ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 16, 2015

MAGUFULI KAMA AKICHAGULIWA KUPAMBANA NA MAFISADI NDANI YA CCM


Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema mafisadi wamo hadi ndani ya chama chake na ndiyo maana baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wengi wao wameanza kuweweseka kutokana na hofu kubwa waliyo nayo dhidi yake.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni ya chama chake mjini Kisarawe, Pwani na baadaye Ukonga, jijini Dar es Salaam jana, Magufuli alikiri kuwa chama chake kiliwalea walarushwa na mafisadi kwa muda mrefu na ndiyo maana baadhi ya watu walianza kukichukia.

Hata hivyo, alisema tatizo hilo halitakuwapo tena kwani atakapoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, atahakikisha kuwa mafisadi wote wanashughulikiwa bila woga.

“Ndugu zangu, nasema kweli mafisadi hawako upinzani tu... ni ngumu sana mtu aliye ndani ya CCM kuyasema haya, lakini lazima niseme ukweli maana msemaukweli ni mpenzi wa Mungu. Haya mafisadi ndiyo yametufikisha hapa na (sasa), lazima tuyashughulikie,” alisema Magufuli na kushangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wake wa Ukonga.

Magufuli aliwataja kwa sifa za jumla mafisadi waliopo kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali, ambao hujihusisha na vitendo vya rushwa na dhuluma dhidi ya wananchi kiasi cha kuifanya serikali ichukiwe na baadhi ya wananchi wake.

Akitolea mfano, Magufuli alisema ni aibu kuona serikali ikikimbizana na mamalishe na wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) ili kupata kodi wakati kuna baadhi ya nchi ambazo zinaendeshwa kwa mapato ya bandari tu.

Magufuli aliongeza kuwa anatambua wananchi wamekuwa wakinyanyaswa katika maeneo mbalimbali ikiwamo kutozwa kodi zisizosaidia kuinua pato la taifa bali kuwafaidisha baadhi ya viongozi na kwamba, kwa sababu hiyo, haoni sababu ya kuendelea kwa hali hiyo hasa kwa kujua kuwa kuna nchi zinajiendesha kwa mapato ya bandari.

Alisema yote hayo ni baadhi ya mambo anayoamini kuwa ni sababu ya yeye kuchaguliwa kuwa rais ili kudhibiti uonevu kwa wanyonge na pia kupambana na mafisadi serikalini, ambao wamezoea kuishi kwa rushwa na ulaghai.

Kwa mfano, alisema anajua namna ambavyo baadhi ya watumishi bandarini huruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na kuikosesha serikali mapato yake ili kuwahudumia wananchi.

“Wapo watu wanaikosesha serikali mapato. Hawa nataka nikapambane nao... na nitapambana nao kweli kweli. Na hawatanikwepa…najua wananiogopa na wameanza kumwaga hela ili nishindwe. Nyinyi hela zao kuleni maana ni kodi zenu, lakini kura ni kwa Magufuli,” alisema.


BARABARA ZA JUU TAZARA
Katika hatua nyingine, mgombea huyo alisema ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya Tazara, Dar es Salaam utaanza muda wowote kwani mkandarasi ameshapatikana.

Dk. Magufuli alisema kuwa serikali ya Tanzania imeshatiliana saini na serikali ya Japan kwa ajili ya ujenzi huo kwani hata michoro imeshakamilika.

Alisema katika makutano ya Ubungo, kutajengwa barabara ya juu ya ghorofa tatu ili kuwezesha magari mengine kupita juu, mengine katikati na mengine chini ili kupunguza msongamano.

AKUMBUKA ALIVYOANGUKA NA CHOPA DAR
Kuhusiana na uteuzi wa baraza lake la mawaziri, Magufuli alisema atateua mawaziri wachapakazi na si wale wa kukaa ofisini huku shughuli nyingi za maendeleo zikikwama.

Alisema anataka mawaziri atakaowateua kuiga mfano wake kwa kushinda kwenye miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Dk. Magufuli alisema kama yeye angekuwa mtu wa kushinda ofisini na kutoa maagizo, huenda barabara za lami zinazofikia kilomita 17,000 zisingekuwapo kwani makandarasi wengi walionyesha uzembe aliwafukuza.

“Kama mimi nilianguka kwenye helikopta (chopa) nikikagua mafuriko Dar es Salaam, nikalala daraja la Dumila Morogoro, nao wafanye hivyo…kama ni Waziri wa Maji, basi ashinde kwenye miradi ya maji, kama ni barabara basi ashinde barabarani kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango,” alisema na kuongeza.

“Nikishinda na kuingia Ikulu nitakuwa nawahoji mawaziri nitakaowateua kama watamudu majukumu yao ama la na yule atakayekubali kwamba anaweza basi atasaini na akishaini ole wake nimpe kazi halafu ashindwe kumudu majukumu yake.”

APATA MAPOKEZI MAKUBWA UKONGA
Mgombea huyo wa CCM alipata mapokezi ya aina yake alipowasili Jimbo la Ukonga akitokea Kisarawe kwenye mkutano wake wa kwanza.

Umati ulijitokeza, wengi wao wakiwa na pikipiki, bajaji na wengine wakitembea miguu walikuwa wakimsubiri njia panda kuelekea kwenye mkutano huo.

Kutokana na idadi kubwa ya watu aliowakuta kwenye makutano hayo, Dk. Magufuli alilazimika kusimamisha msafara na kuzungumza na wananchi hao akiwaomba wamchague.

“Nawashukuru sana kwa mapokezi makubwa, kwa kweli mmefunika nisingeweza kupita bila kuzungumza na umati kama huu…mimi naomba kuwa rais wa Watanzania wote hivyo bila kujali vyama vyenu nipeni kura niwe rais wa awamu ya tano,” alisema Dk. Magufuli.

AWAPIGA KIJEMBE WANAOFAGIA BARABARA
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwashangaa wanaopiga deki barabara za lami ili wagombea wao wapite huku wakibeza kwamba serikali ya CCM haijafanya lolote.

Aliwataka waendeleze utaratibu wa kupiga deki barabara ili ziwe safi hata baada ya uchaguzi ili kuwaonyesha ni namna gani serikali ya CCM imejenga barabara nyingi za lami.

“Huwezi kupiga deki barabara ya vumbi, huwezi kupiga deki barabara yenye mashimo, wanatusema wakati wanapita kwenye barabara hizo hizo za lami tulizojenga,” alisema Magufuli.

Hivi karibuni, baadhi ya wananchi wa mji wa Musoma mkoani Mara walijitokeza kupiga deki barabara kabla ya kutumiwa na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa. Mbali na Chadema, Ukawa inaundwa na CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
CHANZO: NIPASHE

7 comments:

Anonymous said...

Itakuwa kazi kuanzia kamati kuu ya CCM hadi tawi itakuwa haina mtu
Lowassa Lowassa and Ukawa he is coming to us

Anonymous said...

Wewe kweli umefulia badala ya kutuonyesha picha za leo unatuwekea clip ya siku zilizopita. Utashishwa na Mafisi em yako unayoyapigia kampen.

Anonymous said...

Tubafurahi unapolisema hilo mheshimiwa. Ila kusema ukweli wameshaota sugu na wanajua mbinu zaidi unavyodhani japokuwa ulikuwepo ndani ya system kama hujapata mgawo huwawezi. Ukiwa ndani hutawaweza na watakufanya ushindwe kutumikia Taifa. Kila kukicha mazungumzo ni wiziwizi wizi wizi ni wimbo hadi bungeni na ulikuwepo huko uligasikia wapinza i wakisema kila siku. Ilibidi nawewe uungane kuyakemea mlemle ndani. Unapoanza leo ni sawa na unaposema barabara ya juu zinaanza mwezi ujao!! Haiingii akilini mwa wapenda maendeleo. Sio lazima tuambiwe ni swala la kuanza zilikuwa ziwepo miaka mingi tu mbona fedha ipooh.

Anonymous said...

Atapambana vipi na mafisadi wakati yeye mwenyewe anatokea huko ufisadini.

Unknown said...

Magufuli ni jembe la uhakika sijui tena watanzania wanataka kiongozi wa aina gani? Lakini kwa uwezo wa kufanya kazi. Kwa uadilifu na utumishi wa umma uliotukuka. Kwa uzoefu wa kazi katika wizara mbali mbali na jinsi alivyozitumikia hizo wizara kwa uadilifu na ufanisi wa hali ya juu. Ni mtu ambae anakifahamu kila kitongoji. Kila kata. Kila tarafa ya Tanzania na matatizo ya wananchi wanaoishi katika sehemu hizo . Hana skendal hana majungu yeye kwake ni kazi tu. Ni msomi wa kiwango cha PHD na ni mtaalam wa hisabati (mathematical genius) na Na ni mkemia wa kiwango cha juu aliebobea nchini. Magufuli anaposema anataka Tanzania ya viwanda anajua anachokisema. Tanazania ina madini ya chuma yenye uwezo wa kuchimbwa kwa miaka mia nne, 400yrs production non stop na tumesikia raisi kikwete yupo mbioni kwenda kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho cha chuma. Kwa hivyo kama tutazalisha chuma kwanini tusiwe na viwanda? Tunahitaji mtu makini kiwango cha magufuli. Tanzania ina madini ya kutengezea nyukilia ya kumwaga,watafiti wanasema utafiti wa uchunguzi wa sehemu zote zenye madini hayo ikikamilika nchini kuna uwezekano Tanzania ikawa nchi ya kwanza duniani yenye kiasi kikubwa ya( uranium) . Magufuli kaja wakati sahihi kwani hakuna faifa lilopiga hatua duniani bila ya taaluma na maarifa ya nuclear technology. Huwezi kuwa na umeme wa uhakika na salama kama huna nuclear . Ni recipe ya maendeleo ya nchi iliodhibitiwa na mataifa yalioendelea kuyabania mataifa mengine tokuwa na nguvu za nuclear lakini kiukweli nuclear ndio kila kitu kwa maendeleo ya nchi. Sasa Tanzania tumejaliwa kuwa na madini mbao bila ya hayo madini huwezi kuwa na nuclear . Tuna ( yellow cake) yakumwaga kama inavyojulikana na mataifa yalioendelea. Na kwa bahati nzuri tunamgombea mtaalamu katika fani hiyo ya nuclear sasa watanzania tunataka nini hata kama mimi ningelikuwa Edward Lowasa basi ningewashauri wafuasi wangu wamchague Dr Magufuli kwa manufaa ya Taifa ukweli ndio huyo Magufuli yupo vizuri katika kukata kiu yetu ya kumpata mtu atakae iongoza nchi yetu katika maendeleo ya kweli. Katika suala la uranium ningeshauri mwekezaji yeyote atakeingia ubia wa uzalishaji lazima serikali imlazimishe katika suala la kujenga vinu vya kuzalisha umeme vya nuclear hapo ndipo Tanzania na watanzania tutasahu kero zote za maendeleo na maisha ya watu zinazo kwamishwa na kutokuwepo na umeme wa uhakika kwani umeme wa uhakika duniani kote hasa nchi zilizopiga hatua ya kimaendeleo unatokana na nguvu za nuclear. Kwa hivyo Tanzania ya magufuli ni Tanzania ya viwanda na bila shaka hata kidogo uwezo tunao, nguvu tunazo, rasilimali tunazo na watu wa kusimamia kama akina Magufuli tunoa kipi watanzania kitakachotuzuia nchi isiwe the best beacon of Africa lakini kabla ya hapo tuache ushabiki tuchague viongozi makini itakapofika tarehe 25 mwezi huu. Mungu ibariki Tanzania. Amen.

Anonymous said...

Fisadi wa kwanza wa kumfanyia kazi awe Lowasa. Amfikishe Lowasa kizimbani ili wananchi watendewe haki. Karibu Rais Magufuli, tunakusubiri kwa hamu!

Anonymous said...

CCM oyeeeeeeeee!!!!!!!!!!