ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 23, 2015

Naibu Waziri Mpina kutatua Changamoto NEMC

Na Victor Mariki - Ofisi ya Makamu wa Rais

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu Rais - Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Luhaga Mpina (pichani)  amefanya ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kwake wadhifa wa unaibu waziri kwa kutembelea Makao Makuu ya Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Katika ziara hiyo ya kujitambulisha pamoja na kukagua utendaji wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mheshimiwa Mpina alibaini baadhi ya changamoto zinazolikabili Baraza hilo katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa pamoja na kuzipatia utatuzi changamoto hizo.

Aliongeza kwa kuainisha changamoto hizo kuwa ni; uchelewaji wa utoaji vyeti vya Tathimini ya Athari kwa Mazingira kwa wateja, utozaji tozo usioendana na wakati, uchache wa kanda na uchache wa rasimali watu katika utekelezaji wa majukumu.

Aidha katika kutatua changamoto hizo Mheshimiwa Mpina alilitaka Baraza hilo kuwasilisha viwango vya utozaji tozo vilivyowekwa kulingana na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 katika Ofisi ya Waziri ili viweze kujadiliwa pamoja na wadau na kufanyiwa maboresho kulingana na wakati huu.

Pia alilitaka Baraza hilo kutoa vyeti vya Tathimini ya Athari kwa Mazingira kwa wateja wake ndani ya siku 60 kulingana na Sheria hiyo ya Mazingira ya Mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kuviwasilisha vyeti hivyo katika Ofisi ya Waziri ili viweze kutolewa na Ofisi ya Waziri ndani ya siku 30.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Mpina alitoa agizo la siku 30 tu kwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukamilisha utoaji wa vyeti 512 vilivyocheleweshwa utolewaji wake na Baraza hilo kulingana na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.


No comments: