Wednesday, December 30, 2015

Makontena mtihani mzito kwa Magufuli

Wakati Watanzania wakiwa bado hawajasahau mtikisiko uliotokana na kashfa ya ukwepaji kodi wa makontena 2,431 katika Bandari ya Dar es Salaam iliyoibuliwa na Rais John Magufuli, katika kampeni yake ya kuinua mapato, taarifa nyingine ya kustusha imeanikwa jana baada ya kutolewa kwa ripoti inayoonyesha kuwa makontena mengine takriban 12,000 yalipitishwa bure bila kulipiwa tozo ya Bandari maarufu kama ‘wharfage’.
Upotevu huo wa makontena umeanzia Julai mwaka 2014 hadi Aprili mwaka huu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mabrawa, ndiye aliyefichua kashfa hiyo mpya kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuapishwa na Rais Magufuli kushika nafasi hiyo.
Katika taarifa yake hiyo, Prof. Mbarawa alisema uchunguzi uliofanywa na kamati maalum iliyoundwa kufuatilia upitishaji wa makontena na bidhaa nyingine bandarini bila kulipia tozo zinazostahili umebaini kuwa makontena 11,884 (takriban 12,000) yalipitishwa bandarini hapo bila kulipiwa ushuru wa bandari na pia kuna magari 2,019 yalipitishwa bure bila ya kulipiwa tozo hiyo kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Ilielezwa zaidi na Profesa Mbarawa kuwa jumla ya kiasi cha tozo ambacho hakikulipwa na wahusika wa makontena kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni takriban Sh. bilioni 47.42 huku tozo itokanayo na magari ikiwa ni Sh. bilioni 1.07.
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa, makontena hayo 11,884 ni mbali na yale 2,431 yaliyoibuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati alipofanya ziara ya ghafla kwenye bandari hiyo na kuzungumza na waandishi wa habari Desemba 7, 2015 kabla ya kuzitaja Bandari Kavu (ICD’s) zilizohusika na upotevu huo kuwa ni za Azam, DICD, JEFAG na PMM.
Akieleza zaidi, Prof. Mbarawa alisema kuwa baada ya kubainika kwa upotevu mkubwa wa makontena kufutia ziara ya Waziri Mkuu, watumishi 12 wa bandari walisimamishwa kazi na kufikishwa polisi ili wachukuliwe hatua zaidi za kisheria.
Aidha, alisema mawakala 55 wa forodha waliohusika walipewa notisi ya siku 7 ili walipe fedha walizokuwa wanadaiwa na baadhi yao walisitishwa kufanya biashara na TPA huku wengine wakikamatwa na kufikishwa polisi.
“Hadi tarehe 28 Desemba, 2015, jumla ya mawakala 15 walikuwa wamekamatwa na wote walilipa kiasi walichokuwa wanadaiwa ambapo jumla ya Sh. 820,473,830 zililipwa,” alisema Waziri Mbarawa na kuongeza:
“Kutokana na hatua hizo, jumla ya Sh. 900,690,096 zimelipwa hadi kufikia tarehe 28 Desemba, 2015. Zoezi la kuwakamata mawakala ambao bado hawajalipa linaendelea ambapo lengo ni hadi ifikapo tarehe 10 Januari, 2016, wote wawe wamekamatwa na kufikishwa Polisi ili walipe fedha zote wanazodaiwa.”

MAKONTENA 11,884
Akielezea kuhusu kubainika kwa makontena mengine 11,884 yasiyolipiwa ushuru wa bandari, Prof. Mbarawa alisema baada ya kubaini upotevu huo wa mapato katika ICD nne, TPA iliamua kufanyika kwa ukaguzi wa kina ufanyike katika bandari ICD zote ili kubaini kama kuna upotevu zaidi wa mapato ya ushuru wa bandari uliofanywa na mawakala wa forodha.
“Kutokana na ukaguzi huo, imebainika kuwa jumla ya makontena 11,884 na magari 2,019 yalitolewa bila malipo ya wharfage (ushuru wa bandari),” alisema Prof. Mbarawa.
Alizitaja ICD’s zinazodaiwa kukutwa na tuhuma hizo na idadi ya makontena kwenye mabano kuwa ni MOFED (61), DCID (491), JEFAG (1,450), Azam (295), PMM (779), AMI (4,338) na TRH makontena 4,424.
Kadhalika, alizitaja bandari kavu zinazohusika na upitishaji wa magari bila kulipia ushuru wa bandari na idadi ya magari kwenye mabano ni TALL (309), Chicasa (65), Farion (18), Silver (97), Mass (171) na Hesu magari 1,359.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Prof. Mbarawa alisema kufuatia ripoti hiyo iliyobainisha kuwapo kwa upotevu wa mapato ya ushuru wa bandari kwa makontena (11,884) na magari (2,019), tayari hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa watumishi 7 kati ya 15 wa TPA waliokuwa wanahusika na ukusanyaji wa mapato hayo.
“Hadi kufikia tarehe 29 Desemba, 2015, watumishi 7 kati ya 15 waliokuwa wanahusika na ukusanyaji wa mapato ya wharfage (ushuru wa bandari) katika ICD na CFS wamekamatwa na kufikishwa Polisi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa aliwataja watumishi waliokamatwa kuwa ni John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Benadeta Sangawe.
Kadhalika, watumishi wanaodaiwa kutoweka baada ya kusikia kuwa wanatafutwa ni Happygod Naftal, Nathan Edward, Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet Kimaina na Zainab Bwijo.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta mawakala hao ambao walifanikisha kuyatoa makontena hayo katika bandari kavu hizo ili hatua zichukuliwe.
Alisema serikali haitamvumilia mfanyakazi yeyote wa TPA awe mkubwa ama mdogo ambaye ataendelea kujihusisha na upotevu wa mapato bandarini.

TRA WACHUNGUZA ZAIDI
Akizungumzia tarifa za makontena hayo (11,884), Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Kayombo, alisema kujua kama makontena hayo pamoja na magari yamelipiwa ushuru ni mpaka wapatiwe orodha ya hayo makontena.
Alisema wakipatiwa orodha ndipo watakwenda kufanya uhakiki na kubaini kama yamelipiwa ushuru au la.

UMBALI DAR MPAKA CHALINZE
Uchunguzi zaidi wa Nipashe ulibaini kuwa makontena hayo 11, 884 yakipangwa kwa urefu kuanzia Dar es Salaam, yanaweza kufunika barabara yote hadi Chalinze mkoani Pwani, yakifunika bila shida maeneo mengine kadhaa ya mkoa wa Pwani kama Kibaha na Mlandizi.
Tathmini hiyo inatokana na makadirio kwamba nusu ya makontena hayo (yaani 5,942), ni yale makubwa zaidi yenye urefu wa futi 40 kila moja huku nusu nyingine (5,942) yakiwa ya urefu wa futi 20. Kwa hesabu hizo, yote kwa pamoja yanaweza kufunika urefu wa barabara wa jumla ya futi 356,520, sawa na Kilomita 108.67. Kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandao wa distancefrom, umbali wa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ni Kilomita 108.

BILIONI 48/- ZAWEZA KUFANYA NINI?
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa fedha hizo za ushuru wa bandari kiasi cha Sh. bilioni 48.49 si haba kwani zinaeweza kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa taifa.
Mathalani, vyanzo vinaeleza kuwa kipimo maarufu cha CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja. Hivyo, kwa Sh. bilioni 48.49, maana yake mashine takriban 48 za thamani ya Sh. bilioni moja zinaweza kununuliwa na kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na nyingine zikabaki.

Kadhalika, kwa mujibu wa Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, bei ya dawati moja linalochukua wanafunzi watatu wa shule za msingi kwenye jimbo lake ni Sh.100,000. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za ushuru wa bandari zilizokwepwa zitaelekezwa katika eneo hilo, maana yake yatanunuliwa madawati 484,900 na hivyo kupunguza tatizo hilo katika shule nyingi za msingi nchini.

Aidha, Kingu aliiambia Nipashe kuwa gharama za kuchimba kisima katika jimbo lake huwa haizidi Sh. milioni 15. Kwa sababu hiyo, kama fedha hizo za ‘wharfage’ zitaelekezwa kuchimba visima kwa gharama sawa na Singida Magharibi, maana yake vitapatikana visima 3,233.
Ikiwa visima vya kiwango hiki vitachimbwa kwa mgawanyo sawa katika wilaya 133 nchini, maana yake kila wilaya itapata mgawo wa visima 24.

Kadhalika, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi kukaririwa Aprili 20, 2015, akisema kuwa wao walikamilisha ujenzi wa maabara mojawapo shuleni kwao kwa Sh. milioni 58.2. Kwa sababu hiyo, kama makadirio ya fedha hizo za ‘wharfage’ kiasi cha Sh. bilioni 48.49 zitaelekezwa katika ujenzi wa maabara kama ya Sekondari ya Tandika, maana yake zitapatikana maabara takriban 833.

Akizungumza na Nipashe Septemba 16 mwaka huu, Mbunge mteule wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba, alisema kuwa katika jimbo lake, wamekamilisha ujenzi wa zahanati za vijiji kadhaa kwa wastani wa Sh. milioni 80 kwa kila moja. Kwa sababu hiyo, kama fedha za ‘wharfage’ zitatumika kujengea zahanati kama za jimbo la Bumbuli, taifa litapata zahanati mpya takriban 606.

Mwaka jana, Agosti 28, kulikuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milion 76. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha hizo za ‘wharfage’ zitatumika kununua gari la wagonjwa kama walilopata msaada Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, maana yake taifa litapata magari mapya ya wagonjwa takriban 638 na hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa magari hayo katika vituo vya afya na hospitali nyingi nchini.

Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka. Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.

Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha hizo za ‘wharfage’ (Sh. bilioni 48.49) zitatumika kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia 100, maana yake wanufaika watakuwa ni wanafunzi 11,492.
CHANZO: NIPASHE

No comments: