Saturday, January 9, 2016

Bomoabomoa wakati wowote Morogoro

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
By Lilian Lucas,Mwananchi
Morogoro. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amewataka wananchi waliojenga maeneo yasiyo rasmi na wasio na vibali maalumu kuondoka kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Kadhalika waziri huyo amesema ni vyema wakazi hao wakaanza kuondoka mapema ili kuondokana na lawama zinazoweza kujitokeza pindi bomoabomoa itakapoanza wakati wowote mkoani Morogoro.

Mabula alitoa kauli hiyo akiwa katika ziara ya kukagua shughuli zinazoendeshwa na wizara hiyo mjini hapa.

Alisema Serikali inahitaji kuona wananchi wanaishi katika maeneo salama na uamuzi wa kuwataka kuondoka mapema katika maeneo hayo unalenga kuwaepusha na majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mabula alisema bomoabomoa kama iliyofanyika Dares Salaam ni ya nchi nzima, hivyo kila halmashauri ijiandae kutambua maeneo ambayo siyo rasmi kwa makazi na kutoa taarifa kwa wananchi kuondoka sehemu hizo.

Pia, aliwataka watumishi wa halmashauri ambao wanatoa vibali vya ujenzi katika maeneo yasiyo rasmi kwa ajili ya ujenzi wa makazi kuacha mara moja, kwani wamekuwa chanzo cha migogoro baina ya Serikali na wananchi.

“Watumishi wa Idara ya Ardhi katika halmashauri zote nchini wahakikishe wanafanya ukaguzi na kubaini maeneo ambayo yamejengwa kimakosa na kuwataarifu wananchi mapema ili kutosababisha migongano,” alisema Mabula.

Wakizungumzia suala la bomoabomoa wakazi wa Morogoro, Idris Salehe na Idd Masoud waliitaka Serikali kuwachukulia hatua maofisa wake waliogawa maeneo ya ardhi katika mabonde na jirani na mito kwa kuwa walichangia kuwapotosha wananchi.

“Kuwabomolea wananchi nyumba kuende sambamba na kuchukua hatua kwa waliowasababishia hasara hiyo. Serikali isipofanya hivyo utakuwa ni uonevu maana nao walichangia, ” alisema Salehe.

Naibu waziri huyo yupo mjini Morogoro na baada ya kuitembelea halmashauri hiyo, atakuwa na ziara ya kutembelea Wilaya ya Mvomero.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake