ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 22, 2015

HII NDIYO YANGA SC INA KIKOSI BORA ‘KILICHOSHIBA’


Mlinzi wa kati wa Yanga Vicent Bosou ambaye amecheza kwa dakika zote 90 kwa mara ya kwanza wakati Yanga ikicheza dhidi ya Toto Africans 

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam

Licha ya wachezaji wake kuendelea kuendelea kukosa kujiamini wapatapo ‘mkwaju wa penati’, washambuaji wa Yanga SC ameendelea kufunga magoli ya kutosha na kujikita katika kilele cha msimamo. Mlinzi wa kulia, Juma Abdul alifunga goli ‘maridadi’ la mkwaju wa mita zisizopungua 23 mapema dakika ya 9’ wakati Yanga ikicheza na Toto Afrika kwenye uwanja wa taifa Jumatano hii.
Juma alifunga akimalizia mpira wa kona fupi uliopigwa na Haruna Niyonzima. Namna Toto Africans walivyoendelea kucheza licha ya kufungwa goli la mapema usingedhani ni timu ambayo wiki moja iliyopita wachezaji wake waligomea kufanya mazoezi pamoja na kutishia kutokwenda Nangwanda Sijaona, Mtwara kucheza na Ndanda FC siku ya Jumamosi iliyopita.

Walitulia na kuendelea kujiamini dhidi ya Yanga, Hassan Khatib, Robert Magadula, Hamis Kasanga, Carlos Prostus walicheza vizuri katika safu ya ulinzi na kuwabana sana washambuaji watatu wa Yanga, Amis Tambwe, Malim Busungu na Donald Ngoma. Ni Vijana wadogo lakini walicheza kwa kujiamini kiasi cha kuufanya mchezo kuwa na magoli yasiyo tarajiwa.

Yanga waliendelea kuandamwa na ‘mzimu’ wa kukosa penati. Ngoma alishindwa kuifungia timu yake goli la pili baada ya kiki yake kudakwa na mlindunga mlango aliyewabeba sana Toto, Musa Mohamed dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.

Dakika mbili nyuma Miraji Athumani alishindwa kuisawazishia timu yake baada ya kuwekewa pasi ‘murua’ na Edward Christopher. Kiki dhaifu ya kijana huyo ilipanguliwa na Ally Mustapha lakini tayari walikuwa wamejenga hali ya kujiamini.

Wengi walitaraji kushuhudia mechi ya upande mmoja lakini Toto ikiwa na vijana wanne kutoka kikosi cha vijana cha Simba SC 2012 ( Edward, Miraj, Abdallah Seseme na Khatib) ilicheza kandanda safi sana na kuipendezesha gemu hiyo.

Mfungaji wa goli la kuongoza upande wa Yanga, Abdul aliumia na nafasi yake ikachukuliwa na kiungo-mshambulizi Saimon Msuva. Busungu akarudi kucheza beki 2 na Yanga ikapata goli la pili lililofungwa na Msuva dakika nne baada ya kuingia uwanjani. Goli hilo halikuwavuruga sana Toto kwani walijitahidi kucheza kwa kupasiana na kufanikiwa kupata goli la kufutia machozi kupitia kwa Miraji.

YANGA KILA MCHEZAJI SAFI

Andrey Coutinho aliingia kuchukua nafasi ya Geofrey Mwashuiya na M-togo Vicent Bossou alicheza kwa dakika 90 kwa mara ya kwanza na kuwaziba mdomo wale ambao walikuwa wakibeza usajili wake wa gharama kubwa zaidi katika ligi kuu bara. Mlinzi huyo wa kati anajua kuutumia mwili wake mkubwa, si mzito na mtu mwenye uwezo wa kuondoa vizuri mpira katika eneo lake la hatari.

Ni ngumu kwake kuingia moja kwa moja kikosini kwa kuwa tayari nahodha, Nadir Haroub na Kelvin Yondan wametengeneza umoja imara wa muda mrefu klabu hadi timu ya Taifa. Ila Vicent ni beki ambaye klabu kama Yanga inapaswa kuwa naye hasa kulingana na ukweli kwamba Nadir na Kelvin wamekuwa na majeraha ya mara kwa mara.

Alicheza vizuri na Kelvin na alipoingia Nadir hali ikaendelea kuwa vizuri kwa safu ya ulinzi ya Yanga. Mbrazil, Coutinho aliifanya Yanga kucheza kwa kasi zaidi ndiyo maana walifunga magoli mawili kwa mipira ya ‘kuunganisha moja kwa moja’. Msuva alimpa pasi maridadi Tambwe ambaye alifunga goli lake la tano msimu huu dakika ya 81’.

Coutinho akamtengenezea Msuva kwa stahili ile aliyofunga Tambwe na mfungaji bora wa msimu uliopita akafunga kwa mara ya pili katika gemu dhidi ya Toto huku likiwa goli lake la tatu msimu huu. Yanga walistahili kushinda zaidi lakini uimara wa kipa Musa uliwanyima magoli zaidi.
Credit:ShaffihDauda

No comments: