Monday, December 28, 2015

Mama alala kitandani miaka 15 bila msaada

Aisha Baraka akiwa amelala kwenye kitanda cha miti nyumbani kwake katika Kitongoji cha cha Mshikamano Wilaya ya Nachingwea mkoani Linidi. 
Kwa ufupi

Nachingwea. Makosa yaliyofanywa kwenye operesheni ya Aisha Baraka, mkazi wa kitongoji cha Mshikamano wilayani Nachingwea, yamesababisha alale kitandani kwa miaka 15 sasa bila ya msaada.

Mama huyo, ambaye analala kwenye kitanda cha kamba kisichokuwa na godoro akiwa na mpira anaoutumia kwa haja ndogo, alifanyiwa upasuaji huo na madaktari anaohisi walikuwa wanafunzi kwenye Hospitali ya Nachingwea kwa lengo la kutatua tatizo lake la kutopata choo.

“Walinitibu kimakosa,” anasema mama huyo alipoongea na Mwananchi. “Nilikuwa na tatizo la kupata choo nikaenda hospitali ili nipewe vidonge, lakini nilikuta kuna wanafunzi wazungu waliokuja ndiyo wakanifanyia upasuaji kwenye kizazi.

“Nilidhani ningepata choo baada ya mzungu kunikatakata, lakini kuanzia hapo mpaka leo haja ndogo inanitoka tu.”

Aisha sasa anaomba msaada ili tatizo lake liweze kurekebishwa na kurudia hali yake ya kawaida.

Akizungumzia hali hiyo, mtoto wa pili wa mama huyo, Johnston Solomon alisema anajitahidi kumhudumia mama yake lakini amekuwa akishindwa kutokana na kukosa msaada kutoka kwa ndugu ambao anadai wamewatenga.

Alisema tatizo hilo lilisababishwa na upasuaji wa daktari mwanafunzi kutoka Ulaya ambaye anadhani hakuwa na utaalamu wa kutosha.

Akizungumzia hali hiyo mwenyekiti wa Kijiji cha Mshikamano, Zena Jacob alisema baada ya kupatiwa taarifa za bibi huyo alilifuatilia na kwenda naye Hospitali ya Wilaya ambako aliwekewa mpira ya kumsaidia kutoa haja ndogo na kutakiwa kwenda Hopitali ya Mkoa wa Lindi kwa matibabu zaidi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Sonda Shaban alisema ni vigumu kulizungumzia suala hilo kwani miaka 15 ni mingi hivyo wanahitaji kuthibitisha madai ya Aisha kupitia nyaraka zake za wakati anapatiwa matibabu.

“Mpaka nithibitishie kupitia nyaraka zake wakati anapatiwa matibabu. Pia ni muhimu kuchukua maelezo ya bibi kwa ajili ya uchambuzi wa kidaktari, lakini makosa katika udaktari hutokea. Kwa hiyo yanaweza kutokea ama yasitokee,” alisema Dk Shaban.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Nachingwea, Fundi Mohamed alisema Aisha amekuwa akipatiwa huduma kama matibabu bure, lakini suala la rufaa yake kwenda Hospitali ya Mkoa limekosa mrejesho kwa wahusika.

Alisema wilaya hiyo ina vijiji 127, na kati ya yake vijiji 40 vyenye wazee wapatao 7,116 wenye zaidi ya miaka 60 wanahitaji huduma ya matibabu kutoka halmashauri ambayo hugharamiwa na mkurugenzi kwa kuwalipia gharama za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ili waweze kupata matibabu bure.
MWANANCHI

No comments: