Advertisements

Sunday, October 11, 2015

Mabadiliko yaanza

Mabadiliko yaanza
MGOMBEA wa Urais kupitia CCM, Dk John Magufuli, ameunda jopo la wanataaluma huru na magwiji wazalendo wa uchumi, biashara, utawala na sheria.

Hatua hiyo ni maandalizi ya kufanya mabadiliko makubwa serikalini kuanzia siku ya kwanza, atakayokuwa madarakani.

Aidha, katika ngwe ya mwisho ya kampeni, chama hicho kimesema kimeanza kampeni nzito, zinazoshirikisha viongozi wa juu, akiwemo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Katibu Mkuu wa Chama, Abdulrahman Kinana.

Hayo yalibainishwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba.

Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.

Jopo la mabadiliko

Akizungumzia maandalizi hayo kwa ajili ya mabadiliko serikalini, yaliyotajwa kuwa ni ya haraka na ya kweli, January alisema wanataaluma walioteuliwa, wanatoka katika taasisi za elimu ya juu, asasi zisizo za kiraia na sekta binafsi.

Dk Magufuli amelipatia jopo hilo majukumu 10, ambayo ni kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itabana matumizi, ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari.

Majukumu mengine ni kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itaongeza mapato mara moja, bila hatua za kibajeti na kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji, utumishi na ufanisi katika Serikali.

“Pia jopo hilo limepewa jukumu la kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya Serikali inayotekelezwa sasa,” alisema January.

Alisema kwa mujibu wa maagizo ya mgombea huyo, jopo hilo pia litapitia na kuorodhesha sheria zote za nchi, zinazopaswa kubadilishwa haraka kuharakisha mabadiliko ya kweli, aliyoahidi kwa Watanzania.

Alisema jukumu lingine ni kupitia na kuorodhesha masuala na kero zote, zinazosubiri uamuzi wa Serikali ili atoe uamuzi kuanzia siku ya kwanza atakayoapishwa.

Kazi nyingine ya jopo hilo ni kupendekeza miundo na idadi ya wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wakuu, atakaowateua baada ya kuapishwa.

January alisema jukumu lingine la jopo hilo ni kupendekeza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wa umma, hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi ili aanze nao kazi wakiwa na ari ya kusukuma mabadiliko ya kweli.

Jukumu lingine la jopo hilo ni kutengeneza rasimu ya mpango kazi kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizotoa kwenye kampeni, hasa upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika na kupendekeza muundo wa kitaasisi na utaratibu wa kutekeleza ahadi ya kutoa Sh milioni 50 kila kijiji.

Viongozi wa juu majukwaani

Akizungumzia maandalizi ya mwisho ya chama hicho ya kampeni, alisema chama hicho kimeanza kutumia viongozi wake wa juu, kuongeza ushawishi kwa wananchi wa kumpigia kura Dk Magufuli.

“Tayari Katibu Mkuu Kinana ameanza ziara ya kampeni katika majimbo 64, vilevile viongozi wengine akiwemo Mwenyekiti wa chama Rais Kikwete na Rais mstaafu Mkapa nao wataanza safari za kuzunguka nchi nzima kumwongezea kura Dk Magufuli na wagombea wa chama hicho wa ubunge na udiwani,” alisisitiza.

Alisema katika ngwe hiyo ya mwisho, chama hicho kitatumia helikopta nne, isipokuwa kwa mgombea urais, Magufuli na Mgombea Mwenza wa Urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan ambao wataendelea kutumia gari hadi mwisho wa kampeni, isipokuwa pale itakapolazimika.

Wajihakikishia ushindi Kuhusu tathmini ya mwenendo wa kampeni wa chama hicho, January alisema hadi juzi Dk Magufuli alishafanya mikutano mikubwa rasmi 240 na mikutano 865 ya kusimamishwa na wananchi njiani, hasa wa vijijini.

“Dk Magufuli amekuwa akitumia usafiri wa barabara na hadi sasa ametembea kilometa 31,467 kwa barabara kuu, barabara za mikoa, za wilaya, za mijini na za vijijini,” alisema.

Alisema kutokana na mwenendo wa kampeni hizo, tangu zianze hadi sasa zinapoelekea ukingoni, ni dhahiri kuwa chama hicho kitashinda katika uchaguzi mkuu, utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

“CCM haijapanga wala haifikirii kushindwa wala uwezekano wa kushindwa haupo,” alisema.

HABARI LEO

5 comments:

Anonymous said...

Tuko pamoja..kura lazima zitoshe asubuhi na mapema.

Anonymous said...

Kazi kweli kweli yaani serikali inaundwa kabla ya uchaguzi?ndipo utapojua hawa CCM wanafikiri tanzania ni ya kwako.

Anonymous said...

Wao ni wagonjwa wa akili. Wasubiri kazi ya Watanzania Oct 25.

Anonymous said...

Huku ni kuwalaghai wapiga kura ni bora usizipate kwani mnaonekana kulazimisha mambo. January haya ni majanga ndani ya chama chetu na sio mbinu ya kampeni..

Anonymous said...

CCM ni Tanzania na Tanzania ni CCM.