ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 18, 2015

IDADI YA RAIA WA BURUNDI WANAOINGIA NCHINI KUTAFUTA HIFADHI YA UKIMBIZI YAZIDI KUONGEZEKA

Baadhi ya Wakimbizi kutoka Burundi wakipokelewa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nduta, wilayani Kobondo, mkoani Kigoma. Idadi ya wakimbizi kutoka nchini humo inazidi kuongezeka siku hadi siku. Picha na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Watoto wa Wakimbizi kutoka Burundi wakiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo, mkoani Kigoma ambapo wanahifadhiwa

Idadi ya raia wa Burundi wanaoingia nchini kutafuta hifadhi ya ukimbizi inazidi kuongezeka siku hadi siku ambapo hadi kufikia tarehe `17 Oktoba, 2015 idadi hiyo ilikuwa imefikia 107,112.

Raia hawa wa Burundi wanaendelea kuingia nchini kupitia vijiji vya mpakani na wengi wao ni wanawake na watoto kutoka Mkoa wa Makamba nchini Burundi.

Vijiji wanapoingilia raia hawa kutoka Burundi ni pamoja na Bukililo na Katanga wilayani Kankonko, na Kitanga, Kigadye, Manyovu, Kilelema, Biharu, Migongo na Herushingo wilayani Kasulu. Kijiji kingine ni Mabamba kilichopo wilayani Kibondo, ambapo wengine hupitia wilayani Ngara mkoani Kagera.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine, imekuwa ikiwahifadhi wakimbizi hawa katika makambi ya wakimbizi ambapo hupatiwa huduma zote muhimu. Huduma hizo ni pamoja za malazi, chakula, afya, elimu na ulinzi.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeanza zoezi la kuwahamisha wakimbizi wa Burundi waliokuwa wakihifadhiwa kwa muda katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu na kuwapeleka katika kambi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo.

Zoezi hili ambalo limeanza tarehe 04 Oktoba, 2015 linalenga kupunguza msongamano uliokuwapo katika kambi ya Nyarugusu ambayo hadi wakati huo ilikuwa na jumla ya wakimbizi 102,773 kutoka nchini Burundi.

Tangu zoezi hili lianze, kiasi cha wakimbizi 3,808 kutoka nchini Burundi wameshahamishiwa katika kambi ya Nduta kutoka kambi ya Nyarugusu ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Kambi ya Nyarugusu ina kiasi cha wakimbizi 60,000 kutoka DRC.

Zoezi la kuwahamisha wakimbizi hawa kutoka nchini Burundi litaendelea hadi wakimbizi wote kutoka nchi hiyo walioko katika kambi ya Nyarugusu watakapoisha.

Pamoja na kambi ya Nduta, maeneo mengine yanayoendelea kuandaliwa ili kuwahifadhi wakimbizi hawa kutoka Burundi ni Mtendeli na Karago yaliyoko wilayani Kakonko mkoani Kigoma.

Aidha, wakimbizi wote wanaoendelea kuingia nchini kutoka Burundi kwa sasa hupelekwa moja kwa moja katika kambi ya Nduta badala ya kambi ya Nyarugusu.


Imetolewa na Isaac J. Nantanga

MSEMAJI – WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

0754 484286

18 Oktoba, 2015

No comments: