Tuesday, October 27, 2015

Vurugu zaibuka Zanzibar, Bara

By Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Zanzibar, Dar, mikoani. Vurugu zimeibuka katika baadhi ya mikoa ya Bara na Zanzibar, hali iliyowalazimu polisi kutumia nguvu ikiwamo kurusha mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Upande wa Zanzibar hali hiyo ilianza kuonekana baada ya mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kuitisha mkutano na wanahabari na kutangaza matokeo aliyosema ameyakusanya kutoka kwa mawakala wa chama hicho waliokuwa vituoni.

Kutokana na hali hiyo, polisi waliweka kambi kwenye maskani ambayo hutumiwa na wafuasi wa CCM na CUF katika eneo la Msonge Michenzani.

Polisi walifanikiwa kuimarisha ulinzi ikiwemo kuwatia mbaroni, walioonekana kushiriki vurugu hizo.

Dar na mikoni. Polisi katika maeneo mbalimbali, walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wakifanya vurugu katika vituo vya kupiga kura.

Mkoani Dar es Salaam, vurugu na mabomu ya machozi yalidumu kwa takribani saa tatu katika eneo linaloizunguka ofisi ya Kata ya Charambe ambako wananchi walikuwa wanasubiria matokeo.

Wananchi waliokuwa katika vikundi maeneo ya Mbagala jana walikusanyika katika ofisi za kata ya Charambe tangu saa tatu asubuhi wakisubiri matokeo.

Kundi hilo kubwa la wafuasi walizidi kukusanyika hali iliyosababisha vyombo vya usalama kufika eneo hilo kwa lengo la kulinda usalama.

Eneo la Ubungo mataa nako kuliibuka vurugu baada ya vijana kuziba barabara ya Mandela na kuzuia magari, hali iliyozusha sintofahamu na kuwalazimu polisi kufika na kufyatua mabomu ya kutoa machozi, ikiwamo kuwakamata baadhi yao waliokuwa wakiwarushia mawe polisi.

Mkoani Tanga, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walilazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wakazi wa kata za Duga na Mwanzange.

Vurugu hizo zilianza baada ya wakazi wa Kata ya Duga, kukusanyika wakishangilia ushindi wa Khalid Rashid wa CUF aliyeongoza kwa kupata kura nyingi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Zubery Mwombeji alilazimika kupeleka askari eneo hilo, kwa sababu wananchi waliweka mikusanyiko iliyokuwa ikiwaletea fujo wasimamizi wa uchaguzi na kushindwa kutenda kazi zao kwa hatua za mwisho.

Mkoani Morogoro, polisi waliwatawanya wafuasi wa chama kimoja kwa mabomu ya machozi na kumwaga maji ya kuwasha baada ya kufunga barabara ya Morogoro-Iringa kwa kile walichodai kutokubaliana na matokeo ya udiwani kata ya Chamwino.

Tukio hilo lililoambatana na vurugu lilitokea jana saa nane mchana na kudumu kwa zaidi ya saa mbili hali iliyolazimu polisi kuweka kambi katika eneo hilo huku wakiwa na silaha za moto, mabomu ya machozi, gari la maji ya kuwasha pamoja na mbwa.

Wakizungumza katika eneo hilo baadhi ya wafuasi hao, walidai kuwa hawana imani na matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa kata hiyo ambayo yalimtangaza Makanjira wa CCM kuwa ni diwani wa kata hiyo ya Chamwino.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa polisi Wilaya ya Morogoro, OCD Peter Nsato alimtaka mgombea udiwani huyo kuzungumza na wafuasi wake ili waweze kutulia wakati suala hilo likishughulikiwa na Tume ya Uchaguzi ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi katika kata hiyo.

Mabomu ya machozi

Kutoka Mbeya, kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya udiwani, ubunge na urais kaika majimbo ya Kyela, Rungwe na Mbozi jana kulisababisha vijana waanze kuwatupia mawe polisi na hatimaye kurushiwa mabomu katika matukio tofauti.

Katika Jimbo la Kyela, suala la uhakiki wa kura zilizua taflani kwa vijana kuwarushia mawe polisi waliolazimika kufyatua mabomu ya machozi.

Hali kama hiyo ilitokea pia katika Mji wa Tukuyu Jimbo la Rungwe ambako baadhi ya vijana walikusanyika wakisema hawakubali matokeo.

Kutoka Ruvuma, polisi inawashikilia watu zaidi ya 15 na kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wengine waliokusanyika karibu na ofisi ya Manispaa, wakishangilia ushindi wa mgombea wa Chadema Joseph Fuime. Hata hivyo matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa katika jimbo hilo yanaonyesha aliyeshinda kiti cha ubunge ni Leonidas Gama wa CCM.

Imeandikwa na Brandy Nelson, Justa Musa, Stephano Simbeye, Elizabeth Edward na Buruhan Yakub na Joyce Joliga.
MWANANCHI

No comments: