Mgombea urais kupitia chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Chifu Yemba
Dar es Salaam. Kampeni si majukwaani pekee, ndivyo kinavyoamini chama cha Alliance For Democratic Change (ADC).
Ndiyo maana tangu kizindue kampeni zake za urais jijini Tanga Agosti 31 mwaka huu, mgombea wake wa urais, Chifu Lutayosa Yemba hajaonekana tena majukwaani.
Mgombea mwenza wa chama hicho, Said Miraji anasema kuwa Chifu Yemba hafanyi kampeni jukwaani badala yake anataka kumfikia mpigakura mmojammoja. Anasema staili hiyo ya kumfuata mpigakura, inaweza kushawishi watu wengi zaidi kuliko kampeni za majukwaani ambazo uzoefu wa mwaka 2010, unaonyesha kuwa haziwashawishi watu kukipigia kura chama.
“Sisi tunaenda nyumba kwa nyumba kuzungumza na wapigakura.Tunawafuata na kuwaeleza ilani yetu na tumefanya hivyo katika maeneo mengi tukiamini kwamba watu tuliowafikia watatupigia kura wote,” anasema Miraji ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho.
Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya mwenyekiti huyo kueleza kuwa chama hicho ni miongoni mwa vyama kadhaa vilivyoshindwa kufanya kampeni kwa sababu ya ukata.
Miraji aliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kubadili sharia ya kutoa ruzuku kwa vyama vilivyokuwa na wabunge pekee badala yake ruzuku hiyo itolewa kwa vyama vyote vinavyosimamisha wagombea urais ili kuweka mazingira sawa ya ushindani.
Miraji anaeleza kuwa utaratibu wa kuvipa ruzuku vyama vikubwa si tu hautoi mazingira sawa ya ushindani baina ya vyama, bali pia ni hatari kwa usalama wa taifa kwa kuwa kunaweza kutokea kundi fulani la watu likaamua kuvifadhili vyama hivyo kwa nia ovu.
“Hii ni sawa na kuwa na mabondia wawili halafu mmoja unamfunga pingu na bado unamleta uwanjani wapigane,” anasema.
“Hakuna usawa katika mfumo wa uchaguzi nchini. Naiomba Serikali iangalie upya utaratibu wa ruzuku kwa masilahi mapana ya taifa.”
Kuibuka kwa Chifu Yemba
Ingawa alikuwa na shauku kubwa ya kumaliza kero nne za Watanzania iwapo ataingia Ikulu, Chifu Yemba, ambaye ni mtalaamu wa madini, ameonekana kukwama kuwafikia wapigakura ili awaeleze sera hizo.
YEMBA NI NANI?
Yemba ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma, alizaliwa Mbinga mkoani Ruvuma mwaka 1966. Alisoma Shule ya Msingi ya Kaluta kati ya mwaka 1975 na 1981. Alisoma Shule za Sekondari za Uyui na Ujiji kati ya mwaka 1982 na 1985. Mwaka 1986 hadi 1987 alisoma kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari ya Iyunga mkoani Mbeya.
Kati ya mwaka 1988 hadi 1990 alisoma katika Chuo Kikuu cha Southern Carolina na kutunukiwa shahada ya elimu ya viumbe. Mwaka 1998 alisoma katika Chuo Kikuu cha Frankfurt Ujerumani na kupata shahada ya uzamili ya Hydrogas.Kisiasa aliwahi kuwa mwanachama wa CUF kabla hajahamia katika ADC.
Aliwahi kufanya kazi katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji kati ya mwaka 1987 hadi 1997. Hivi sasa ni mjasiriamali anayejishughulisha na uchimbaji wa madini.
Chifu Yemba alikuwa mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Shinyanga aliyekuwa amepania kupambana na Profesa Ibrahim Lipumba kwenye mbio za uenyekiti wa chama hicho, ingawa wakati huo hakuonekana kuwa alikuwa akianza safari ya kuelekea Ikulu.
Hata hivyo, harakati zake za kushika wadhifa wa juu wa CUF ziligonga mwamba baada ya Baraza Kuu kumtimua kwa tuhuma za ubadhirifu na kutumia vibaya jina la Profesa Lipumba.
Akiwa mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Chifu Yemba aliona kuna uwezekano wa kupindua uamuzi huo na hivyo kuandika barua ya rufaa kwa katibu mkuu, Maalim Seif Sharrif Hamad, ambaye hakutengua uamuzi huo.
Akizungumza na waandishi wakati huo, Chifu Yemba alisema CUF ilikuwa imepanga kumtimua muda mrefu kutokana na misimamo yake kwenye vikao vya chama.
“Zilikuwapo kamati tatu zilizonichunguza, nasikitika walitoa
taarifa za uongo ili kulilazimisha baraza lichukue uamuzi,” alisema.
“Waliamua kuwarekodi watu kwa maelekezo yao binafsi na kwa makusudi wakatumia maneno hayo kama uthibitisho. Utaratibu walioutumia kunifukuza, sijaridhika nao na nimekataa rufaa kupinga uamuzi wa baraza,” alisema
Chifu Yemba. Kwa mujibu wa Chief Yemba, baada ya uchunguzi huo hakupewa nafasi ya kujitetea wala hakuwahi kusomewa mashtaka badala yake baraza lilimpa hati ya mashtaka nusu saa kabla ya kikao cha kutoa uamuzi.
Vipaumbele vyake
Safari hii ameibuka upya, akiwa chama hicho cha ADC ambacho kimempa fursa ya kuwania urais. Yemba anasema iwapo atachaguliwa kuongoza taifa la Tanzania, mambo manne atayapa kipaumbele ni pamoja na kuboresha huduma za afya ili kila Mtanzania anufaike, huduma za maji, kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, kutumia rasilimali zilizopo na kuboresha maisha ya watu.
Anasema asilimia 78 ya Watanzania hawana afya bora na kwamba kutokana na idadi hiyo kubwa, itakuwa vigumu kwa watu wa aina hiyo kujiletea maendeleo.
Anasema kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi, atazitumia ili kuboresha huduma za afya ili kila mtu bila kujali ana kipato cha aina gani, aweze kupata huduma hizo.
Kuhusu maji, Yemba anasema hicho ni kipaumbele kingine muhimu na anaungana na mgombea mwenzake, Rakesh kusema maji yamekuwa yakiwatesa Watanzania kwa muda mrefu.
Anasema Serikali haijawa na nia ya dhati katika kukabaliana na tatizo la maji ndiyo maana hata bajeti katika miradi ya maji zimekuwa hazitekelezeki.
“Tanzania ina kiu ya maji na utafiti wangu umebaini kwamba asilimia 20 tu ya Watanzania ndiyo wanaopata majisafi na salama baada ya zaidi ya miaka 50 ya uhuru, huu ni utani,” anasema.
Anasema asilimia 74 ya ardhi ya Tanzania ina maji ya kutosha na kwamba kutowapatia wananchi majisafi na salama ni kuwapuuza.
Mgombea huyo anasema akichaguliwa atahakikisha anadhibiti
mianya ya ukwepaji kodi hasa kwa kuangalia upya utoaji wa misamaha. “Hatuwezi kupata maendeleo kama tutaendelea kutoa misamaha ya kodi. Nitalishughulikia eneo hili kikamilifu ili kuinua maisha ya Watanzania,” anasema.
Pamoja na kwamba alipania kupambana na Lipumba kuwania uenyekiti wa CUF, Chifu Yemba anaonekana hana kinyongo na uamuzi wa Baraza Kuu kumtimua uanachama.
Wakati Profesa Lipumba alipotangaza kujivua uenyekiti wa CUF kwa maelezo kuwa dhamira inamshitaki kutokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpa fursa kada wa zamani wa CCM, Edward Lowassa kuwania urais, Chifu Yemba alimuomba msomi huyo wa uchumi ajiunge na ADC.
No comments:
Post a Comment