
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere
Huwezi kusikiliza lolote kuhusu kampeni za uchaguzi Tanzania bila kulisikia jina la Mwalimu Julius Nyerere likitajwa kwa kunukuliwa alichokisema. Kila upande, uwe ni upinzani au Chama Cha Mapinduzi (CCM) mgombea akitaka kutia uzito maneno yake, atamnukuu Mwalimu Nyerere.
CCM kinampinga mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa kwa kusema; “hata Mwalimu alimkataa Lowassa mwaka 1985”. Lowassa naye anajibu mapigo kwa kusema; “Hata Mwalimu alisema wananchi wakiyakosa mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM”.
Kwa maneno mengine, Mwalimu Nyerere haepukiki katika siasa za Tanzania hasa wakati wa uchaguzi. Kauli zake ni mtaji mzuri wa kisiasa kwa yeyote yule awe chama cha upinzani au chama tawala. Hapo ndipo unapokuja umuhimu wa kuangalia uhusiano wa Mwalimu Nyerere na uchaguzi Tanzania.
Mwalimu katajwa kwa mengi lakini kuna moja ambalo Mwalimu Nyerere halitajwi ni lile la kutaka kuwaamulia Watanzania nani awe rais wa Tanzania. Hili ndilo linaloipa tabu wanaCCM kuona haiwezekani chama kingine kushika madaraka badala yao.
Katika makala iitwayo: “Great leaders groom heirs and relinquish power,” mtunzi, Peter Mutua anasema kwamba viongozi wakubwa huandaa warithi wao kisha huachia madaraka.
Mwalimu na kuachiana madaraka
Mwaka 1985 wakati Mwalimu anang’atuka, kama alivyosema Peter Mutua kuwa watu mashuhuri huandaa warithi wao kabla ya kuachia madaraka, na yeye alijaribu kumrithisha uongozi wa Tanzania mtu wake ambaye alikuwa ni balozi Salim Ahmed Salim.
Kwa bahati mbaya ingawa Mwalimu alikuwa na nguvu kubwa katika CCM, mtu wake huyo hakukubaliwa hasa na Wazanzibari. Baada ya Mwalimu kuona hali hiyo, Balozi Getrude Mongella akatoa wazo kwa kumwambia: ‘‘Mwalimu kwa nini usimjaribu Makamu Ali Hassan Mwinyi?”.
Mwalimu hakuwa kama viongozi wa sasa wa CCM ambao hawasikilizi watu wanasema nini. Zaidi ya mara moja aliwaambia CCM katika kutafuta kiongozi chama lazima kisikilize watu wanasema nini. Mwalimu alisikiliza maoni hayo na kilichotokea hivi sasa ni historia.
Mzee Mwinyi akawa Rais wa Tanzania kumrithi Mwalimu ingawa hakuwa chaguo lake. Kwa kufanya hivyo, Mwalimu Nyerere akaweka utaratibu wa kiongozi aliye madarakani kutaka kurithisha mtu anayemtaka yeye badala ya kuwaachia wananchi kumchagua wamtakaye.
Mwalimu na uchaguzi 1995
Miaka 10 baada ya Mwalimu kung’atuka madarakani, muda wa urais wa Mzee Mwinyi ukawa umemalizika kikatiba.
Katika kutafuta nani atamrithi Mzee Mwinyi, wanaCCM kadhaa wakajitokeza wakiwamo John Samuel Malecela, Jakaya Mrisho Kikwete na hata Edward Lowassa anayegombea urais kupitia tiketi ya Chadema mwaka huu.
Mwalimu aliwapinga wote hao na kwa John Malecela alifikia kusema; “Kama jina la John lipo basi mimi narudisha kadi ya chama”. Si mahali pake kueleza sababu kwa nini hakumtaka Malecela lakini jambo la muhimu ni kwamba kwa mara nyingine tunamuona tena mwalimu akitaka kumrithisha mtu aliyeona yeye anafaa.
Walipobaki Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, Mwalimu alimwambia Kikwete kuwa wakati wake bado. Hapa Mwalimu alipuuza mawazo ya watu kwani aligundua kwa kusikiliza watu asingeweza kumpata yule anayeona anafaa kuiongoza Tanzania baada ya Mzee Mwinyi.
Mwalimu alimuona Benjamin Mkapa kuwa ndiye anayefaa kuwa rais baada ya Mwinyi. Kwa kuwa alitaka kumuweka ‘mtu wake’, ilibidi Mwalimu ainuke mwenyewe kumnadi Mkapa nchi nzima. Mkapa akashinda na CCM ikabaki madarakani.
Mwalimu alifariki mwaka 1999 akiwa amewaachia Watanzania utamaduni wa rais aliyeko madarakani kuona ni haki yake kumrithisha ‘mtu wake’ madaraka. Utamaduni ambao ukifuatwa unaonekana kuwa na madhara kwa CCM na hata Taifa .
Mwaka 2005, Benjamin Mkapa alijaribu kufanya kile alichokifanya Mwalimu, kumrithisha ‘mtu wake’ madaraka. Mkapa hakuwa na nguvu na ushawishi kama Mwalimu Nyerere hivyo ilibidi asalimu amri kwa kundi lililojulikana kama wanamtandao, kundi ambalo lilikuwa na Jakaya Kikwete na Edward Lowassa.
Tukumbuke kuwa mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alimwambia Kikwete muda wako bado. Kauli hiyo ilikuwa na maana Kikwete anafaa kuwa rais lakini zamu yake ilikuwa tu haijafika.
Kwa maneno mengine, mwaka 2005 hata akiwa kaburini Mwalimu Nyerere aliamua nani awe mgombea wa CCM kwani kwa kumkubali Kikwete wakati wa uhai wake, ilikuwa ni sawa na kumkubali akiwa kaburini.
Mwaka huu, athari ya Mwalimu Nyerere katika uchaguzi huu imebakia katika nukuu ya maneno yake. Mwalimu amesababisha Lowassa kukataliwa na CCM kwa madai kuwa “hata Mwalimu alimkataa”.
Kwa vyovyote vile, Watanzania wanapokumbuka miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Nyerere athari yake katika uchaguzi haiepukiki iwe ni kwa wema au ubaya, kwa CCM au vyama vya upinzani. Lililo baya ni ule utamaduni wa rais aliyeko madarakani kutaka kumrithisha madaraka anayemtaka.
Hili iwapo halitoachwa, litasababisha nchi kuja kuingia katika machafuko. Kama watu wananukuu Mwalimu Nyerere alisema “katika kutafuta wagombea chama lazima kisikilize watu”, tujiulize ni chama gani cha siasa Tanzania kinasikiliza watu katika kuwapata wagombea wake?
Fikiria kile kilichotokea CCM mwaka huu; je, mgombea aliyepo alitokana na sauti ya watu? Matokeo yake ni huu mpasuko tunaoushuhudia katika CCM kwa kuhamwa na makada wake waandamizi akiwamo mmoja wa waasisi wake, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru. Hatujui ni nani atafuatia lakini haya ni madhara ya jaribio la Mwalimu kutaka kumrithisha mtu wake uongozi.
Muda mfupi kabla ya uteuzi wa mgombea wa CCM, rais Mstaafu Benjamin Mkapa alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akisema kuwa chama hakiwezi kwenda kinyume na matarajio ya watu kuhusu uteuzi wa wagombea kwa ajili ya urais. Kauli hiyo ni kamba Mkapa anakumbuka wosia wa Mwalimu usemao: “Katika kuwapata wagombea, lazima chama kisikilize watu wanasema nini”.
Lowassa aliijua kauli hiyo ya mwalimu kwa hiyo akapiga kampeni na kujipanga ili chama kisikie watu wanasema nini. Kitu ambacho alikisahau ni ile kanuni kwamba kiongozi hupenda kuachia madaraka kwa mtu ambaye alimwandaa. Bahati mbaya mtu huyo hakuwa yeye Edward Lowassa.
dinyampuntaz@yahoo.com
2 comments:
Mtoa mada, hii makala yako ni pumba kabisa ni makala ambayo mtu anadiscuss na mkewe au hawara yake baada ya kukosa kitu cha kuzungumza. Lakini sio makala ya kuitoa hadharani kujaribu kuwaaminisha watu wazima wa akili na ufahamu timamu wa nini hasa upeo na uadilifu, uchungu na uzalendo ulitukuka wa mwalimu nyerere kwa Tanzania na watanzania wote kwa ujumla. Mtoa hii mada umetoa kisiasa zaidi kwa ajili ya kumtetea lowasa kana kwamba lowasa ni mtakatifu kuliko busara za mwalimu nyerere? Mwalimu nyerere wakati anapigania uhuru aliteseka sana lakini aliamini kuwa ili kujenga taifa lenye upendo na amani basi itakuwa vizuri kama uhuru wa nchi yake utapatikana kwa njia ya amani na kweli alufanikiwa kwa hilo. Kama lowasa angelikuwa ni kiongozi akiongoza kupigania uhuru wa nchi hii hadi kupatikana kama ilivyokuwa kwa mwalimu nyerere basi mawili yangetokea aiza lowasa angelikuwa dikteta au mfalme wa nchi hii na watu wa kabila lake lingekuwa ndilo kabila lililotukuka Tanzania zima. Au kama lowasa angekosa kujipa ufalme au udikteta kama angelikuwa na nafasi ya nyerere baada ya uhuru basi angejikatia mkoa mzima ukawa mali yake hilo halina shaka . Sasa huyo lowasa mwalimu alishauri kuwa hafai kuwa raisi na kweli lowasa hakuwahi raisi licha ya jitahada zake kutakakuwa. Lowasa ana mali na utajiri wa ajabu kuzidi utajiri wote wa maraisi wa staafuu wa Tanzania kuanzia mwalimu nyerere? Sasa je kama angelikuwa raisi angekuwa mtu wa aina gani,? Lowasa hakuwahi kuwa mfanya biashara au alierisi mali kutoka kwa wazee wake. Utajiri wake kaupata kutokana na kukwapua rasimali za watanzania kutokana na nyazifa zake mbali mbali serikalini alizokuwa akilitumikia taifa. Nyerere kamwe asingekuwa tayari kuweka misingi ya viongozi wabadhirifu wa aina za kina lowasa alafu watu waje kusema ni yeye alieijenga misingi ya viongozi wa hivyo wanalolitafuna taifa. Nyerere alimpendekeza mkapa kwa kuwa viongozi wanadiaspora kama kina mkapa watakuwa wanaupeo mkubwa kuhusu maendeleo ya nchi. Alumshauri kikwete apate uzoefu zaidi kabla ya kuomba nafasi hiyo licha ya kuwa alikuwa kijana smart, kwani nna uhakika kikwete alifaidika sana na ushauri huo wa baba wa taifa, kwani baada ya miaka kumi kama balozi wa nchi za nje wa watanzania kikwete alirudi kugombea uraisi akiwa ameshaiva hasa. Nani asiejua umahiri wa Salim Ahmed A slim na taaluma yake katika masuala ya uongozi hasa masuala ya kimataifa. Sasa kwanini nyerere asitamani salim kuwa kiongozi wa nchi anaipenda kwa dhati? Nyerere kamwe hakumpendekeza mtu kuwa kiongozi wa nchi kwa maslahi yake yeye binafsi, kamwe. Alimpendekeza mtu kuwa kiongozi wa nchi kwa uwezo wa mpendekezwa na zaidi maslahi ya nchi kwanza.
Mwandishi siyo mkweli anapoandika kuwa CCM inawaamulia Watanzania nani awe rais wao. CCM ina vikao vyake mbalimbali na wajumbe wa vikao hivyo wanatoka sehemu mbali mbali za nchi ikiwa ni pamoja na vijijini, mijini, wilayani, mikoani na hata kitaifa. Hawa wajumbe kabla ya kwenda kwenye mikutano huwazungukia wananchi wao ili kusikia sauti zao na hivyo wanapokwenda kukutana katika vikao vyao ikiwa ni pamoja na vikao kama hivi vya kuteua wagombea wa urais, udiwani na wabunge, wanakwenda huko kuwasilisha maoni ya wananchi. Hawaendi kule kwa nafsi zao ndio maana wananchi wanawachagua ili wawawakilishe katika maswala yote yanayowahusu. Bila kuwa na wawakilishi wa wananchi kama hawa hoja za wananchi wengi zingekuwa zinapotea bure kwani siyo kila mmoja wetu anauwezo wa kufikisha hoja yake kule inakotakiwa.
Mwandishi lazima aelewe kuwa pamoja na kusikiliza sauti za watu kiongozi anatakiwa pia kuwa mshauri wa hao watu anaowasikiliza. Ukweli uliopo ni kwamba siyo kila mwananchi anawajua viongozi wetu hususan walioko juu. Ndiyo maana viongozi katika ngazi tofauti ni kazi yao kuwashauri watu walioko chini yao kuhusu viongozi walioko juu yao. Ushauri kama huu ni muhimu sana hasa kama kuna jambo amblo linatakiwa kutolewa msimamo. Tujiweke katika hali ya uchaguzi, kwa mfano, kama kiongozi na anasikia watu wanataja jina la mtu wanayetaka kumchagua na anajua ana kasoro, kiongozi huyo hawezi kukaa kimya na kuachia jambo hili litokee. Anachotakiwa ni kuwajuvye watu wake na kama inabidi kuondoa jina la mtu huyo katika mchakato huo. Yote haya yafanyanyika kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Pamoja na haya yote mwandishi anasema kuwa “swala la kuwaamulia Watanzania nani awe rais wao ndilo linaloipa tabu wanaCCM kuona haiwezekani chama kingine kushika madaraka badala yao.” Sioni vipi mwandishi anafikiria CCM itawaamulia wananchi nani awaongoze badala yake kama wananchi wataamua kupigia kura chama kingine. Mwandishi lazima ajue kuwa CCM siyo chama kilichoko juu ya vyama vingine bali vyama vyote viko ngazi moja na chama kimoja hakiwezi kushurutisha chama kingine kufuata matakwa yake. Kama hoja ni chama gani kushinda uchaguzi itategemea jinsi kila chama na wagombea wake wanavyo nadi sera zao na anayvoweza kuwashawishi wapiga kura ili wawachague. Kwa mantiki CCM haiwezi kuwaamulia wananchi wachague chama gani.
Kuhusu uteuzi wa mgombea wa sasa wa CCM mwandishi amehoji ati ulitokana na sauti gani! Hivi mwandishi alitaka mamillioni ya wanachama wa CCM wote waende Dodoma kila mmoja akapige kura yake kwenye vikao vya chama vilivyoandaliwa maalum kwa shughuli hiyo? CCM ilipokea majina 38 ya wagombea urais. Kutokana na katiba ya CCM mchujo ulianza na wagombea ambao hawakuwa na sifa zilizotakiwa wakaondolewa. Wagombea walianza kuchujwa na kubaki wagombea 5. Wakapunguzwa tena wakabakia 3. Mchujo ukaendelea zaidi hadi mgombea 1 akabakia na ndiye ambaye alipewa jukumu la kupeeperusha jina la CCM katika uchaguzi wa mwaka huu na sasa anapambana vikali na wenzake wa upinzani. Kutokana na hali ya mapambano yanayoendelea sasa katika kampeni imejionyesha dhahiri kuwa mgombea huyu amekubalika na siyo wanaCCM tu bali hata na wengine wengi ambao siyo wanachama wa chama hiki. Pamoja na haya yote mchujo wa viongozi wa CCM umefanyika kuanzia ngazi ya chini kabisa ya katiba hadi kufikia ngazi juu kama ilivyoidhinishwa na katiba ya chama. Kama tunakubali kuwa wajumbe wa ngazi zote za kamati hizi za chama ni wateuliwa na wawakilishi wa wanachama na ambao ndiyo sauti ya wananchi, je mwandishi anataka kusikia sauti gani nyingine ndiyo aridhike kuwa uteuzi wa CCM ulikuwa halali na umefuate taratibu na kanuni zote za katiba ya chama? Au anataka kutuambia kuwa sauti ya wananchi ingesikika tu pale Lowassa angeteuliwa na kamati hizi? Je huko Lowassa alikokimbilia taratibu gani za katiba ya chama hicho imefuatwa? Zaidi ya mgombea wao huyu kuteuliwa na mtu mmoja au kikundi cha watu wenye mwelekeo mmoja kuna mwanachama gani mwingine aliruhusiwa kuomba kugombea zaidi ya kuona viongozi wengine kujitoa kwenye chama hicho pamoja na muungano wao?
Post a Comment