ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 3, 2015

Kamishna TRA afunguka tuhuma za ufisadi Uingereza

Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitillya.

Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitillya, ambaye anadaiwa kuhusika katika kashfa ya ununuzi wa dhamana ya serikali (hati fungani) zenye thamani ya trilioni 1.2, amefunguka kuhusiana na tuhuma hizo akisema kuwa muda muafaka ukifika ataeleza kila kitu.

Kitillya ambaye ni Mwenyekiti wa kampuni ya Egma iliyokuwa wakala wa ununuzi wa dhamana ya serikali wenzake, inadaiwa kuingiziwa Dola za Kimarekani milioni sita. Fedha hizo wanadaiwa kuzipata baada ya kujiongezea asilimia moja badala ya asilimia 1.4 na kuwa asilimia 2.4.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Kitillya alieleza kwa kifupi kuwa kwa sasa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa lipo katika uchunguzi.
Alisema muda mwafaka ukifika atalitolea maelezo suala hilo kwa kirefu, ingawa hakutaja lini atafanya hivyo.

“Kwa sasa sina comment (maoni) yoyote kwa kuwa suala hilo lipo katika uchunguzi, lakini muda ukifika nitalizungumzia,” alisema Kitillya na kukata simu.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema kwa sasa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa lipo katika uchunguzi.

Kayombo alisema kama fedha hizo zitarudishwa na serikali ya Uingereza na kukiwa na uwezekano wa TRA kuchukua kodi, watatekeleza mara moja.

KAULI YA GAVANA
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, alisema kwa sasa BoT haiwezi kuchukua hatua yoyote kwa kuwa ilishafanya kazi yake awali ya ukaguzi na kugundua ubadhirifu huo.

Alisema baada ya kugundua ndipo Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) nayo ikapata taarifa.

Alipoulizwa ni hatua gani BoT kwa sasa wanazichukua dhidi ya benki ya Stanbic Tanzania kuhusika mara kwa mara katika kashfa za fedha nchini ikiwamo kupitisha fedha za mgawo kwa watu walionufaika na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, Profesa Ndulu alisema hatua za kisheria haziwezi kuchukuliwa kwa benki husika bali kwa waliotenda kitendo hicho.

“SFO wao walipa taarfa kutoka kwetu mara baada ya kugundua, hata Oktoba 1, mwaka huu walituomba tuwapatie ripoti yetu katika kwa ajili ya kesi na tukawapa,” alisema Ndulu.

HOSEA: MASHTAKA YAIVA
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, alisema taasisi yake ilishaanza uchunguzi wa suala hilo muda mrefu.

Alisema hivi sasa uchunguzi wa suala hilo umefikia hatua ya mashtaka ambayo kiutaratibu inatakiwa kufanyika baada ya kuwa na ushahidi usio na mashaka juu ya suala hilo.

Hata hivyo, Dk. Hosea aliliambia gazeti hili kuwa suala hilo linapaswa kufanyika kwa kwa umakini kwa kuzingatia kuwa linahusisha benki za kimataifa.

MGIMWA ATOA MAELEZO
Awali kulikuwapo na taarifa kuwa mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Fedha mwaka 2012/13, hayati Dk. William Mgimwa, Godfrey Mgimwa alitumwa na benki ya Stanbic akiwa kama mwajiriwa kwenda wizara ya fedha kupeleka nyaraka za dokezo la mkopo huo lililoonyesha kuwa riba yote ya asilimia 2.4 na kulitekeleza.

Akizungumza na Nipashe Mgimwa, ambaye ni Mbunge wa Kalenga, alikiri kuwa mwaka huo alikuwa mwajiriwa wa benki hiyo, lakini hakuhusika katika kupeleka dokezo lolote kwa baba yake (waziri wa fedha).

“Kama nilikuwa mfanyakazi wa kawaida wa Stanbic kipindi hicho, nisingepewa document (nyaraka) nzito kama hiyo kumpelekea waziri wa fedha hata kama alikuwa ni baba yangu,” alisema Mgimwa jana.

Jumatatu wiki hii, Mahakama ya London, Uingereza ilibaini ufisadi wa Sh. trilioni 1.3 zilizotokana na mkopo uliotolewa na benki ya Standard ya Uingereza kwa serikali ya Tanzania.

Mahakama hiyo iliamuru serikali ya Tanzania irejeshewe Dola za Marekani milioni saba, baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu huo.

Baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama hiyo na SFO, ilibainika kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni Dola milioni sita zililipwa kwa Egma ambayo inamilikiwa na Kitillya, ambaye kwa wakati huo alikuwa Kamishna Mkuu wa TRA.

Mmiliki mwingine wa kampuni hiyo ni Gasper Njuu na aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Soko la Mitaji ya Umma Tanzania, Dk. Fratern Mboya, ambaye kwa sasa ni marehemu.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, juzi alitoa taarifa ya serikali kuhusiana na sakata hilo na kusema kuwa baada ya uchunguzi kufanyika ilibainika kwamba Benki ya Uingereza iliitaka Tanzania ilipe mkopo huo na riba ya asilimia 1.4, lakini Stanbic Tanzania ilidanganya na kusema ulipwe asilimia 2.4 na asilimia moja ambayo ni nyongeza wakalipwa Egma.

NAMNA ILIVYOBAINIKA
Mwaka 2013 BoT ilikagua Benki ya Stanbic na kubaini kuwapo kwa malipo yasiyokuwa ya kawaida yaliyofanywa kwa kampuni ya Egma, ambayo yalikuwa kinyume cha taratibu za kibenki.

Fedha hizo Dola milioni sita ziliingizwa kweye akaunti ya Egma na ndani ya siku kumi fedha hizo zilitolewa na mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo marehemu Mboya.

Baada ya BoT kufanya ukaguzi huo walitoa taarifa kwa serikali ya Uingereza kupitia SFO ambayo ilianzisha uchunguzi ambao ulisababisha kesi kufunguliwa.

Hata hivyo Benki ya Standard Group ambayo ni benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri makosa hayo na kukubali kulipa faini ya Dola milioni 25.2 (Sh. bilioni 54) kwa kosa hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: