ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 24, 2015

Askari Handeni watishia kugoma kusimamia vituo vya kupigia kura

Askari akilinda moja ya vituo vya kupigia kura
By Rajabu Athumani, Mwananchi

Handeni. Askari mgambo 114 wilayani Handeni wametishia kugoma kwenda kusimamia vituo vya kupigia kura kutokana na kutolipwa fedha zao kama walivyokubaliana na mkurugenzi.

Wakiongea na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo mgambo hao wamesema kuwa katika makubaliano yao walisaini hela yote lakini kwenye malipo walipewa nusu ya hiyo hela ambapo ni kinyume na maelewano ya awali.

Seiph Mhando askari kata ya Chanika wilayani Handeni ambae ndio kiongozi wa mgambo hao amekiri kutokea kwa kutoelewana huko kuwa mgambo hao walikataa kupewa pesa nusu na ikiwa hivyo hawatakwenda kulinda vituo.

Amesema mgambo walitaka fedha kama walivyosaini na ikiwa haitakuwa hivyo maamuzi yao yatakuwa ni yale Yale.

Akifafanua suala hilo Mkurugenzi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Handeni mjini Keneth Haule amesema ni kweli kulitokea tatizo hilo ambapo mgambo hao 114 wametaka kulipwa fedha zote ila taratibu zinabana kufanya hivyo.

Ameeleza kuwa ni kweli kuna makosa yalifanyika kwa kuwaeleza kiasi chote watakacholipwa lakini wakawapa nusu lakini walikata na kutaka kulipwa fedha yote kama walivyokubaliana kwenye mkataba wa awali.

Haule amesema sababu ya kutotoa fedha zote ni ili kuweza kujikinga na dharura yoyote itakayoweza kutokea kwa mmoja wa askari hao ila kwasababu wametaka kulipwa fedha zote wameshawalipa.

Ameongeza kuwa kwa kuwa kila mgambo atakabidhiwa vifaa basi ndio itakuwa dhamana kwa kila askari.

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi kesho ameeleza kuwa yapo vizuri hakuna tatizo lolote lililoripotiwa kwenye eneo lake na mambo yote kesho yatakwenda vizuri.

No comments: