ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 2, 2015

Ahadi 5 za Kikwete zigo kwa rais ajaye.


Rais Jakaya Kikwete.

Wakati zikiwa zimebaki siku 22 kuanzia leo kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, imebainika kuwa Rais ajaye atakuwa na mzigo mzito wa kutekeleza ahadi kadhaa zilizowahi kutolewa na serikali ya Rais Jakaya Kikwete anayetarajiwa kumaliza muda wake baada ya uchaguzi huo utakaompata mrithi wake.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa, licha ya mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali katika kipindi cha miaka 10 ya serikali iliyopo madarakani, bado kuna ahadi tano kubwa ambazo ni miongoni mwa zile zinazoonekana wazi kuwa utekelezaji wake utahitaji muujiza kutokana na muda mfupi uliobaki kati ya sasa na siku ya kupiga kura.

Kwa sababu hiyo, imebainika kuwa Rais ajaye atalazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa walau anatekeleza ahadi hizo na hivyo kufufua matumaini waliyokuwa nayo wananchi kwa kipindi chote tangu wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

Hadi sasa, wagombea wanaoonekana kuchuana vikali katika kampeni zinazoendelea ni Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF). 

Wagombea wengine wanaotafuta ridhaa ya Watanzania katika uchaguzi mkuu wa tano tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 ni Fahmy Dovutwa wa UPDP, Hashim Rungwe wa Chama cha Umma (Chaumma), Maximillian Lymo wa TLP, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Chifu Lutasola Yemba wa ADC na Janken Kasambala wa NRA. 

Kadhalika, imebainika kuwa yeyote ayakayeshinda kati ya wagombea hao wa urais, hasa Dk. Magufuli wa CCM na Lowassa wa Ukawa wanaoonekana kuchuana kwa karibu kutokana na maelfu ya watu wanaojitokeza kwenye mikutano yao kila uchao, atakabiliana na mtihani mzito wa kutekeleza ahadi hizo. 

Uchunguzi umebaini kuwa Rais ajaye kutoka miongoni mwa wagombea nane wanaoendelea na kampeni hivi sasa, atakuwa na kazi ya kutekeleza ahadi zake binafsi na zilizotolewa katika ilani za chama chake na pia atakuwa na kibarua kizito cha kuangalia ni kwa namna gani atatekeleza ahadi zilizowahi kutolewa na Rais Kikwete kwa nyakati tofauti kabla na baada ya chaguzi zilizoiingiza serikali ya sasa madarakani.

Ahadi tano kubwa kati ya zile zilizowahi kutolewa na serikali ya Rais Kikwete ni pamoja na ununuzi wa meli katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa; ununuzi wa bajaji maalum za kubebea wagonjwa katika hospitali; kuimarishwa kwa mgodi wa makaa ya mawe Kiwira ili mwishowe usaidie kuzalisha umeme; ujenzi wa reli mpya ya kati na pia kumalizwa tatizo la maji katika maeneo kadhaa nchini ikiwamo katika Jimbo la Nzega mkoani Tabora. 


1. KIGOMA KUWA DUBAI YA AFRIKA
Serikali ya Rais Kikwete iliahidi kuwa itaubadilisha Mkoa wa Kigoma na kuwa Dubai ya Afrika kwa maana kuwa wa kibiashara kama ilivyo Dubai kwa kujenga uwanja wa ndege, kupanua bandari na kuimarisha reli ili kuhudumia nchi za maziwa makuu na za kusini mwa Afrika.

2. AFYA (BAJAJ KUBEBEA WAGONJWA)
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, Rais Kikwete alitoa ahadi ya kununua pikipiki za miguu mitatu (bajaj) 400 za wagonjwa kwa nchi nzima.

Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Mkwajuni wilayani Chunya mkoa wa Mbeya.

Ahadi hiyo itakuwa mtihani mzito kwa Rais ajaye ambaye atatakiwa kuitekeleza kwa kuwa baadhi ya maeneo, hususani ya vijijini, bado yanaendelea kukabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa magari ya kubebea wagonjwa ili kuwawahisha kwenye hospitali kubwa. Waathirika wakubwa wa tatizo hili huwa ni kina mama wajawazito, hivyo ni mtihani wa aina yake.

3. UJENZI WA 'FLY-OVERS'
Miongoni mwa ahadi maarufu za serikali ya awamu ya nne ni ujenzi wa barabara za juu (fly-overs) kwenye makutano ya barabara kubwa za jiji la Dar es Salaam kama Mandela/Nyerere na Mandela/Morogoro, lengo likiwa ni kupunguza makali ya foleni. Licha ya ahadi hii kurudiwa mara kadhaa, bado haijatekelezwa hadi sasa. 

Rais ajaye atalazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa inatekelezwa ili kutimiza kiu ya maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliojawa na matumaini waliyopewa na serikali yao ya sasa kwa kuamini kuwa hilo likifanyika, adha wanayoipata ya kutumia muda mwingi wakiwa kwenye foleni za magari itapungua kwa kiasi kikubwa.

4. UJENZI RELI YA KATI
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2010, Rais Kikwete akiwa wilayani Nzega, mkoani Tabora, aliahidi kuwa serikali yake ingejenga reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Aidha, akizungumza na wananchi wa wilaya ya Pangani, mkoani Tanga Septemba 10, mwaka 2010, aliahidi pia kujenga reli kutoka Tanga kwenda Arusha hadi Musoma.

Hata hivyo, hadi kufikia sasa hakuna utekelezaji wa kuonekana kwa vitendo katika kutimiza azma hiyo ya kuwa na reli mpya. Kwa sababu hiyo, Rais ajaye na serikali yake watalazimika kuifanyia kazi ahadi hii ili kuboresha sekta ya uchukuzi wa reli hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

5. AHADI YA MELI ZIWA VICTORIA, TANGANYIKA
Hii ni ahadi mojawapo maarufu ambayo bado haijatekelezwa na kuna kila dalili kuwa haitatekelezwa katika kipindi kilichobaki, hivyo kumpa mtihani wa aina yake rais ajaye. 

Katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010, Rais Kikwete alitoa ahadi ya kununua meli kubwa kuliko ya Mv Bukoba iliyozama mwaka 1996. Alitoa ahadi hiyo Agosti 24, mwaka 2010 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bukoba Vijijini. 

Aidha, katika mkutano wake Bukoba Vijijini, Rais Kikwete aliahidi pia kujenga uwanja wa ndege ili kuwarahisishia usafiri wananchi wa mkoa wa Kagera. 

Akiwa katika wilaya ya Nkasi, mkoa wa Rukwa Agosti 28, 2010, Rais Kikwete aliahidi kuwa serikali yake itanunua meli mpya itakayokuwa inatoa huduma katika Ziwa Tanganyika. 

Aliahidi pia kununua meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400 katika Ziwa Nyasa. Hadi sasa hilo halijafanyika.

Mrithi wa Rais Kikwete katika serikali ijayo ya awamu ya tano, atalazimika kuumiza kichwa na serikali yake ili kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine, ahadi hii pia inatimizwa. 

AHADI NYINGINE
Ahadi nyingine zilizowahi kutolewa na Rais Kikwete na ambazo utekelezaji wake bado haujafanyika ni pamoja na ya kuwapelekea kivuko wakazi wa Buchosa mkoani Mwanza. Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo Agosti 23, 2010, Rais Kikwete aliahidi kununua kivuko cha Maisome ili kuwaondolea adha wananchi wanaotaka kuvuka kwenda maeneo mengine. Hilo hadi sasa halijafanyika na hivyo rais ajaye atakuwa na kazi ya ziada kutekeleza.

Zipo pia ahadi nyingine kadhaa zilizoibua matumaini mapya kwa Watanzania lakini hadi sasa utekelezaji wake haujafanyika kwa asilimia mia moja. Baadhi ya ahadi hizo ni ujenzi wa barabara za pembezoni (ring roads) jijini Dar es Salaam, kukamilisha katiba mpya, kumaliza madai ya walimu, uraia wa nchi mbili, kuufanya mji wa Tanga kuwa wa viwanda na pia kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira.

MAFANIKIO SERIKALI YA JK 
Licha ya changamoto zilizopo, serikali ya awamu ya nne imefanikiwa katika maeneo kadhaa yaliyotokana na ahadi zilizotolewa wakati wa chaguzi zilizopita, hivyo kumpa kibarua cha ziada rais ajaye katika kuhakikisha kuwa serikali yake inaongeza juhudi ili idumishe mafanikio hayo.

Baadhi ya maeneo ya mafanikio ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa mtandao mkubwa wa barabara za lami na pia ujenzi wa madaraja makubwa kama la Mto Malagarasi. 

Mafanikio mengine ni kuwapo kwa shule nyingi zaidi za sekondari nchini, kushamiri kwa vyuo vikuu na kuongezeka kwa ufanisi katika sekta ya Bandari ni miongoni mwa maeneo ya mafanikio, sawa na ilivyo katika harakati za kuimarisha amani na utulivu katika visiwa vya Zanzibar kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

SOURCE: NIPASHE

No comments: