Tuesday, December 8, 2015

Warioba: Mabadiliko bila maadili kwenye Katiba Mpya kazi bure

“Tangu mwaka 1996 hadi leo rushwa bado ni
By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema nchi haiwezi kuwa na mabadiliko ya kweli, kama miiko na maadili ya viongozi havitaingizwa kwenye Katiba Mpya.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo ya maisha ya utumishi wa umma uliotukuka juzi, Warioba alisema kwa miaka mingi akishirikiana na rafiki zake, walijaribu kuleta mabadiliko makubwa katika jamii, bila mafanikio.

“Huwezi kuwa na mabadiliko kama huna miiko na maadili kwenye Katiba, lazima kuwe na separation of power (kutenganishwa kwa madaraka), naamini kanuni hizi zitaingia kwenye Katiba Mpya,” alisema.

Mara kadhaa Jaji Warioba amekuwa akisisitiza umuhimu wa vipengele hivyo viwili kuingizwa kwenye Katiba Mpya. Katika rasimu ya pili ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliyokuwa akiiongoza ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi kama tunu za Taifa, lakini Bunge Maalumu la Katiba liliyaondoa na kuyaweka katika msingi wa utawala bora.

Jaji Warioba amekuwa akihoji kuwa uzalendo na uadilifu si mpaka mtu awe kiongozi na kwamba mambo hayo mawili si misingi ya utawala bora ni ya kitaifa na inamhusu kila Mtanzania.

Azungumzia tuzo

Akiizungumzia tuzo hiyo aliyopewa na Umoja wa Maofisa Watendaji wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt), Warioba alisema anaamini alipewa heshima hiyo, kutokana na mchango wake alioutoa kwenye sekta binafsi alipokuwa Waziri Mkuu wakati wa Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Alisema kutokana mabadiliko ya mfumo wa maisha duniani wakati huo, Tanzania ilijikuta imeingia kwenye soko la uchumi bila kujiandaa, ndipo alipoomba msaada wa kitaalamu kutoka sekta binafsi.

“Nikiwa Waziri Mkuu nikasema sekta binafsi wasaidie, nikaunda tume walikuwapo pia wasomi, mchango wao ulikuwa mkubwa sana,” alisema.

Kuhusu rushwa


Pia, alizungumzia ushiriki wake katika tume ya kuchunguza mianya ya rushwa aliyokuwa mwenyekiti wake. Alisema ilifanya kazi kubwa ya kupambana na rushwa, lakini haikufanikiwa kiasi cha kutosha kwa kuwa bado vitendo hivyo vinaendelea mpaka sasa.


“Tangu mwaka 1996 hadi leo rushwa bado ni tatizo, tulisema kila kitu kiwe wazi, lakini bado sijaona uwazi na uwajibikaji. Tulisema rais amtake kila kiongozi baada ya miezi sita aonyeshe alivyofanya kupambana na rushwa kwa uwazi,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa CEOrt, Ali Mufuruki, alisema takribani miaka 20 iliyopita Warioba aliweka msingi wa namna ya kupambana na rushwa ambao mpaka sasa bado unaendelea kutumika.

“Pia amefanya hivyo katika mchakato wa kupata Katiba Mpya,” alisema.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva na Katibu Mkuu mstaafu wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim.

1 comment:

Anonymous said...

Unazungumza nini Babu Warioba.Katiba gani Mpya uliyonayo Kichwani. wee mzee ni msaliti,mwongo na mnafiki.siioni mantiki yeyote kwa maoni yako ambayo ni very disturbing na ulipaswa uyahifadhi kwenye ubongo wako uliojaa ukigeugeu.wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa tanzania 2015 uliofanyika octoba 25,CCM walikuvalisha Magwanda ya Kijani[ambayo ulikua hujayavaa kwa miaka 20 na zaidi]wakakupandisha majukwaani na kule ukaikana ile rasimu ya katiba mpya,kazi iliyoligharimu taifa mabillion,kama hamkutumia trillon moja.ilikua wewe na ccm ccm na wewe,wewe na mwanao mgombea wa jimbo la Kawe Kippi warioba.Majukwaani, kwa mbwembwe Mnaichana chana Katiba mpya.Ghafla umegeuka Kippi kaanguka,umerejesha magwanda,tukuone kama sio wewe.this is ridiculous,mwongo mkubwa.lakini nikupe angalizo.mimi namfahamu mheshimiwa jpMagufuli rais wetu.usije ukalogwa ukamsogelea kwa hilo.yule ni philosopher akiiona midomo yako inacheza cheza KWA KUTANGULIZA UNAFIKI,ATAKUFUKUZA,ATAKUPA UKWELI KUHUSU WEWE,MWENZIO HAANGALII UWE CCM,UWE UKAWA AU UWE RAIA USIYE NA CHAMA.yaani warioba ni kidudu mtu,ni kero.