Alisema kilichofanywa na Zec kimeteteresha imani ya wananchi kwa tume hiyo kwani Mwenyekiti wake alipaswa kuwachukulia hatua mara moja makamishna waliokiuka sheria na kanuni siku ya kupiga kura.
“Zec ilitakiwa iwe na uwezo wa kukamata watu waliovunja sheria na kuwachukulia hatua, siyo kusubiri siku zimepita ndipo wanayasema haya na kufuta matokeo…naona kama hawakuzingatia sheria kwa kutotoa taarifa mapema,” alisema.
Aliongeza: “Zec wamepoteza imani ya wananchi na fedha za walipakodi ambazo zingelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.”
Hata hivyo, alisema kwa sasa itamlazimu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Wawakilishi ili kuidhinisha muda wa kuendelea kukaa madarakani hadi hapo uchaguzi mwingine utakapofanyika.
STOLA: DEMOKRASIA IMEBANWA
Akizungumzia uamuzi huo wa Zec, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola, alisema pamoja na kwamba hautaathiri uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kitendo hicho kimebana demokrasia.
Alisema inasikitisha kuona kuwa kasoro ndogo zinaahirisha uchaguzi na kufuta matokeo, akifafanua kuwa hilo linachangiwa na kuwapo kwa masalia ya sheria za chama kimoja ambazo zinapaswa kufutwa kwa kuwa haziwezi kufanya kazi kwa haki katika uchaguzi wa kidemokrasia.
Hata hivyo, alisema uchaguzi wa Rais wa Zanzibar pamoja na wawakilishi unasimamiwa na Zec na kwamba tume hiyo ni wakala wa Nec ambaye hana mamlaka ya kutengua matokeo ya Jamhuri ya Muungano.
“Uchaguzi wa Zanzibar siyo suala la Muungano kwa sababu urais na uwakilishi upo chini ya Zec…Nec itatazama hizo kasoro na itaamua kwa sababu Zec ni wakala tu wa Nec,” alisema.
SUNGUSIA: NI UTATA MKUBWA
Naye mwanasheria mwingine ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia, alisema kufutwa kwa uchaguzi huo kunaweza kuwa na athari kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihoji wapigakura wanaodaiwa kushiriki uchaguzi wakiwa hawana vitambulisho vyao.
Alisema kama Nec na Zec hazijafuta matokeo ya uchaguzi wa wabunge visiwani humo, ni vigumu kujiridhisha kama wapigakura wanaolalamikiwa na Zec hawakupigakura za urais na ubunge wa Jamhuri ya Muungano kwa kuwa kura zilipigwa siku moja.
“Tunaweza kusema kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar hakuna athari zozote kwa urais na ubunge wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu unasimamiwa na mamlaka mbili tofauti…lakini mimi kama mwanasheria naona bado kuna utata mkubwa ambao ningetamani mamlaka zetu (Zec na Nec); zingetoa ufafanuzi zaidi,” alisema.
Sungusia alisema moja ya sababu za kufuta uchaguzi huo ambayo ni kuwapo kwa wapigakura wasio halali, inaweza kuathiri uchaguzi wa wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kuwa kura zilipigwa siku moja na hakuna anayeweza kuthibitisha kuwa wapigakura hao (wasio halali), hawakuchagua viongozi hao.
Aliongeza: “Kama Zec au Nec ikifuta uchaguzi wa wabunge visiwani Zanzibar itawezekanaje kuzindua Bunge la Jamhuri bila wabunge kutoka Zanzibar au uteuzi wa Baraza la Mawaziri utafanyikaje wakati baadhi ya wabunge wa Zanzibar huteuliwa kwenye Bazara la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano.”
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 74 (13), ya Katiba ya Zanzibar na Ibara ya 74 (13), ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zec na Nec zinapaswa kushauriana kwenye masuala mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi hivyo akashauri kuwa jambo hilo ni muhimu likazingatiwa katika hali ya sasa.
Alisema hilo linapaswa kufanyika kwa kuzingatia kuwa Zec ndiyo iliyosajili wapigakura kwa kukasimiwa madaraka na Nec kwa mujibu wa kifungu cha 12 (A) cha sura namba 343 ya uchaguzi baada ya kukasimiwa madaraka na Nec.
Hata hivyo, alisema uchaguzi wa rais na wawakilishi Zanzibar siyo suala la Muungano hivyo Zec ina mamlaka ya kuamua chochote pindi inapobaini kasoro kwenye mwenendo wa uchaguzi.
MAREKANI WATAKA UWAZI URAIS ZANZIBAR
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani jana jijini Dar es Salaam, imewataka maofisa wote wa serikali kuheshimu wajibu wa waangalizi rasmi wa uchaguzi kwa kuwaruhusu bila kipingamizi chochote kuangalia vipengele vyote vya mchakato wa uchaguzi.
Aidha, taarifa hiyo ya Marekani ilisema inafuatilia kwa karibu mchakato wa uchaguzi nchini kote Tanzania.
“Tunaendelea kufuatilia zoezi la majumuisho ya kura, ikiwa ni pamoja na zoezi linaloendelea la majumuisho ya kura za urais wa Zanzibar linalofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), tunatoa wito kwa mchakato huu kukamilishwa kwa wakati na kwa uwazi,’ ilisema taarifa hiyo
Wakati taarifa hiyo ikitolewa na Marekani na kuitaka Zec kukamilisha mchakato huo kwa wakati na kwa uwazi, tayari jana mchana tume hiyo ilitangaza kufuta uchaguzi na matokeo yote ya Zanzibar.
JAJI MIHAYO
Jaji mstafu Thomas Mihayo alisema hatua ya kufutwa matokeo ya urais Zanzibar, hayawezi kuathiri mchakato wa kumpata mgombea urais Bara kwa ni serikali mbili tofauti.
Alisema Zec, imetengua kura za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na siyo za wagombea ubunge na urais wa Serikali ya Muungano.
Alisema kwa mujibu wa sheria, rais anayemaliza muda wake wa uongozi Dk. Shein, ataendelea kuongoza Zanzibar hadi pale uchaguzi utakapofanyika tena.
WAKILI KAMALA
Naye Wakili wa kujitegemea Pascal Kamala , alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ibara ya 28 kifungu cha 1(a), Rais ataendelea kuwa madarakani hadi pale rais mwingine atakapopatikana na kuapishwa.
Alisema kutokana na maelezo ya kifungu hicho, Dk. Shein ataendelea kuwa madarakani.
Alisema kifungu cha 28 (ii) cha Katiba hiyo kinaeleza kuwa rais atakuwa madarakani kwa miaka mitano toka siku alipokula kiapo.
Hata hivyo, alisema vifungu hivyo vinakinzana kisheria kwa kuwa kimoja kinampa madara rais aliyopo madarakani kuongoza hadi pale rais mwingine atakapopatikana, lakini kifungu kingine kinamwelezea kuwa ataongoza kwa miaka mitano tu.
Kuhusu kufutwa kwa matokeo ya urais Zanzibar alisema hakuwezi kuathiri matokeo ya uchaguzi wa matokeo ya Serikali ya Muungano kwa kuwa ni serikali mbili zinazoendeshwa na Tume mbili tofauti za uchaguzi.
WAKILI NDUSIEPO
Lakini Wakili wa Kujitegemea, Apson Ndusiepo, alisema tukio la Zec kufuta matokeo ya uchaguzi linaathiri moja kwa moja kwa Rais wa Muungano kwa kuwa Rais wa Muungano hawezi kupatikan kabla ya kura za wananchi wa Zanzibar.
Alisema sababu kubwa ni kutokana na uchaguzi huo kutokuwa wa uaminifu, haki na huru.
Alisema hadi Zec wanafikia hatua ya kufuta matokeo, inamaanisha uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.
Alisema Katiba ya Zanzibar haijaeleza kama endapo uchaguzi ukisitishwa, serikali itaongozwa na nani, bali Katiba imeeleza tu endapo rais akifariki dunia, akiugua ama akipata ugonjwa, nchi itaongozwa na Makamu wa Rais.
MHADHIRI RUCO
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa (RUCo), Rwezaura Kaijage, alisema hatua ya Zec kutangaza kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kutokana na madai ya kugubikwa na kasoro mbalimbali, kunaleta athari kubwa za kisheria katika matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema: “Baada ya Zec kutangaza kufuta uchaguzi huo na matokeo yake yote, athari inayojitokeza ni kwamba wakazi wa Zanzibar watakosa Rais wao katika muda mwafaka uliowekwa kikatiba, lakini pia kujiongezea muda wa kukaa madarakani kwa Rais wa Zanzibar ni kuvunja katiba.
Alisema na kuongeza, Katiba inasema uchaguzi mkuu wa Zanzibar utafanyika kila baada ya miaka mitano na ukomo wa Rais kimadaraka ni vipindi viwili, hivyo Dk. Shein atakuwa amejiongezea muda kinyume cha Katiba katika kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mwingine.”
Alisisitiza kitakachoathiri kisheria uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ni kwamba Rais mpya aliyechaguliwa hawezi kutangazwa kwa sasa mpaka upande wa pili ambao ni Zanzibar ufanye uchaguzi mkuu mpya, kitu ambacho kinaweza kikauvuruga mchakato mzima licha ya kuwapo kwa mamlaka mbili ambazo ni Nec na Zec.
Kwa mujibu wa Kaijage, hata kama sheria inairuhusu Zec kufuta uchaguzi huo kutokana na kuwapo kwa kasoro, ilipaswa ieleze sababu za msingi ambazo si za kuiridhisha tume peke yake, lakini pia ziwe wazi mbele ya Watanzania na walimwengu wote.
*Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Rahma Suleiman, Godfrey Mushi, Gwamaka Alipipi, Restuta James na Mary Geofrey
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment