekodi hizi hazijahusisha mechi za kirafiki, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Kagame au Nani Mtani Jembe. Ni mechi za Ligi Kuu tu.

Tangu kuingia kwa karne mpya, Simba na Yanga zimekutana mara 31 kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mechi hizo zote jumla ya magoli 61 yamefungwa, Simba ikiwa imefunga magoli 35 dhidi ya 26 ya Yanga.

Kuelekea pambano hilo, wafungaji magoli kwenye mechi hizo za watani waliobaki wanazichezea timu hizo ni watatu tu, Simon Msuva wa Yanga na Mussa Hassan Mgosi na Hamisi Kiiza wa Simba.

Wengine waliopata 'kutupia' mabao katika mechi hiyo inayovuta hisia za nchi nzima, ama amezihama timu hizo, wamekwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi huku baadhi yao wamestaafu soka.

Hata hivyo, kati ya watatu hao, Kiiza ataichezea timu pinzani ya Simba badala ya Yanga aliyokuwa akiichezea huko nyuma, huku Mgosi na Msuva wakiwa kwenye klabu zao zilezile za zamani.

Takwimu zinaonyesha kuwa wachezaji wanaoongoza kwa kufunga magoli mengi kwenye mipambano hiyo ya karne ya 21 ya watani wa jadi ni Mgosi na Jerry Tegete ambao wamepachika magoli manne kila mmoja.

Kati ya magoli hayo waliyofunga kila mmoja, mawili walifunga kwenye mechi moja iliyochezwa Aprili 18, 2010 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-3.

Katika mechi hiyo, Mgosi alifunga magoli mawili dakika ya 53 na 74, Tegete akifunga dakika ya 69 na 89.

Mgosi ana nafasi ya kuboresha rekodi yake ya kufunga katika mechi ya watani Jumamosi, wakati Tegete ameshaihama timu hiyo ya Jangwani na kutua Mwadui FC.

Wachezaji wanaofuatia kwa kupachika magoli mengi kwenye mechi hizo za watani wa jadi tangu iingie karne ya 21 ambao wamefunga magoli matatu kila mmoja ni Idd Moshi (Yanga), Mganda Kiiza na Mganda Emmanuel Okwi.

Kiiza amehamia upande wa Simba na kuifanya timu hiyo kuingia uwanjani ikiwa na mastraika wawili wenye na rekodi ya kufunga magoli mengi kwenye mechi hizo akiwa na Mgosi.

Tangu kuingia kwa karne ya 21, Yanga imechukua ubingwa wa Tanzania Bara mara nyingi zaidi (8) kuliko wapinzani wao, Simba, waliotwaa taji hilo mara sita.

Kwa ujumla tangu mwaka 1965 ligi hiyo ya juu zadi nchini ilipoanzishwa, Yanga ndiyo inayoshikilia rekodi ya kuutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara nyingi zaidi ikiubeba mara 25, ikifuatiwa na Simba iliyoutwaa mara 18.

Wachezaji wachezaji ambao wameshazichezea klabu zote mbili ambazo wanaweza kucheza Jumamosi hii ni Ali Mustapha 'Barthez', Kelvin Yondani na Amisi Tambwe wa Yanga, pamoja na Hamis Kiiza wa Simba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: