TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Agizo alilolitoa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka
fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kugharamia hafla ya
wabunge zipelekwe Katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia
vitanda na magodoro ya wagonjwa wanaolala chini limetekelezwa.
Katibu Mkuu
Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema fedha hizo zimefanikisha kupatikana
vitanda 300 vya wagonjwa pamoja na magodoro yake, shuka 600, Baiskeli za
kubebea wagonjwa na vifaa vingine na kwamba hivyo vyote tayari vimepelekwa
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Balozi Sefue
ameuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha vitanda vyote vinafungwa kesho
jumapili na kwamba atakwenda kuvikagua siku ya jumatatu vikiwa tayari
vinatumiwa na wagonjwa waliokua wanakosa vitanda vya kulalia na kulazimika
kulala chini.
Wadau mbalimbali
walichanga fedha kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla
ya wabunge baada ya uzinduzi rasmi wa bunge la 11 lakini Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliagiza fedha hizo zitumiwe kwa
kiasi kidogo kisichozidi shilingi milioni 15 na nyingine zipelekwe hospitali ya
Muhimbili kutatua tatizo la uhaba wa vitanda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi
wa Mawasiliano IKULU,
Novemba 21, 2015.
No comments:
Post a Comment