
NA FRIDAY SIMBAYA, IRINGA
Ufaulu wa wanafunzi
waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2015
mkoani Iringa umeongezeka ukilinganisha na mwaka jana, ambapo ufaulu
kwa mwaka huu ni asilimia 73.25, wakati mwaka jana ulikuwa ni asilimia
68.58, sawa na ongezeko la asimilia 4.67.
Hayo yalisemwa na Afisa Elimu Taaluma
wa Mkoa wa Iringa, Euzebio Mtavangu hivi karibuni wakati akitoa
taarifa ya mwelekeo wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi
2015 kwa wajumbe wa kamati ya uchaguzi wa mkoa wa kuchagua wanafunzi
wataojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016.
Alisema kuwa kuongezeka kwa ufaulu
mwaka huu mkoani Iringa ni kutokana na utekelezaji mzuri wa mpango wa
matokeo makubwa sasa (BRN) ulioanzisha na serikali hivi
karibuni.
Alisema kuwa wanafunzi waliofaulu
mwaka 2015 ni 15,311 (7,163 wavulana na 8,148 wasichana) ambapo
wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu wamechaguliwa kujiunga na kidato
cha kwanza mwaka 2016.
Katika mwaka 2014 matokeo ya
watahiniwa waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi walikuwa ni
wanafunzi 14,650 (6,835 wavulana na 7,815 wasichana).
Mtavangu aliongeza kuwa kwa mwaka 2015
wanafunzi 413 (258 wavulana na 155 wasichana) ambao ni asilimia mbili
hawakufanya mtihani wakilinganishwa na 177 (109 wavulana na 68
wasichana) ikiwa ni asilimia moja kwa mwaka 2014.
Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi
ulifanyika tarehe 09-10 Septemba 2015 nchini kote.
Aidha, alisema kuwa shule za msingi
467 kati ya shule 491 ndio zilizokuwa na watahiniwa wa mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2015 mkoani Iringa.
Mtavangu alisema kuwa watahiniwa
waliofanya mtihani na kumaliza elimu ya msingi 2015 wanaendelea kujibu
maswali ya mitihani kwa kutumia fomu za ‘Optical Mark Reader’
(OMR).
Alisema kuwa matumizi ya fomu za OMR
yalianza mwaka 2012 na lengo la kutumia OMR ni kusoma moja kwa moja
kwa kompyuta majibu ya mtahiniwa kutoka katika karatasi yake ya majibu
na kuokoa muda wa usahihishaji.
Takwimu za watahiniwa waliofanya
mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015 ni wanafunzi 20,905
(9,612 wavulana na 11,293 wasichana) na waliofaulu ni jumla ya
wanafunzi 15,311 (7163 wavulana na 8148 wasichana), sawa na asilimia
73.25.
Hata hivyo, kiwango cha kumaliza elimu
ya msingi (completion rate) mkoani Iringa kimeongezeka kutoka asilimia
77.2 (2014) hadi kufikia asilimia 81.1 (2015).
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa
Mkoa ya kuchagua wanafunzi wataojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016
alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa (RAS), Ayubu
Wamoja.
No comments:
Post a Comment