Advertisements

Friday, November 27, 2015

TUONYESHE YAKO MISULI

BY MOHAMED MATOPE
Raisi ni Magufuli, onyesha yako misuli,
Hongera wastahili, taifa halina shari,
Tumekuchagua heri, Raisi usofedhuli
"Hapa kazi tu" iwe kampeni kweli.

Tinga tinga  mtamboni,shuhudie ujasiri.
Jina lako asili,kisukuma na Kiswahili.
Litumie kwamakini,vile linavyostahili
John Pombe Magufuli, hakuna wa kusaili.

Usiwe mlevi pombe, lakini shika kufuli.
Ambalo uzitumie, mafisadi kuhimili.
Ahadi utekeleze, muda umeshawasili.
Kufungua mahakama, kuhukumu ufisadi


Zulu hospitalini, Bugando na Muhimbili.
Fichua manesi, pamoja na madaktari.
Nafuu haipatikani,twameza dawa  feki
Tiba haitolewi, bila kuhonga shilingi.

Mfagio utumie, serikali ishamiri,
Wazembe uwafagie, na wasioficha siri,
Ofisi zao vijiwe, kama hawana mwajiri,
Mishahara kuchukua, bila kugusa faili.

Tuonyeshe wako mpini, chaguo la waziri
Zingatia utendaji, hapana rudisha fadhiri
Dira iwe maadili,wananchi watujali
Watuliao nyumbani,si ughaibuni kusafiri

Vamia idara mbili, za kodi  na Bandari
Ujionee  dhahili,walarushwa mashuhuri     
Wale wenye magari, na majumba ya fahari                                   
Uwaweke kizimbani, kama Mramba Basili

Plani utuwekee , ya misururu barabarani
Barabara uzikuze, reli na baharini,
Serikali uhamishe,itandae  miji mbali
Watumishi wapungue, usafiri uwe shwari,

Biashara ndogo  sapoti, na ajira za binafsi
Watumie wetu  wasomi, nchini tuwahimili,
Dumisha  kilimo madini,uvuvi  na utalii.
Utumie yetu gasi, kwa shule na hospitali



Tusafishie mazingira ili tuishi vizuri
Himiza miti panda, nchi isiwe Kalahari
Mazingira elimisha, kwenye yetu maskuli
Nchi iwe waridi, kama wenzetu Kigali.



Tamati  ndugu raisi,anza yako shughuli
Elfu mbili na ishirini, alama tutajadili
Tutakupatia  daraja ,ile unayostahili
Mchakato tupamoja, taifa lisonge mbele

1 comment:

Anicetus said...

Watanzania wanaoishi ugaibuni wote tuko pamoja ili nchi iendelee mbele