ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 24, 2015

Mchakato wa kunyang’anya mashamba, viwanja waanza



Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru.
By Suzan Mwillo na Julius Mathias, Mwananchi

Dar es Salaam. Mchakato wa kunyang’anya mashamba na viwanda kutoka kwa wamiliki walioshindwa kutekeleza masharti waliyopewa na Serikali umeanza.

Taarifa zilizofikia gazeti hili, zimeeleza kuwa miongoni mwa mashamba na viwanda hivyo ni kutoka mkoani Morogoro, Lindi, Arusha, Mbeya, Tanga, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilitoa tangazo kwa wawekezaji walionunua viwanda na mashamba ya Serikali ikiwakumbusha kurejea kwenye mikataba yao.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru (pichani) ilieleza kuwa inarejea mikataba yote ya mauzo ya viwanda na mashamba iliyoingiwa kupitia Mpango wa Ubinafsishaji na kwamba kuna wawekezaji wamekiuka masharti ya mikataba yao.

Miongoni mwa masharti hayo yaliyokiukwa ni kutoendelezwa viwanda na mashamba kwa mujibu wa mikataba, kushindwa kutekeleza mpango wa uwekezaji, baadhi ya wanunuzi kuuza mashine walizozikuta bila kurudisha mashine mbadala, kutokamilisha malipo ya ununuzi wa viwanda na mashamba na kubadilisha matumizi ya viwanda na mashamba bila idhini.

“Ninawaagiza wawekezaji wote walionunua viwanda na mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wawasilishe taarifa zao za sasa ndani ya siku 30, kinyume na hapo Serikali itachukua hatua stahiki ikiwamo kurejesha viwanda na mashamba hayo kwenye miliki yake,”ilisema taarifa hiyo.

Lakini zikiwa zimebaki siku 24 kwa tangazo hilo kufika kikomo taarifa zinaeleza kuwa tayari mashamba yameanza kurejeshwa kwenye umiliki wa Serikali, kwa madai ni utekelezaji wa agizo la Serikali.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata akizungumzia taarifa hizo za kuanza kurejeshwa kwa baadhi ya mashamba alisema hawezi kutoa maelezo kuhusu madai hayo kwa kuwa hana taarifa nayo.

Lakini alisema anatambua kwamba mambo yanaendeshwa kwa sheria na taratibu zake tofauti na madai ya taarifa hizo.

“Sidhani kama mtu anaweza kuamka tu na kusema hili lifanyike. Lazima taratibu zifuatwe,” alisema Kidata.

Hata hivyo, Kidata alifafanua kuwa wizara hiyo imekuwa ikiendesha ikirejesha ardhi serikalini kutoka kwa wamiliki walioshindwa kuendeleza masharti.

Alisema mtu anapopewa dhamana ya kumiliki ardhi, dhamana hiyo huambatana na masharti ikiwamo kuendeleza na anaposhindwa hunyang’anywa.

“Lakini kabla ya kufanya hivyo hupewa notisi na asipoifanyia kazi uamuzi wa mwisho ni kuichukua,”alisema Kidata.

Alisema Serikali chini ya wizara hiyo itaendelea kufanya hivyo kama wamiliki watakiuka masharti wanayotakiwa kufuata.

Kwa upande wake, Mafuru alisema serikali imetoa tangazo hilo na kuwapa wahusika siku 30 ili ndani ya muda huo, wajipange na kuandaa taarifa za utekelezaji wa miradi waliyopewa kuiendesha.

No comments: