Dar es Salaam. Ni miaka 42 imepita tangu Tanzania ing’are katika medani ya soka Afrika.
Nyota hiyo iliyoanzia kwa mshambuliaji Maulid Dilunga na kipa Omari Mahadhi, iling’ara pia juzi kwa Mbwana Samatta aliyeteuliwa katika kikosi bora cha mwaka Afrika.
Samatta aliungana kikosini na kipa Robert Kidiaba (DR Kongo), mabeki; Serge Aurier (Cote d’Ivoire), Aymen Abdennour (Tunisia), Mohamed Meftah (Algeria), viungo; Andre Ayew (Ghana), Yaya Toure (Cote d’Ivoire), Sadio Mane (Senegal), Yacine Brahim (Algeria) na washambuliaji; Pierre-Emerrick Aubameyang (Gabon) na Baghdad Bounedjah (Algeria).
Samatta, amebebwa na mafanikio makubwa katika soka akiwa na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), yakiwamo ya kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao saba.
Hayo ni mafanikio makubwa yanayorejesha kumbukumbu za kina Dilunga na Mahadhi (wote sasa ni marehemu), walioteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuunda kikosi cha nyota Afrika, Africa All Stars, mwaka 1973.
Tofauti na Samatta aliyeibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora Afrika mwaka 2015 kwa wanaocheza soka ndani Afrika akiwa na TP Mazembe, Klabu Bingwa ya Afrika, Dilunga na Mahadhi walitokea Yanga na Simba na kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki michezo ya Afrika mwaka 1973 mjini Lagos, Nigeria.
Taifa Stars , wakati ule ilicheza nusu fainali baada ya kufanya vyema kwenye michezo ya awali kwa kuibana Super Eagles au Nigeria A na kutoka 0-0, ikaichapa Nigeria B kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Dilunga.
Pia, timu hiyo ilizifunga timu zinazotamba leo Afrika, Ghana na Togo, bao 1-0 kila moja na baada ya mashindano hayo, CAF iliwateua wachezaji hao kuiwakilisha Afrika, ambako walizuru Hungary, Bulgaria barani Ulaya pia kutembelea Mexico, Guatemala, Uruguay, Peru. Rekodi zinaonyesha kuwa kikosi hicho cha kina Dilunga, Mahadhi kilishinda mechi tatu, sare mbili na kufungwa mechi moja.
Hata hivyo, uteuzi wa Dilunga kwenye kikosi hicho ulizua utata baada ya kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT, sasa TFF), kudhani mchezaji aliyeteuliwa alikuwa Abdallah Kibaden.
Majibu ya CAF kwa FAT, yalieleza kuwa shirikisho hilo lilimhitaji mchezaji aliyekuwa akivaa jezi namba 10 Stars, ambayo wakati ule ilivaliwa nao, Dilunga na Kibaden.
FAT ililazimika kuomba ufafanuzi CAF na ndipo ilipobainika kwamba, mchezaji aliyehitajika ni Dilunga na siyo Kibaden.
Sababu za CAF kumteua Dilunga ni uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao, aliouonyesha kwenye mechi dhidi ya Nigeria B, ambako alipachika wavuni mabao mawili akitokea benchi.
Dilunga, aliyetokea Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro kabla ya kutua Yanga mwaka 1966, pia aliwahi kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa England mwaka 1970 kwenye timu iliyokuwa Daraja la Pili , West Bromwich, ambayo kwa sasa ipo Ligi Kuu.
Timu ilizuru Tanzania kucheza na Yanga na hadi leo kuna madai kuwa aliyekuwa mwenyekiti wa FAT, Said Hamad El-Maamry alimzuia Dilunga kwenda Ulaya ili aichezee Taifa Stars michezo ya kimataifa.
Alipoulizwa jana kuhusu mzozo huo wa Dilunga na Kibaden, El- Maamry alijibu kuwa hawezi kulizungumzia, badala yake waulizwe viongozi wa FA ndio wasimamizi wa soka nchini.
Wadau wamzungumzia Samatta
Kiongozi wa klabu ya African Lyon, zamani Mbagala Market iliyomwibua Samatta kabla ya kusajiliwa Simba, Rahim Zamunda alipongeza mafanikio ya mshambuliaji huyo, huku akitoa wito kwa wadau wa soka wenye uwezo kuwasaidia wanasoka chipukizi nchini ili wapige hatua.
Mbunge wa Jimbo la Malindi, Zanzibar, Ally Saleh aliyekuwa pia wakala wa wachezaji aliyeidhinishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), alimpongeza Samatta na kumshauri baadhi ya mambo anayoamini yatamsaidia kufanikiwa zaidi katika soka.
Mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Said El- Maamry alisema kuwa ushindi wa Samatta utatoa mwanga mpya wa soka kwa vijana wanaochipukia akiwa kama chachu ya mafanikio kwa wengine watakaokuwa na ndoto kama zake.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake