ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 22, 2015

SIMBA MSIPIGE MILUZI, SIO MAHALA PAKE


Na Nicasius N Agwanda (Nicasius Coutinho Suso)

Wakati wa ukuaji wangu sikufanikiwa kufaulu masomo ya Sayansi kwa kiwango sahihi, nasema sikufanikiwa kwa sababu walimu na wazazi waliamini ninaweza lakini ule uvivu wa kutokupenda kujisomea na kuhisi kuwa kila mara kutakuwepo na njia nyepesi kuliko ile ya kusoma kwa nguvu nyingi.
Ila hii ni akili ambayo nililishwa, haikuwa yangu, ilikuwa ni elimu ambayo niliipata kwa wale nilioongozana nao kila wakati. Sijutii kwa sababu ndio njia niliyoichagua ila nakumbuka kuwa ilikuwepo njia ambayo ingenifaa pia, ila huku nako ni sahihi nilipo.

Hili suala halina tofauti kubwa sana na usajili, unashauriana na wanaokuzunguka, hutakiwi kusikiliza mashabiki au kuwapa nafasi sana, unatizama mahitaji yako kisha unafanya chaguo sahihi ambalo muda mwingi huwa limeambatana na tafiti zilizokuwa sawa.

Tukirudi uwanjani wasahihishaji wako wanakuwa wapinzani wako wewe mwenyewe, na mashabiki wanabaki kuwa wazazi ambao watachukizwa ama kufurahishwa na mwenendo wa mwana.

Nilikuwa natizama usajili wa Simba, naam hawako mbali sana katika msimamo wa ligi, wapo jirani hasa kama isingekuwa akili nzuri ya Tambwe, inawezekana wangekuwa mahala salama zaidi ya klabu nyingine yoyote. Lakini bado kuna kitu kinanirejea kichwani juu ya aina ipi wanayoondokea.

Je wanaenda kwa tabia za upepo au ni ule mwendo wa risasi? Upepo hutembea kadiri ya uelekeo, muda wowote za kusi huweza kuelekea magharibi, tofauti na risasi ambayo daima hufuata uelekeo wa mtutu.

Ukiachilia mbali nafasi tofauti ndani ya uwanja, akili yangu imetua katika eneo la ushambuliaji. Kuna namna mbili za usajili katika eneo hilo katika soka la kisasa.

Mosi ni upate mshambuliaji wa kati anayekupa uhakika wa magoli mengi(alivyokuwa Tambwe), au upate mshambuliaji wa pembeni au mshambuliaji wa pili anayekupa magoli mengi kuliko mshambuliaji wa kati hivyo kuziba au kuweka mbadala wa magoli ya mshambuliaji wa kati(kama ilivyokuwa okwi), bahati nzuri wengine hufika mbali zaidi na kuwa nao wote kwa wakati mmoja (kama Msuva na Tambwe msimu uliopita Yanga).

Tofauti na hapo utakuwa unakumbatia mbuyu, au utaishi katika filosofia ya miaka nenda rudi inayofahamika kama unfinished Rebuilding (ujenzi usiokwisha), bahati mbaya sana huwezi kuwa mjenzi mzuri ndani ya uwanja wakati kiuchumi, kimasoko, uboreshaji wa chapa, na miundo mbinu haipo katika hali nzuri na inayokidhi mahitaji.

Sina tatizo na Mgosi, sina kuhitilafiana na Ndaw pia, lakini nabaki na swali kama je, hivi ni vipande ambavyo Simba ilikuwa inavikosa ili kuunganisha katika lile zuria lililokuwa limetandikwa tayari, je hii ilikuwa nyongeza (squad players) au ilikuwa ni usajili stahiki (marquee signings)?

Wakati unamuuza mchezaji wako bora Okwi, unahitaji kariba yake ndio iwe mbadala, lakini kwa sababu haukuwa miongoni mwa waliokuwa bora msimu uliomalizika, unahitaji mshambuliaji mwingine bora kuongezea katika safu yako na kumsukuma vyema kinda Ibrahim Ajib na kumpunguzia presha za kuhitaji matokeo. Hapa namaanisha sio dhambi klabu kumiliki washambuliaji watatu bora kwa wakati mmoja.

Kwa umri wa Mgosi hakuna shaka kuwa alionyesha kiwango bora akiwa Mtibwa lakini huku majukumu hayakupaswa kuwa yake, alistahiki kuwa ziada iliyo bora kuliko kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza moja kwa moja.

Hii ingempa nafasi kubwa ya kuwa hatari zaidi, hii ingempa fursa ya kutoa athari za Mtibwa, nani kakwambia utampata Mgosi yule aloweza kukupa kiburi cha kumwacha Samata agomee gari kwa wakati huu?

Bahati mbaya zaidi unampa na unahodha, unahitaji awe kiongozi wa mfano na mtendaji (leading by example) au uongozi wa kimalkia pale Uingereza yaani (ceremonial leader), huu anao hata Mikel Arteta pale Arsenal lakini ni mpole, anaufanyia kazi jirani na kocha katika benchi, yaani unapewa kwa heshima tu lakini kule ndani kuna waziri mkuu ambaye anahakikisha kila mtu yupo salama, anaitwa Per Metersacker. Tanzania inabidi tuishi katika misingi sahihi ya soka la kisasa.

Simsemi sana Ndaw, lakini kutokumuona uwanjani kwa dakika nyingi, tukio la mechi ya watani linaniwazisha sajili za siku zote, narejea maisha Mbiyavanga na mwenzake. Napenda Hamis Kiiza anachokifanya, lakini sifurahishwi na anachopewa.

Alihitaji msaada zaidi, alihitaji mtu wa kumfanya asipewe umakini mkubwa zaidi, mtu wa kumpunguzia kashikashi za wapinzani, mtu wa kumpunguzia mzigo pale akiwa hayupo katika kiwango bora, na mtu wa kuibeba Simba ikiwa ameumia kama ilivyo sasa.

Maisha yanaendelea, Simba inashinda, shukrani kwa kiwango bora na mwendelezo kwa wachezaji, hata kama una bahati lakini huwezi kufunga bila ya kushambulia, lakini kuna muda inabidi uwe na wivu tu. Lazima utamani kuwamiliki Busungu, Tambwe na Ngoma kwa pamoja huku ukiwa na Msuva mkono wako wa kushoto. Mnyama anaunguruma lakini napata shaka na malisho yake, sijui kama ana nguvu ya kutosha ya kuwala wanyama korofi, Mbeya City ni korofi iliyodhoofu kiafya.

Safari hii mkifika salama ni kheri, ikishindikana bahati mbaya pia, lakini hakuna namna inatakiwa mipango na kamati zenu zisiwe za muda mfupi (Ad Hocs), ziwe za muda mrefu na zinazosimama (standing plans).

Hakuna kitu cha bei rahisi na ambacho vilabu vinavyoendelea duniani vinawekeza kama scouting (utafutaji vipaji) yaani mara elfu nane kuliko majaribio ya kila mwaka ya hawa wachezaji wageni, maisha ya Youtube yaacheni kwa wale wanaokaa majukwaa ya njano na bluu.

Nasikia kuna ile namba mliyoipuuza ipo inafanya kazi kituo cha mabasi kwa umakini sana, msiitizame tena, wala msipige mluzi maana midomo yenu ina maji na mpaka myameze sekunde zitakuwa zimekatika, na mashavu yameloa. Bahati mbaya hata jirani zenu wale wanaweza kurudia haya yenu msimu kesho, si unajua binadamu tunaweza kukuna kisogo tusichoweza kukitizama kwa kuhisi kina ushabihiano na kiganja.

Ahsanteni.

Instagram: @Nicas.coutinho

No comments: