BAADA ya kutoweka hadharani tangu Julai 28, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amejitokeza hadharani na kuelezea kilichomsibu, akiweka wazi kwamba amestaafu siasa baada ya chama hicho kumpokea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye amesisitiza hawezi kukwepa kashfa ya Richmond.
Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliodumu kwa takribani saa mbili katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam jana kuwa Lowassa si kiongozi anayefaa kuwa rais wa nchi kutokana na kuhusika na vitendo vya rushwa na kwamba ni mhusika namba moja katika kashfa ya Richmond, iliyomwondoa madarakani Februari 2008. Tangu Julai 28, wakati Lowassa alipoanza kuonekana katika vikao vya Chadema, Dk Slaa amekuwa haonekani katika vikao vya chama hicho ikiwemo Mkutano Mkuu uliomtangaza Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho na umoja wa wapinzani (Ukawa) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Mbali ya Mkutano Mkuu, Dk Slaa hakuonekana katika matukio muhimu kama yale ya Lowassa kufika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya kugombea urais na wakati wa kuirejesha, na pia katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni kwenye Viwanja vya Jangwani, Agosti 29, mwaka huu.
Katika mkutano wa jana, Dk Slaa alieleza kwa kirefu kilichotokea na kumfanya kupotea katika harakati za Chadema huku akiweka wazi kuwa ujio wa Lowassa ulimfanya ajiuzulu nafasi ya Ukatibu Mkuu, tofauti na madai ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kwamba alikuwa likizo. “Nimejitokeza leo, mimi sikuwa likizo.
Mengi yamesemwa na viongozi wangu, lakini ukweli ni kwamba sikupewa likizo na yeyote, nasisitiza sina barua yoyote ya likizo. “Kilichotokea ni kwamba niliamua kuachana na siasa tangu tarehe 28/7 majira ya saa 3 usiku, baada ya kuona yanayofanyika ndani ya chama changu na sikukubaliana nayo,” alisema Dk Slaa na kuongeza: “Wapo watu wanaosema Dk Slaa alishiriki kutoka mwanzo katika ujio wa Lowassa.
Nilishiriki kweli, lakini niliweka msingi tangu dakika ya kwanza kutaka kujua Lowassa anakuja Chadema kama mali au anakuja kama mzigo? Msimamo wangu huu haukupatiwa majibu na hadi sasa viongozi wa Chadema hawana majibu katika hili.”
Akisimulia mkasa mzima, padri huyo wa zamani wa Kanisa Katoliki alisema baada ya Lowassa kukatwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM mjini Dodoma, alipigiwa simu na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aliyemwita kuwa mshenga wa Lowassa, akimuarifu hatua hiyo ya kukatwa Lowassa ni mtaji kwa Chadema.
Alisema katika maelekezo yake, Askofu Gwajima alimuelekeza Dk Slaa awasiliane na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe kuhusu mpango huo na kumrejeshea majibu ya kile walichoafikiana na kwamba alitekeleza ombi hilo kwa kuwasiliana na Mbowe na baadaye walimkaribisha Askofu Gwajima ili kuzungumza kwa kina.
“Tangu wakati huo niliweka msimamo wangu. Unajua kwa kawaida ni vizuri kumsikia mtu ana nini na si kutomsikiliza kabisa. Chadema ni chama cha siasa haikatazwi kumpokea mtu. “Niliweka msimamo kwanza atangaze kutoka ndani ya CCM, baada ya kutangaza hilo atangaze pia ni chama gani anakwenda, halafu tatu atumie nafasi hiyo kujisafisha na tuhuma zake anazoshutumiwa.
Niliweka msimamo huo kwa kuamini kuwa Chadema ni chama kilichojijenga katika misingi ya uadilifu na iwapo asingefanya hivyo ni hatari,” alifafanua Dk Slaa aliyegombea urais kwa chama hicho mwaka 2010. Alisema kinyume cha msimamo aliouweka, Lowassa hakutangaza kujitoa CCM na kutangaza anakwenda chama gani kwa wakati huo, lakini pia hakujisafisha hadi alipokuwa katika kikao cha utambulisho Chadema ndipo alipozungumzia suala la Richmond baada ya kuulizwa na waandishi wa habari tena katika hali ya udikteta.
Alisema mbali ya msimamo huo, aliweka msimamo mwingine wa kutaka kujua, Lowassa anakwenda Chadema akiwa ni mali au mzigo, katika kile alichosema ilikuwa ni kutaka kutathmini kama ujio huo wa Lowassa kwa Chadema ungekuwa na manufaa au hasara. “Ujue kwenye biashara au siasa, anayejiunga leo ni lazima mfahamu, je, anakuja kama mali au kama mzigo?
Watu hapa wanasema nilipatwa na hasira kwa vile alipewa nafasi ya kugombea urais, suala si urais, hadi siku hiyo nilikuwa sijachukua fomu ya urais, kama ningekuwa nataka urais ningetangaza au kuchukua fomu kwani jina langu lilishapitishwa na vikao tangu Februari. “Hapa ukweli ni kwamba Slaa alikuwa anataka mgombea mwenye uwezo, sifa na anayeweza kuivusha Chadema kuiondoa CCM.
Hata mwaka 2010 sikujitokeza mimi kugombea urais, bali niliombwa. Urais si wangu, mimi binafsi ni kwa ajili ya watu,” alieleza akifafanua madai hayo ya kuwa alikasirika kwa kutoteuliwa kuwania urais. Alisema kutokana na swali hilo, alijibiwa kwamba Lowassa angekwenda Chadema na wabunge 50 waliokuwa wakimaliza muda wao, wenyeviti wa CCM wa mikoa 22, wenyeviti wa CCM wa wilaya 88, na hivyo aliamini kama ingekuwa hivyo nchi ingeweza kutetemeka.
“Niliweka sharti majina yatajwe, nilifanya vile kwa kuwa Katibu Mkuu makini wa chama hawezi kupokea tu watu, bila kujua ni akina nani na wanagombea wapi maana tulikuwa tayari na mfumo wa kuwaandaa wagombea ndani ya chama, hata hivyo majina hayo sikuyapata. Alisema ilipofika Julai 25, kilifanyika kikao ambacho aliagizwa kuitisha kikao cha Halmashauri Kuu na alipohoji nini kinaenda kuzungumzwa, hakupewa jibu.
Alisema Julai 25, alipigiwa simu na Mbowe ambapo katika mazungumzo yao kwa mara ya kwanza walitofautiana, ingawa alikubali kufika katika kikao alichowakuta Mbowe, Askofu Gwajima na Mwanasheria wao, Tundu Lissu. “Kikao kile kilianza saa 3 asubuhi hadi saa 9 jioni, na tulibishana sana, maana swali langu lilibakia kuwa lile lile, je Lowassa anakuja Chadema kama mali au kama mzigo?
Baada ya pale walisema twende nyumbani kwa Lowassa, lakini nilikataa kwani Lowassa ni mwanachama wa CCM hivyo mimi nisingeweza kwenda. “Tulirejea tena katika kikao kuanzia saa 9 jioni hadi saa 12.30, tukapumzika, lakini hatukuelewana. Wakaunda kamati ndogo ya kuzungumza na mimi na kunishauri, lakini nilikataa. Pale pale niliandika barua ya kujiuzulu nikampa Mwenyekiti wa kikao, Profesa Safari (Abdalah) lakini aliichana pale pale.
“Sikuridhika na hatua hiyo niliandika barua nyingine na kumkabidhi Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar ambaye alinijibu kwamba Dk Slaa unajisumbua bure haya mambo yamepangwa. Hata hivyo, kesho yake niliandika barua rasmi ya kujizulu,” alieleza kiongozi huyo aliyeheshimika kwa misimamo yake ndani ya Chadema.
Akizungumzia nini kilifuata baada ya Lowassa kupokelewa Chadema; alisema alikwenda kama mzigo na si mali kwani yeye na wafuasi wake ni watu ambao ama walikataliwa na wananchi katika kura za maoni, au ni ambao wamekuwa wakituhumiwa katika masuala ya ufisadi na hawawezi kukubalika ndani ya jamii.
“Awali niliweka msimamo kwamba wale watakaokuja na Lowassa ni vizuri waje kabla ya kufanyika kura ya maoni, hilo halikuzingatiwa. Dk Mahanga (Makongoro, aliyekuwa Mbunge wa Ukonga na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira) huyo ni mali au ni mzigo? Huyo amekataliwa na wananchi hivyo alikuwa anatafuta kichaka cha kujificha. “Hivi Sumaye (Frederick, Waziri Mkuu mstaafu) huyo ni mtu safi kweli. Watu wote wanamfahamu kwamba ni fisadi.
Nilimwita fisadi ndani ya Bunge wakati ule alipopokonya shamba la Magereza Kibaigwa. “Huyu Sumaye ndiye ambaye alisema CCM ikimteua Lowassa atahama chama. Watu wote mnajua Sumaye alikuwa anaitwa nani wakati ule… (kicheko). Leo makapi yametoka CCM yamekwenda Chadema.
Wenyeviti waliondoka ni mizigo, wote tunamjua Msindai (Mgana, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM). “Mimi namfahamu Msindai, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali kabla yangu pale Bungeni alichokifanya ipo siku nitamuweka hadharani.
Mtu ambaye siwezi kumsema ni Mgeja (Khamis, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga)… huyo siwezi kumsema maana simfahamu,” alieleza Dk Slaa. “Kuna mtu anaitwa Chizi, hivi Chizi ni nani? Nilipofuatilia ili kumjua vizuri nikaambiwa eti alikuwa anapanga mipango ya wizi wa kura ndani ya CCM.
Yaani Chadema inampokea mtu kwa vile tu alikuwa mwizi wa kura? Kama tunataka Chadema kuiba kura kuna umuhimu gani wa kuiondoa CCM madarakani? Unaiondoa CCM kwa programu safi serious (makini) na watu serious (makini).”
Kuhusu Richmond, Dk Slaa alisema bado anaamini kuwa Lowassa hawezi kukwepa kashfa hiyo na alionesha na kusoma vielelezo na barua mbalimbali, alizosema zinadhihirisha Lowassa kuwa mpangaji mkuu wa mpango wa ufisadi wa Richmond na kwamba kupokelewa na Chadema, kumekifanya chama hicho kupoteza nguvu ya hoja ya kupambana na ufisadi, hoja aliyosema ilikuwa silaha pekee kwa Chadema.
Dk Slaa alimtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani, kujitokeza na kueleza namna alivyohusika na sakata la Richmond, kwa kutaja Richmond ilikuwa kampuni ya nani, na ni wakubwa gani walioshinikiza kutolewa kwa zabuni hiyo ya kufua umeme wa dharura kama alivyodai na kuahidi kutoa taarifa zaidi ya umma kwa suala hilo.
Habari Leo
8 comments:
Akihojiwa na redio station mh.Lissu anasema ameshangaa sana maneno aliyoyasema leo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.
Anasema Dr.Slaa alikwisha kuteuliwa kuwa mgombea urais mwezi January na mwezi April akathibitishwa na kamati kuu,
Anaendelea kusema ameshangaa Dr.Slaa kusema Gwajima ndo alimleta Lowassa jambo ambalo siyo kweli kabisa, yeye Dr. Slaa mwezi wa tano ndo alianza kumtafuta Lowassa kwa kumtumia Gwajima
Anasema wakati Lowassa anapokelewa tarehe 27 July kwenye Kamati Kuu, Dr.Slaa hakulala nyumbani aliporudi nyumbani mchumba wake alimtupia mabegi nje na DR. alilala kwenye gari.
Anasema dr. slaa asiwadanganye watanzania tatizo ni urais na mchumba wake.
Anasema ameacha siasa tangu siku ya kikao cha kamati kuu alipoandika barua ya kujiudhuru kwa nini amepokea mshahara wa mwezi huu?? kwanini anaendelea kutumia gari la chama la katibu mkuu na nyumba aliyonunuliwa na chama muulizeni awaambie kwanini anaendelea kunufaika na hayo yote toka CHADEMA??
Jamani unafiki huo. Double standard. Kashindwa kupitishwa na UKAWA sasa hana la kufanya zaidi ya kubakia sukari ya ccm kwa pembeni. Ushauri wangu kwa huyu babu, just go back and serve the Lord achana na siasa usiyoiweza. UKAWA will remain strong without you. He's trying to get attention by the forces of ccm. UKAWA don't pay attention to this guy.
Watumishi,mrudieni Mungu!hatuhitaji kujua sana but why you?chagueni Mungu ama kaisali!
Huyo Tundu Lisu ni mnafiki mkubwa yupo pale chadema akiongoza idara ya upotoshaji kwa uma wa watanzania hivyo kweli yupo mtu makini anaamini anachokisema Tundu Lisu? Hivyo kweli ushafika wakati sisi watanzania tunaamini wanacho kisema wanasiasa kuliko watu mungu? Anachokisema Dk slaa ni ukweli wa asilimia mia moja 100% na alicho kizungumza Tundu Lisu kuhusu Dk slaa ni uwongo wa asilimia mia moja 100%.
Si kila anae elimishwa huelimika.
Mungu mkubwa huyu babu angekuwa rais tungekuwa tunaongozwa na mkewe, ingekuwa balaa tu.shetani kweli anahangaika sana kama yeye ni mtakatifu mke wa pili amemtoa wapi? People made their mind they don't listen to his rubbish. Good luck saint bishop
“Nimeamua kujitokeza leo hii ili kukomesha upotoshaji na kuuweka wazi ukweli.Sina tabia ya kuyumbishwa na ninasimamia ninachokiamini”Dr. Slaa. Ni haki yake ya kikatiba na ya msingi kueleza anachokiamini. I respect this guy. Leo hii tunasahau huyu mzee ndiyo alikuwa mpiganaji mkubwa kwa upande wa opposition,kisa kaongea anachokiamini. Acheni kuwa wakosefu wa fadhila na kufuata siasa za ushabiki. Pia tukumbuke kuna maisha baada ya October 25, atayechaguliwa atatuongoza kama raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania si wa chama hiki wala kile
Dr Slaa alitaka yeye kuwa Rais. Kweli Big Ego
Post a Comment