Mchapalo wa Maadhimisho ya Miaka 70 ya mkutano wa Kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulifanyika Januari 10,1946 katika Ukumbi wa Westminster, London Uingereza . Pichani anaonekana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akimpatia kipande cha keki, Sir Brian Urquhart aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi akishughulikia masuala ya Siasa na mmoja wa watumishi wa kwanza wa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Maadhimisho hayo yamefanyika siku ya jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jana jumatatu limeadhimisha miaka 70 tangu mkutano wa kwanza wa Baraza hilo ulipofanyika January 10, 1946 huko Westminister, London, Uingereza.
Pamoja na kuzungumzia mafanikio na changamoto mbalimbali ambazo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepita, moja ya jambo ambalo limebainika wazi ni uwiano mdogo wa idadi ya mabalozi wanawake na wanaume wanaoziwakolisha nchi zao katika ngazi ya Wawakili wa Kudumu.
Akizungumzia tofauti hiyo, Rais wa Baraza Kuu la 70, Bw. Mogens Lykketoft, ambaye naye ametimiza miaka 70 ya kuzaliwa kwake Januari 10, amesema
“ Cha kuvutia, lakini na ambacho si cha kushangaza, siku ulipofanyika mkutano wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hapakuwa na Mwakilishi wa Kudumu mwanamke. Hali hii inaendelea hadi sasa ambapo idadi ya wawakilishi wa wanawake haizidi asilimia 18”.
Wakati huo mwaka 1946 nchi wanachama walioshiriki mkutano huo wa kwanza wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilikuwa 51. Miaka 70 baadaye Umoja wa Mataifa una nchi wanachama 193.
“Mkutano ule wa kwanza ulikuwa na mambo mengi ya kuvutia, kwanza ulidumu kwa saa moja, na ndani ya muda huo, palipitishwa uamuzi mmoja tu nao ulikuwa ni wa kumchagua Rais wa Baraza hilo” amesimulia Bw. Lykketoft
Na kuongeza “ Hata hivyo uamuzi huo ulibidi upigiwe kura. Bw. Tyrgve Halvdan Lie wa Norway, alipoteza kura kwa Bw. Paul Henri Spaak wa Ubeligiji. Hata hivyo Bw. Lie hakuhitaji kuwa na hofu sana kwani wiki tatu baadaye alikuja kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Rais wa Baraza Kuu la 70 ameeleza kwamba hapana shaka mkutano ule wa kwanza uliofanyika mwaka 1946 uliweka msingi wa mambo mengi na ulikuwa mwanzo wa hatua muhimu wa kile kinachojulikana hivi sasa kama Jumuiya ya Kimataifa.
Akabainisha pia kuwa, baada ya dunia kupitia misukosuko na matukio ya kutisha kama vile vita kuu za dunia, uharibifu mkubwa, mauaji ya kimbali, ulipuaji wa mabomu ya nyukilia, mataifa ya dunia yaliamua kwa makusudi kuwa kitu kimoja na kuchagua njia sahihi ya kuifanya dunia iwe ya amani, usalama, haki, haki za binadamu na maendeleo ya kijamii.
“ Na katika Baraza Kuu, waliunda chombo cha kweli, chombo ambacho kila taifa liwe dogo ama kubwa limeweza kuwa na sauti na sauti yake inasikilizwa” akasema Rais wa Baraza Kuu. Huku akifafanua kwamba wakati huo wa mkutano wa kwanza, sehemu kubwa ya dunia na hususani Afrika ilikuwa bado katika utawala wa kikoloni
“ Leo hii nchi wanachama ni 193 zikiwakilisha asilimia 99.5 ya idadi ya watu wote duniani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limekuwa chombo chenye uwakilishi jumuishi na chenye kutoa maamuzi kuhusu mambo mengi muhimu.
Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Sir Brian Urquhart, raia wa Uingereza na ambaye aliutumika Umoja wa Mataifa kwa miongo minne, pamoja na wawakilishi wa kudumu wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa.
1 comment:
Magufuli mchaguwe Mwanaidi awe balozi huko anafaa sana
Post a Comment