ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 22, 2015

Kesi mita 200 moto.

Mvutano mkali wa hoja za kisheria ulitikisa kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana wakati Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson alipoiomba mahakama itupilie mbali maombi ya walalamikaji katika kesi inayohusiana na umbali wa mita 200 za kusimama kutoka kwenye vituo vya kupigia kura.

Dk. Ackson alidai mahakamani hapo kuwa maombi ya kesi ya kikatiba ya kutaka tafsiri ya kifungu cha 104 cha Sheria ya Uchaguzi yamewasilishwa na walalamikaji kwa kutumia sheria isiyostahili na kwamba, kwa sababu hiyo hayana mashiko na hivyo (maombi hayo) yatupiliwe mbali.

Kadhalika, Dk. Ackson alidai kwamba mlalamikaji katika kesi hiyo, mgombea ubunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Amy Kibatala, hajanyimwa haki ya kikatiba ya kupiga kura siku ya uchaguzi utakaofanyika Jumapili ijayo.

Dk. Ackson alitoa madai hayo jana wakati akijibu hoja iliyowasilishwa kwa hati ya kiapo cha dharura ya mgombea huyo (Kibatala), dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo, Lugano Mwandambo na Aloysius Mjujulizi wanaosikiliza kesi hiyo.

Alidai kuwa madai ya mlalamikaji hayajaonyesha ni namna gani haki yake itakuwa imevunjwa hadi kufikia kuwasilisha maombi ya kutaka tafsiri ya sheria.

“Maoni yetu walalamikiwa kwamba sheria imesema wazi masuala ya tafsiri sheria itumike ipi… sheria nzima iliyoleta haya maombi mbele yenu siyo yenyewe hivyo kwa kuwa kifungu cha 104 kidogo cha (1) kinatoa tafsiri ya mambo matatu,” alidai wakati akijibu hoja za mlalamikaji.

Akifafanua zaidi, alisema sheria hiyo inakataa kufanya mkutano siku ya uchaguzi, hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura huku akionyesha picha au kuvaa nguo ya chama chochote.

Alisema sheria hiyo pia inakataza umbali wa mita 200 mtu yeyote kuonyesha picha na pia mtu yeyote asiyehusika kuwapo katika eneo hilo la kituo cha kupigia kura.

Dk. Akson alidai kuwa sheria namba 72, kifungu kidogo cha (1) kinasema mtu asiyepiga kura hatakiwi kuwapo eneo la tukio hilo kwa kuwa mgombea atawakilishwa na wakala wake.

“Watukufu majaji, NEC wana mamlaka ya kutoa maelekezo kwa makatazo lakini pia Rais Jakaya Kikwete alisisitiza kuhusu makatazo yaliyotolewa na tume hiyo kuhusu kufuatwa taratibu za sheria za uchaguzi” alidai na kuongeza kuwa:

“Sheria namba 104 inakataza mikutano bila kujali umbali na kwamba tafsiri ya sheria namba 72 inaeleza watu gani wanatakiwa kuwapo sehemu ya kuhesabia kura na kwamba, ambaye hakutajwa hatakiwi kuwapo eneo hilo,” alidai Dk. Akson wakati akiwasilisha hoja za walalamikiwa kwa muda wa saa 2: 37.

Alidai kuwa kutokana na hoja hizo, na kwamba kwa kuzingatia ukweli kuwa vituo viko kwenye makazi ya watu, hakuna mwenye uhakika wa kuwapo kwa utulivu katika mazingira hayo.

“Tunaomba maombi haya (ya walalamikaji) yatupiliwe mbali kwakuwa yameletwa hapa mahakamani kupitia sheria isiyostahili,” alidai.

Awali, akiwasilisha hoja za mlalamikaji, wakili Peter Kibatala alidai kuwa mlalamikaji anaiomba mahakama itoe tamko kuhusu maana halisi na kusudio la sheria namba 104 kifungu kidogo cha (1), sura ya 343.

Pia, mlalamikaji anaiomba mahakama iangalie maana ya kifungu hicho cha watu kuweza kukaa mita 200 kutoka umbali wa kituo cha kupigia kura.

Wakili Kibatala alidai mbele ya jopo hilo kwamba wapiga kura na watu wenye shauku wana haki ya kukaa kwa utulivu wakati tukio la upigaji kura likiendelea.

“Watukufu majaji, mlalamikaji kupitia kiapo chake anadai kuwa makatazo hayo yaliyotolewa na Nec na Rais Kikwete ambayo ameambatanisha nakala ya baadhi ya magazeti (siyo Nipashe), yataathiri ufuatiliaji wa tukio la kuhesabu kura na majumuisho siku ya kupiga kura Jumapili ijayo,” alidai.

Alidai kuwa tafsiri ya sheria namba 104 inaweza kuangaliwa kwa mitazamo mikuu miwili, kwa mpiga kura au watu wenye shauku.

Jaji Mujulizi alimhoji Wakili Kibatala kuhusu matamshi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, dhidi ya kuzuia wananchi kusubiri kulinda kura na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yao:

Jaji Mujulizi: Mbowe alisema wakimaliza kupiga kura wakae mita 200, ni kweli?

Wakili Kibatala: Ndiyo mheshimiwa.

Jaji Mujulizi: Wakae ili wafanye nini?

Wakili Kibatala: Walinde Kura.

Jaji Mujulizi: Aliwaambia akina nani?

Wakili Kibatala: Wapiga kura na wafuasi wa chama chake.

Jaji Mujulizi: Kinacholindwa watu, kura au tukio la uchaguzi kwa usalama na amani?
Wakili Kibatala: Mchakato mzima wa uchaguzi.

Aidha, wakili alidai kuwa haki ya kikatiba haiwezi kuchukuliwa kwa msingi wa madhanio kwani ni kinyume cha sheria.
Pamoja na mambo mengine, mlalamikaji ameomba kulipwa gharama za kesi na stahiki nyingine ambazo mahakama itaona zinafaa.

Mapema Oktoba 16, mlalamikaji alifungua kesi ya kikatiba iliyopewa usajili namba 37, ya mwaka huu, akiioomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 104 kidogo cha (1) cha Sheria ya Uchaguzi kama kinazuia ama la, wananchi kukaa kwa utulivu mita 200 baada ya kupiga kura katika vituo vyao.

Kesi hiyo inaendelea leo kwa ajili ya maelekezo muhimu yatakayotolewa na jopo la majaji.
CHANZO: NIPASHE

No comments: