Iringa. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Iringa Mjini kitaanza kufanya vikao vya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa hiyo, kwenye eneo la bustani lililo wazi ili kutoa nafasi kwa wananchi kuhudhuria.
Hatua hiyo inakuja baada ya Chadema kuwa na uhakika wa kushinda nafasi ya meya na naibu meya baada ya kupata viti 21 vya madiwani wakiwamo 14 wa kuchaguliwa, huku CCM ikiambulia viti vitano.
Akizungumza wakati akiwatambulisha madiwani wateule wa chama hicho kwa waandishi wa habari, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema kupitia vikao hivyo, wananchi watapata fursa ya kujua namna madiwani wao wanavyowawakilisha kwenye vikao.
“Vikao vyote vya baraza la madiwani vitafanyika kwenye bustani ya manispaa isipokuwa vile vinavyotakiwa kufanyika ndani, tutavipeleka ukumbini,” alisema Mch Msigwa.
Alisema tayari wamekamilisha mchakato wa awali wa kumteua diwani atakayegombea nafasi ya meya na naibu wake na kinachosubiriwa ni uamuzi wa Kamati Kuu.
Alimtaja Diwani wa Isakalilo, Alex Kimbe kuwa ndiye aliyeongoza kwenye mchakato huo akitarajia kubadili historia ya Jimbo la Iringa Mjini kwa Chadema kuongoza halmashauri, ikiwa jina lake litapitishwa kwenye vikao vya juu.
Alimtaja Diwani wa Kwitwiru, Baraka Kimata kuwa alishika nafasi ya pili huku Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Iringa, Frank Nyalusi akishinda nafasi ya tatu.
Kwa upande wa nafasi ya naibu meya, Diwani wa Kwakilosa , Joseph Lyata aliongoza akifuatiwa na Diwani wa Mkimbizi, Evarist Mtitu wakati Diwani wa Gangilonga, Dadi Igogo alishika nafasi ya tatu.
Mchungaji Msigwa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema kazi ya chama hicho kwenye jimbo ni kupendekeza jina la mgombea na kuliwasilisha kwenye kwenye vikao vya juu vyenye uamuzi wa kuteua mgombea mwenye sifa.
Aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi, Desemba 2, wakati madiwani hao watakapokuwa wanaapishwa tayari kwa kuanza kazi yao ya kuwatumikia.
Nyalusi alikiri kuwa mchakato ndani ya chama hicho uliambatana na mgogoro lakini akasisitiza kuwa suala hilo limekwisha.
“Unapofanyika uchaguzi unaohusisha watu zaidi ya watatu lazima kutakuwa na makundi. Tumemaliza makundi yote na sasa wote tumebaki kuwa wamoja” alisema Nyalusi.
Awali, katibu wa Chadema wa Wilaya ya Iringa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Mgonokulima alisema chama hicho kimefuata taratibu na miongozo ya kuwapata wagombea.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment