ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 25, 2015

Utafiti Ukawa 76% mwingine Dk. Magufuli 62%.

Siku mbili baada ya ripoti ya utafiti uliofanywa na Twaweza kwa njia ya simu kuonyesha kuwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli angeshinda kwa asilimia 66, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umetangaza matokeo ya utafiti wao yanayompa mgombea wao kupitia Chadema, Edward Lowassa, ushindi wa zaidi ya asilimia 76.

Hata hivyo, vita kuhusiana na ripoti za utafiti baina ya CCM na Ukawa imechukua sura mpya baada ya utafiti mwingine kutangazwa kupitia taarifa zilizosambazwa kwenye vyombo vya habari jana ukionyesha kuwa Dk. Magufuli atashinda kwa asilimia 62 dhidi ya wagombea wengine akiwamo Lowassa anayetajwa kuwa atavuna asilimia 31 ya kura.

Utafiti wa Twaweza uliohusisha watu 1,848 na kupondwa vikali na baadhi ya wasomi na wanaharakati mbalimbali, ulifanyika kati ya Agosti 19 na Septemba 7, mwaka huu na kumpa Lowassa nafasi ya pili nyuma ya Magufuli kwa asilimia 25 huku Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo akipata asilimia 3. Ripoti hiyo ilidai kuwa asilimia saba ya kura ni za wapiga kura waliosema hawajui watampigia nani. Ukawa unaundwa na Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.

UTAFITI WA UKAWA
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema utafiti uliotolewa na Twaweza una kasoro nyingi za kiufundi na umejaa prapaganda zenye lengo la kuibeba CCM.

Mbatia alisema kuwa utafiti wao wa ndani (Ukawa) uliofanywa na wataalam kutoka nje ya nchi unaonyesha kuwa Lowassa atashinda kwa asilimia 74 huku wataalamu wa ndani wakitoa matokeo yanayompa Lowassa ushindi mwingine wa kishindo wa asilimia 76.

“Upo pia utafiti uliofanywa kupitia mitandao ya simu na kuonyesha kuwa Lowassa atashinda kwa asilimia 79,” alisema Mbatia.

Kwa mchanganuo huo, kwa mujibu wa Ukawa, Lowassa atashinda kwa wastani wa asilimia 76.3.

Mbatia alisema wataalam hao walifanya utafiti huo baada ya Lowassa ameshajiunga na umoja huo.

Mbatia alisema utafiti wa Twaweza umejaa kasoro nyingi zikiwamo za kulinganisha zaidi wagombea wawili tu wa urais wa CCM na Chadema na kuwaacha wagombea wengine, wakiwamo Hashim Rungwe wa Chaumma, Fahmy Dovutwa (UPDP), Janken Kasambala (NRA), Macmillan Lyimo (TLP) na Chifu Lutasola Yemba (ADC).

Kadhalika, alisema utafiti huo wa Twaweza umeeleza kuwa ulikuwa wa kitaifa wakati ukweli ni kwamba ni sehemu moja ya Tanzania Bara badala ya Jamhuri ya Muungano ambayo Zanzibar ni sehemu yake, lakini haikuhusishwa kabisa.

Aliongeza kuwa katika utafiti huo, Twaweza wameshindwa kujua uchaguzi mkuu unapaswa kutoa wabunge au madiwani wangapi.

“Taarifa ya Twaweza imejaa propaganda za kisiasa kwa ajili ya manufaa ya Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu, lakini bila ya kufahamu kwamba propaganda hizo zimeishia kuidhalilisha taasisi ya Twaweza na CCM,” alisema Mbatia.

Mbatia alisema picha moja iliyowekwa kwenye taarifa ya wagombea nane wa urais inaonyesha kutokuwapo utaratibu wa kuzingatia usawa wa binadamu, hivyo kudhalilisha baadhi ya wagombea.

Kadhalika, Mbatia alisema katika kielelezo cha tisa ya utafiti huo kinaonyesha udhaifu mkubwa wa kimahesabu.

Alifafanua kuwa ukijumlisha asilimia za Lowassa kwa wima, jumla yake ni 27% na asilimia 73 ya wahojiwa katika kumchagua Lowassa havikujumuishwa katika kielelezo hicho, pamoja na wahojiwa kutoa maoni kuhusu sera za wagombea urais kabla hazijatolewa.

ABAINISHA KASORO
Mbatia alisema waliotafitiwa walipewa simu za bure na watoa utafiti, watafiti kuielezea Ukawa ni chama cha siasa, kupotosha maana halisi ya Ukawa kwa kuuita “Walinzi wa Katiba ya Wananchi.”

“Ukirejea ukurasa wa 11, aya ya kwanza wamepotosha maana halisi ya Ukawa, pia hata ukurasa wa kwanza wanasema Ukawa ni chama cha siasa,” anasema Mbatia.

Kasoro nyingine ni kutokuthamini kwa usawa michango ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi mkuu, huku mtiririko wa vyama ukiwa haujapangwa vizuri.

Nyingine ni kuorodhesha vyama visivyokuwa na wagombea urais katika swali la kuchagua rais, kwa mfano CUF na NCCR-Mageuzi katika ukurasa wa saba.

Alisema kulikuwapo na kauli zilizokinzana, majumuisho ya utafiti hayaendani na maswali ya utafiti, jumla ya asilimia kutofikia asilimia 100.

PROF. BAREGU

Mshauri wa masuala ya ufundi wa Ukawa, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Twaweza miezi ya hivi karibuni waliwahi kufanya utafiti wa urais uliomuonyesha Lowassa (akiwa CCM) akiongoza kwa 13%, akifuatiwa na Mizengo Pinda (12%), wa tatu ni Dk. Willibrod Slaa wa Chadema (11%), Ibrahim Lipumba (6%) na Dk. John Magufuli (3%).

Profesa Baregu alihoji iweje mgombea huyo huyo aliyeongoza akiwa CCM aanguke kwa asilimia kubwa baada ya kuhama CCM na kujiunga Chadema.

Mbatia alisema wanawaalika Twaweza katika mdahalo wa kutetea taarifa yao ambao unapaswa kuwahusisha wataalamu wenye kufanya tafiti kwa kutumia takwimu na wawakilishi kutoka kila chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi mkuu.

Aidha, Mbatia aliwataka Watanzania wote kutotilia maanani utafiti huo wa Twaweza na kuendelea kuikuza na kulinda amani ya nchi kama mboni ya jicho kwa kukataa kusikiliza propaganda za kuvuruga uchaguzi mkuu Oktoba 25.

MAGUFULI ANG'ARA TENA
Katika ripoti ya utafiti wa Ipsos ambayo Nipashe inayo nakala yake, Magufuli anaonekana kung’ara kwa kuelezwa kuwa atashinda kwa asilimia 62 dhidi ya 31 za Lowassa baada ya watu 1,836 kuhojiwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara kati ya Septemba 5 hadi Septemba 22, 2015. Mgombea wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amepata asilimia 0.3 huku asilimia saba ya wapiga kura wakiwa hawajui watampigia kura mgombea yupi miongoni wa wagombea urais kwenye uchaguzi huo.

Mwakilishi Mkazi wa Ipsos nchini, Charles Makau, alisema utafiti huo haukuhusisha wananchi wa Zanzibar kutokana na sheria zilizopo visiwani humo kuhusiana na masuala ya utafiti.

“Utafiti ulifuata vigezo vyote vya kisayansi ingawa hatusemi kwamba haya ndiyo matokeo yatakayotokea baada ya upigaji kura wa Oktoba 25 mwaka huu,” alisema Makau.

KERO 5 KWA WANANCHI
Katika hatua nyingine, Makau alisema utafiti wa Ipsos ulibaini kero tano kwa Watanzania ambazo ni bei kubwa za vyakula, mafuta na gharama kubwa za kuishi; maji, elimu, masuala ya afya, chakula na njaa.

Alisema katika sifa mahususi za wagombea urais, wananchi walitoa maoni yao yanayoeleza ni nani wanadhani anaweza kutatua kero kuu zinazowakabili.

Magufuli ameonekana kuaminika zaidi katika eneo la miundombinu kwa asilimia 44 dhidi ya Lowassa asilimia 26. Aidha, Lowassa ameonekana kumzidi Magufuli katika eneo la vita dhidi ya rushwa kwa kupata asilimia 27 ya waliohojiwa dhidi ya asilimia 26 za Magufuli.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Ni ajabu kuona wasomi kama akina Mbatia, Profesa Baregu wanapoteza muda adimu wa kufanya kampeni ku address issues za opinion polls.
Hii ni sawa na pilot kushusha ndege ili ashughulikie nzi anaemsumbua kwenye cockpit.
Fanyeni kampeni, msitafute visingizio mfu.Wengine vyama vinawafia mikononi lkn.kila siku mko kujibu trivial issues kwenye media.

Anonymous said...

Hapo safi tumerithika na nafsi zetu

Anonymous said...

Kumbuka huu ni utafiti wa hasira wa ukawa wa kujibu mapigo ya matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi huru ya utafiti ya taweza. Huu utafiti wa ukawa utawaharimu kwani mficha maradhi kifo kinamchngulia.