ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 16, 2015

Mkwasa akiri kosa, wadau wamtetea

Dar es Salaam. Wakati mashabiki wakimshushia lawama kocha wa Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa kutokana na sare ya mabao 2-2 iliyopata Stars dhidi ya Algeria, makocha na wachambuzi wa soka nchini wamemtetea wakidai hapaswi kuangushiwa mzigo wa lawama kutokana na matokeo hayo.

Katika mchezo huo ambao Stars iliutawala kwa muda mrefu, ilishindwa kulinda mabao yake mawili na kuwaruhusu wageni kusawazisha ndani ya dakika tano.

Mashabiki wengi wa soka nchini wamekuwa wakililaumu benchi la ufundi kwa kufanya mabadiliko ya kuwatoa wachezaji Elias Maguli na Mudathir Yahaya na kuwaingiza Said Ndemla na Mrisho Ngasa mabadiliko ambayo yaliwarudisha mchezoni Algeria walioanza kutawala mpira na kusawazisha mabao hayo haraka.

Mkwasa alisema kikubwa kilichowaangusha ni bahati ya kukosa kutumia nafasi nyingi walizozitengeneza huku pia wakikosa umakini kwa muda fulani ambao uliwagharimu.

“Tumetengeneza nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia, tungeweza kupata mabao mengi, lakini kama ninavyosema kuwa lazima tukubaliane kuwa kuna wakati mpira unategemea.

“Vijana wamejitahidi, labda niseme kuwa tulifanya makosa pengine ya mabadiliko wakati ambapo tulishakuwa imara, lakini ni matokeo ya mchezo na nafikiri tuna mlima mrefu kwa sababu nilivyowatazama hawa wanaweza kuwa sio watu wazuri watakapokuwa kwao. Bado tunajenga timu na nadhani ndani ya muda fulani tutakuwa na timu nzuri kama wao,” alisema Mkwasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wametaja kasoro zilizoigharimu Stars kwenye mchezo huo na kumtaka Mkwasa kuziangalia kabla ya mchezo wa marudiano kesho mjini Blida, Algeria.

Liewig: Ni kawaida kocha kukosea

Kocha wa Stand United, Mfaransa Patrick Liewig alisema, “Timu imecheza vizuri na sikuona kosa la kocha katika mabadiliko yale aliyoyafanya kwa sababu sisi makocha tunakuwa na mipango na mbinu zetu ambazo si kila wakati zitafanya kazi.”

“Nadhani tatizo kubwa kwa Stars lilikuwa kutoimaliza mechi tangu kipindi cha kwanza ambacho walipata nafasi nyingi wakashindwa kuzitumia,” alisema Liewig.

Mayai: Uzoefu tatizo

Nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema uzoefu wa mechi kubwa ulionekana kuanzia kwa wachezaji hadi benchi la ufundi chini ya kocha Mkwassa.

“Uzoefu wa mechi kubwa kama ya Algeria ulikuwa bado tatizo kwa timu yetu, kwa kocha hakujua nini cha kufanya kila mchezo ulivyokuwa ukienda jambo lililofanya wachezaji kupoteza mwelekeo,” alisema Ally Mayay.

Mayay alisema kutokuwa na mbinu ya mchezo pia ilikuwa kasoro nyingine kwa Stars, kwani jinsi ilivyoanza mechi hiyo ndiyo ilivyoendelea kucheza kipindi cha pili tofauti na wapinzani wao.

Mwaisabula: Kukosa mipango

Kenny Mwaisabula alisema katika mchezo huo, Stars pia ilikosa mipango ya kutumia muda kama ilivyokuwa kwa wapinzani wao ambao katika dakika 90 za mchezo ilicheza na muda na kubadirisha mchezo kila baada ya dakika 15.

“Dakika 15 za kwanza Algeria ilicheza taratibu bila parapara yoyote, dakika 15 zingine ilicheza kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza na dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza ilicheza mpira wa polepole.

“Ilivyorudi kipindi cha pili, ilianza kwa mashambulizi ya nguvu, ikabadirika na kucheza mpira wa taratibu kuanzia dakika ya 61 kisha ikaanza kucheza kwa kupoteza muda dakika 15 za mwisho, hii ilikuwa ‘game plan’ yao tofauti na sisi hatukuwa na mpango wowote,” alisema.

Chambua: Tatizo makocha wetu

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekolojo Chambua alisema ni wakati wa makocha wanaozinoa klabu za Ligi Kuu Bara kujifunza kwa makocha wa nje.

Akifafanua kauli yake Chambua alisema kwa jinsi alivyoshuhudia mechi ya Stars na Algeria, amebaini tatizo la wachezaji kukosa elimu ya umakini kutoka kwenye klabu zao tofauti na wapinzani waliokuwa wanapambana kusaka matokeo.

“Hakuna Stars bila klabu za Ligi Kuu Bara, hivyo hatuwezi kumbembesha mzigo kocha Mkwasa, kwani yeye anakaa na wachezaji kwa kipindi kifupi ingawa alikosea kumtoa Maguli na kumuingiza Ngasa,” alisema.

“Tumeona katika mechi za ligi wachezaji wanafanya vizuri dakika 45, zinazofuata kama timu imeshinda ni kuridhika siyo wapambanaji na ndiyo maana nawashauri makocha waige mfano kwa wema,” alisema.

Machupa: Wasife moyo

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Athumani Machupa aliipongeza Stars kwa kucheza soka la kiwango cha juu tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Stars imefanya vizuri ila nashangaa kwa nini kocha Mkwasa alifanya mabadiliko yalioigarimu timu, lakini wasife moyo wanatakiwa kupambana,” alisema.

Alisema wachezaji wa Kiarabu wanatumia akili kuliko nguvu kwani huwezi kuona kwamba wanafanya kitu uwanjani unakuja kushtukia wamefanya madhara kama walivyowafunga kizembe.

“Hawakuja na mastaa wao wote, kuna kikosi wamekiacha kwao kinachoendelea na mazoezi na sare ugenini kwa upande wao ni ushindi, hivyo Stars wanatakiwa kuongeza umakini zaidi,” alisema Machupa.
MWANANCHI

2 comments:

Anonymous said...

Algeria walisawazisha lakini mtaalam yeyote aliyeona ile mechi Stars ilikuwa timu bora zaidi. Mimi sikupendezwa na ile substitution lakini Stars walicheza mpira mzuri sana shida ni walikosa magoli mengi sio vizuri unapocheza na timu kubwa kama Algeria. Lakini Mkwasa kafanya kazi nzuri sana na stars timu ipo organized wanacheza kwa kujiamini kwa hiyo nampongeza sana kocha. Tumeenda hadi Brazil kutafuta makocha kumbe tunao nyumbani

Anonymous said...

mkwasa ni mzigo,hafai,hafai,hafai.yeye alikua ana bahati kubwa kwani anawaunganisha wachezaji ambao tayari walikua wanavipaji vizuri kutoka kwenye klabu zao.anashindwa kupanga team boniface,yaani ni mhujumu,hafai.akili yake ni upendeleo,upendeleo,upendeleo.kocha gani huyu majanga.AFUKUZWE,MFUKUZENI.ALGERIA TUNAKWENDA TUKIWA TAYARI TUMEKWISHA CHANGANYIKIWA.FUKUZA.kwenda zako.