Dar es Salaam. Siku 74 baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kimefanya kikao cha kujitathmini na kuweka mpango kazi kwa miaka mitano ijayo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa alishindwa na Rais John Magufuli wa CCM aliyepata kura Milioni 8.8 sawa na asilimia 58.5.
Lowassa alipata kura Milioni 6 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Chadema pia ilipata wabunge 70, wakiwamo 36 wa viti maalumu huku CCM ikipata wabunge 188. Katika chaguzi ndogo saba zilizofanyika baada ya uchaguzi huo mkuu, CCM iliongeza wabunge takribani tisa, wakiwamo wa viti maalumu watatu na Chadema mbunge mmoja wa kuchaguliwa.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho jana, ilieleza kuwa itajadili vipaumbele vyake vya mwaka 2016-2020 na kuwasilisha katika kikao cha kikatiba na uamuzi kwa ajili ya utekelezaji.
“Lengo ni kukiimarisha chama na kuiondoa CCM madarakani ili kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kweli kuliko haya yanayofanyika sasa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika mkoani Kilimanjaro zinaeleza kuwa moja ya ajenda ilikuwa ni kubadilishwa kwa idara za chama hicho kwa ajili ya kujipanga kwa ajili ya mkutano ujao wa Bunge.
“Pia, watajadili tamko la Waziri Mkuu, Kassim (Majaliwa) la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa,” ilieleza taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake