ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 13, 2015

TRA kumwagia wafanyabiashara EFDs bure

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikitangaza kuanza kuwasaka wafanyabiashara waliokwepa kodi na ambao wameshindwa kulipa ndani ya siku saba kama walivyoagizwa na Rais John Magufuli, itagawa bure mashine 200,000 za EFDs kwa kuanzia, ikiwa ni jitihada za mamlaka hiyo kuongeza mapato ya serikali.

Hatua hiyo ya TRA ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alilolitoa kwenye mkutano wake na wafanyabiashara Ikulu mwezi huu, ambapo aliitaka mamlaka hiyo kuangalia uwezekano wa kuwapatia mashine hizo bure.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Magufuli pia alitangaza msamaha kuanzia Desemba 4 hadi 11, kwamba mfanyabiashara aliyekwepa kodi ambaye atakwenda kulipa kwa hiyari yake TRA, hatachukuliwa hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Phillip Mpango alisema wafanyabiashara hao pamoja na mmiliki wa bandari Kavu ya Azam ICD, waliamriwa kulipa deni la makontena ambayo yalipita kwenye bandari kavu yao bila kulipiwa ushuru.

Alifafanua kwamba mmiliki wa ICD ya Azam anakumbushwa kwa mara ya mwisho kulipa kodi yote inayodaiwa kwa mujibu wa nafasi yake kama mwenye dhamana.

Alisema hadi jana, Sh. bilioni 10.6 zilikua zimelipwa na kampuni za waagizaji binafsi 28 kufuatia agizo lililotolewa na Dk. Magufuli.

Mpango alisema ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi ya makontena yaliyoondoshwa bandarini kinyume cha sheria na taratibu za forodha, TRA imefungua akaunti maalum katika benki ya NBC ijulikanayo kama ‘Commissioner for Customs and Excise-Container Account’, namba 9921169765.

Aliwakumbusha watumishi wote wa TRA, kuwasilisha taarifa zao kuhusu mali wanazomiliki pamoja na fedha walizonazo benki hadi siku ya Jumanne wiki ijayo, Desemba 15 mwaka huu.

Aidha, alisema watumishi zaidi ya 36 wa TRA, wanaotuhumiwa kuhusika na upotevu wa makontena 329 na kuondoshwa bandarini kinyume na taratibu watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mpango, alisema wameshapokea baadhi ya taarifa za watumishi wa TRA zisizopungua 15 kutoka kwa wananchi kuhusu mali za kifisadi na mwenendo mbaya wa walipa kodi na alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa hizo.

“Nataka niwatie moyo watumishi ambao ni waadilifu ndani ya TRA, kuendelea kukusanya mapato kwa bidii zaidi ili kufikia malengo ya ukusanyaji mapato kwa asilimia 100 na kuliinua taifa letu,” alisema Mpango.

Alisema wafanyabiashara ambao mpaka sasa hawajalipa kodi ni 15 na kiasi wanachodaiwa ni Sh. bilioni 3.7, wakati wafanyabiashara 13 wamelipa fedha zote walizokuwa wanadaiwa kiasi cha Sh. bilioni 4.1.
Aidha, alisema wafanyabiashara 15 wamelipa sehemu ya deni la Sh. bilioni 2.3 kati ya Sh. bilioni 16.4 wanazodaiwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: