Thursday, January 7, 2016

Fatma Karume amshauri Dk Shein akae pembeni

Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume

By Florence Majani, Mwananchi

Dar es Salaam: Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume amemshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein kuachia madaraka.

“Dk Shein lazima aondoke kwa sababu kuendelea kubaki madarakani ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi,” alisema Fatma ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Fatma alisema kuwa mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria kufanya hivyo.


Fatma alisema Jecha hana mamlaka kikatiba na kisheria kufuta matokeo hayo kwa kuwa maamuzi kama hayo yanatakiwa kufanywa na ZEC yenye mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watano; watatu kutoka CCM na wengine wawili kutoka CUF.

“Akidi ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na wajumbe wanne. Kama kikao kilifanyika, akidi ilitimia na jambo hilo likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi walipokubali wajumbe wengine. Hata makamu mwenyekiti hajashiriki kwenye maamuzi hayo kwa sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila kupata akidi hiyo,” alifafanua Fatma.

Mwanasheria huyo alisema kuwa amekuwa akiwasikia baadhi ya wana CCM Zanzibar wakisema kuwa Jecha ndiyo tume na tume ndiyo Jecha, hivyo ana haki ya kufuta uchaguzi. Lakini Fatma alisema Jecha hana mamlaka kusema jambo ambalo halijakubaliwa na tume.

Alipoulizwa ikiwa hatua ya aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, Seif Sharrif Hamad ya kutangaza matokeo aliyodai yalimpa ushindi si kosa, Fatma alisema, “Sikumuona Maalim Seif alipokuwa anatangaza matokeo hayo hivyo sijui kama alijitangaza kuwa mshindi au alitangaza matokeo kama yalivyobandikwa kwenye vituo.

“Katika nchi zilizokomaa kidemokrasia mgombea anaweza kuona mwelekeo wa matokeo na akampigia mwenzake kumpongeza. Nadhani Maalim Seif alisoma jumla ya matokeo ya uchaguzi kama yalivyobandikwa kwenye vituo, hivyo hilo si kosa ati,” alisema na kuongeza: “Ninasikitishwa na tabia hii. Sikutegemea kama CCM watatumia nguvu kutaka kubaki madarakani kwa njia hii. Sikutegemea kama watavuruga katiba…ndiyo maana nina huzuni.”

Jambo jingine alilosema litazua mgogoro Zanzibar ni mamlaka yenye haki ya kuidhinisha fedha za uchaguzi wa marudio ikiwa watalazimisha ufanyike.

“Kisheria fedha hizo ni lazima zikubaliwe na Baraza la Wawakilishi. Baraza lipo wapi? Ili mtu awe waziri lazima awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Rais alivunja Baraza Agosti na kwa hiyo hadi ilipofika siku ya kuapishwa rais mpya, Zanzibar hakuna Baraza wala Waziri. Ina maana fedha za wananchi zinatumiwa bila idhini ya Baraza, ” alisema.

Alisema kinachofanyika Zanzibar ni ‘ukoloni’ wa watu weusi dhidi ya watu weusi ambao unawakosesha Wazanzibari haki yao msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Hali si shwari Zanzibar. Watu wamekata tamaa kwa sababu unapokuwa na Serikali ambayo inanyang’anya haki ya wananchi ya kupiga kura, kuandamana, watu wanakosa imani na Serikali hiyo,” alisema.

Kurudia uchaguzi

Kuhusu kurudiwa uchaguzi nchi nzima, Fatma alisema ulipofanyika uchaguzi mwaka 2000 ambao Amani Karume aligombea kwa mara ya kwanza, zilitokea dosari katika majimbo 10 ya Unguja. CUF walipotaka uchaguzi urudiwe nchi nzima, CCM chini ya Benjamin Mkapa waligoma wakasema ni katika majimbo yenye dosari tu.

“Nini kimetokea mwaka huu? Kama dosari zilijitokeza Pemba kama wanavyodai kwa nini urudiwe Unguja? Kwa nini hawataki kutumia uamuzi wa mwaka 2000 wa kurudia maeneo yenye dosari tu?” alihoji.

“Mkapa alisema wazi kwenye kipindi cha Hard Talk cha BBC akihojiwa na mtangazaji Tim Sebastian uchaguzi hauwezi kufutwa ila utarudiwa tu katika baadhi ya majimbo. Kwa nini leo mambo yamebadilika na CCM inataka uchaguzi mpya?” alihoji.

Fatma ambaye alikataa kueleza msimamo wake kisiasa, alisema iwapo uchaguzi huru na wa haki utafanyika leo Zanzibar, CCM haiwezi kushinda kwa sababu Wazanzibari wanajionea yale ambayo wanafanyiwa na chama hicho.

“CCM imeshindwa Zanzibar kwa sababu ilishindwa kuwashawishi watu wake na badala inawakemea, ikawanyima haki zao. Kisaikolojia wapiga kura wanataka haki zao na wasibaguliwe lakini ukiwapelekea jeshi na vifaru, unazidi kuwapoteza,” alisema.

Sherehe za Mapinduzi

Wakati zikiwa zimesalia siku nne kufikia kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma alisema kwa hali ilivyo haina maana kutokana na CCM kung’ang’ania kukaa madarakani kwa nguvu.

“Ninajisikia kusalitiwa. Madhumuni ya Mapinduzi haikuwa kuiweka CCM madarakani milele bali kurejesha madaraka kwa wananchi,” alisema.

Alisema aliambiwa kuwa waliofanya mapinduzi (wakiongozwa na Abeid Amani Karume) walitabiri kuwa ipo siku Zanzibar itakuwa na uchaguzi au Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini CCM hawataki.

“Wakati hao waliofanya mapinduzi wakisema hivyo, CCM haikuwepo, ilikuwepo ASP. Hao ASP hawakuwa wakijiaminisha kuwa watakaa madarakani milele,” alisema.

“Wakati tunaadhimisha mapinduzi ya Zanzibar, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa malengo ya mapinduzi hayo yalikuwa ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote na kuweka misingi ya kidemokrasia lakini CCM wamevuruga,” alisema Fatma.  

3 comments:

Anonymous said...

Licha ya yote yaliotokea kuhusu uchaguzi wa Zanzibar. Mansouri Yusufu Humidi ambae kwa wanzanzibar wanamuelewa kuwa miongoni mwa watu waliosisi kundi la mwamsho na vile vile Missouri ni moja ya kiongozi mwandamizi wa CUF. Mansouri ni kaka wa damu wa mama wa Fatma Karume anaemshauri dk sheni akae pembeni. Serikali sheni ilishamuweka ndani au kizuizini Mansouri pale Zanzibar kutokana na vurugu zake za kisiasa vile vile akihusishwa na kundi la mwamsho. Inasemekana kama Mansouri asingekuwa shemegi wa Amani karume basi angeliozea jela kwani alituhumiwa kukutwa na sila ya moto kinyume cha sheria. Vile vile familia ya karume akijumuuishwa shemegi yake Mansouri ambae aliwahi kuwa waziri wake katika serikali ya mapinduzi Zanzibar inatuhumiwa kujibinafsishia mali nyengi za umma hasa maeneo ya wazi ya serikali yaliotengwa kwa matumizi ya umma. Hii ni kwa kifupi tu jinsi gani suala za Zanzibar lilivyokuwa very complicated. Mfano ilipoundwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, ilibidi iitishwe kura ya maoni wanzanzibar waamuwe. Kura ikapigwa unguja na pemba matokeo yake waunguja wakapiga kura ya hapana kukataa uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa lakini matokeo yake waunguja wakapuuzwa bila ya kuulizwa kwanini wanapinga na serikali ya kitaifa ikaundwa.
Sisa za Zanzibar ni CUF kuimiliki pemba na CCM unguja licha ya CUF kupata baadhi ya viti unguja na hii inatokana na kuwa unguja ni capital city of Zanzibar kwa vyovote vile itakuwa imebeba karibu wakazi wake wa maeneo mbali mbali ya nchi wengi wao kutoka pemba.
Kuundwa kwa serikali ya kitaifa CUF pembeni wakaunda kundi lenye msimo mkali wa kidini pamoja na kisisa ili kuwavuga wanzanzibar na kuwa na msimamo ghasi kuhusu muungano,CCM na watu wa bara, CUF ilikuwa inaendesha kampeni ya (divide and rule) miongoni mwa wanzanzibar kwa kutumia udini kupitia kundi la mwamsho. Mambo ni mengi sana yanayosababisha wingu jeusi kutanda Zanzibar lakini la msingi busara kubwa inatakiwa itumike Zanzibar kuepusha kisichotarajiwa kutokea kwani visiwa hivyo vinaweza vikajikuta vinagawanyika hao akina karume wasiangalie kupata tu bali waangalie hatima ya wanzanzibar wote kwani kama muaisi mzee wao mzee Abeid Karume kama angefufuka leo na kukutana na utumbo wa familia yake unaofanywa pale Zanzibar basi angeikana kuwa sio familia yake alioacha.

Anonymous said...

Zanzibar kuna viongozi wa kijeshi kwa sasa hawa heshimu maamuzi ya wananchi walio piga kura kwa amani na kumchagua rais wanae mtaka CCM wameamua kuitawala zanzibar kwa nguvu za dola,damu ikimwagika hakuna atakae salimika kuanzia Magufuli.Mwamunyange mpaka sheni wote watakuwa watuhumiwa hili lieleweke.
Hongera bi Fatma Karume kwa ushauri wako watakukumbuka watakapo kuwa safarini kuelekea "The Hague" kuungana na kina charles Taylor,Gbagbo etc.

mdau.

UK.

Anonymous said...

MDAU WA KWANZA MIMI SITAKUWA NA MUDA WA KUTOA MAELEZO NA DARASA, ILA MAELEZO YAKO KIDOGO YANAHITAJI UFAHAMU SIO USHABIKI, KAFANYE UTAFITI UAMSHO VIPI ULIANIA NA ULIANZISHWA VIPI, WAKATI UAMSHO UNANZISHWA HAWA MANSOUR WALIKUWA WAPI KWA WAKATI HUO NA WAKIFANYA NINI, UNAPOTOA TAARIFA UWE NA UHAKIKA SIO UNAKURUPUKA, UNAIPOTOSHA JAMII