ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 14, 2015

BARAZA KUU LA USALAMA LAJADILI NAFASI YA MWANAMKE: PINDI CHANA AZUNGUMZA

Taswira ya Ukumbi wa Baraza Kuu la Usalama ulivyosheheni wajumbe na Washiriki wa Majadiliano kuhusu Azimio la Wanawake, Usalama na Amani, majadiliano ambayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na wawakilishi kutoka mataifa mbalimbali.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Pindi Chana akizungumza mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakati Baraza hilo lilipokutana kwa siku zima ya Jumanne kujadili Azimio 1325, Azimio linalozungumza fursa ya wanawake kama kiungo muhimu katika masuala ya amani na usalama wa Kimataifa.

Na Mwandishi Maalum, New York

Kwa siku nzima ya jumanne, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilikutana kwa majadiliano kuhusu nafasi ya ushiriki wa mwanamke katika masuala ya Amani na Usalama, kwa mujibu wa Azimio maarufu namba 1325 ambalo lilipitishwa na Baraza hilo miaka 15 iliyopita (2002).

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano katika majadiliano nayo na ambayo yalijikita Zaidi katika kufanya tathmini ya utekelezaji wa azimio hilo pamoja na changamoto zake na nini kinatakiwa kufanya kwa siku za baadaye, uliongozwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Pindi Chana.

Majadiliano hayo na ambayo yalitoka na Azimio jingine linalochagiza Zaidi pamoja na mambo mengine utekelezaji dhabiti wa ajenda hiyo ya Wanawake, Amani na Usalama litatekelezwa kwa miaka 15 ijayo, yaliwahusisha viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa, wakiongozwa na Katibu Mkuu, Ban Ki Moon ambaye amesema, bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanywa ili kuhakikisha kwamba mwanamke anapata fursa ya kuwa kiungo muhimu katika masuala ya ujenzi wa Amani, usalama na kupata fursa pana Zaidi katika majadiliano yanahusu eneo hilo.

Akasema kuwa yeye kama muumini mkubwa na anayetambua nafasi na mchango wa mwanamke katika nafasi za uongozi na maamuzi amesema katika uongozi wake ameteua wanawake na kuwapa nafasi za juu za uongozi zikiwamo katika Misheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.

“Miaka kumi na tano iliyopita, Baraza la Usalama lilipitisha Azimio 1325 ambalo lilisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia kama kiungo muhimu katika ujenzi na uimarishaji wa Amani na usalama wa kimataifa. Na tangu wakati huo, Baraza hili limendelea kupitisha maazimio kadhaa kila mmoja likisisitiza katika kuchukua hatua za kuwashirikisha wanawake katika eneo hilo” amesema Ban Ki Moon

Na kuongeza “ mimi binafsi nina nia ya kutekeleza maazimio haya na nimetekeleza kwa kuteua wanawake watano ambano ni Wawakilishi wangu maalum katika ujenzi na Amani na usalama, kuanzia Haiti hadi Ivory Coast na kutoka Sahara ya Magharibi , Sudan ya Kusini mpaka Cyprus ambako Kamanda Mkuu wa Misheni ya Kulinda Amani ni Meja Jenerali Kristin Lund ”.

Katibu Mkuu amewashukuru Nchi wanachama waliohudhuria na kushiriki majadiliano hayo ambayo yalikuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Hispania Bw. Mariano Rajoy. Hispania ndiye Rais wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Octoba.

Akizungumza wakati wa majadiliano hayo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Pindi Chana amesema kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa Azimio 1325 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita ni uhaba wa rasilimali za kutosha na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa ushiriki kamilifu wa wanawake .

Akasema kuwa mgao mdogo wa raslimali, ukosefu wa utashi wa kisiasa, kutotekelezwa kwa hadi na uwajibikaji katika mataifa mengi kumechangia kurudisha nyuma juhudi za kuwashirikisha wanawake katika eneo hilo muhimu.

Akaongeza kwamba utafiti umeonyesha kwamba pale ushiriki wa mwanamke katika jambo lolote lile liwe la ulinzi na ujenzi wa Amani, maendeleo na kuupiga vita umaskini matokeo huonekana kwa haraka.

“ Wanawake wakishirikishwa katika utatuzi wa migogoro Amani inapatikana na inakuwa endelevu, ni kwa ukweli huo kwamba tunahitaji kushirikiana Zaidi katika kuhakikisha ushiriki wa mwanamke katika nafasi mbalimbali”. Amesisitiza Mhe.Pindi Chana.

Akizungumzia ni kwa kiasi gani Tanzania imetekeleza Azimio 1325 amesema pamoja na changamoto za hapa pale serikali imejitahidi kuongeza fursa na nafasi za wanawake katika vvombo vya kutoa maamuzi kama vile Bunge, Sheria na hata nafasi za uongozi ndani ya serikali.








No comments: