ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 20, 2016

Kalamu za Sh30 milioni zaipa ushindi Ukawa Dar

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akishauriana na
By Bakari Kiango, Mwananchi

Dar es Salaam. Kila kukicha watu hubuni mbinu ili wafanikiwe kwenye jambo fulani. Hivi ndivyo ilivyotokea Januari 16, kwa Ukawa kuja na mbinu ya kununua kalamu maalumu ya kuandikia na kupiga picha wakati wa upigaji kura wa uchaguzi wa mameya wa manispaa za Kinondoni na Ilala za jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Diwani wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob alishinda umeya wa Kinondoni kwa kura 38 dhidi ya 20 alizopata Benjamin Sitta wa CCM. Naibu Meya alichaguliwa Jumanne Mbunju wa Kata ya Tandale (CUF) aliyepata kura 38 dhidi ya 19 za John Manyama (CCM).

Kwa upande wa Ilala, aliyeshinda ni Charles Kuyeko (Chadema) aliyepata kura 31 na naibu ni Omari Kumbilamoto (CUF) ambaye pia alipata kura 31 za madiwani wa Ukawa baada ya wale wa CCM kususia.

Kabla ya uchaguzi huo, kulikuwa na vuta nikuvute na ushindani mkali, hali iliyosababisha Ukawa kuwa na wasiwasi wa kuhujumiwa na hivyo kuandaa mazingira ya kushinda, ikiwamo kununua kalamu hizo.

Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ukawa ambaye hakutaka kutajwa jina lake, viongozi walibuni mkakati huo uliowagharimu takriban Sh30 milioni katika ununuzi wa kalamu za kupigia kura na wakati huo huo kuwapiga picha wanaozitumia na kuandaa sehemu ya kufuatilia jinsi kura zilivyopigwa.

Kila mjumbe alipewa kalamu yenye jina lake na kuitumia katika upigaji wa kura.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliliambia Mwananchi kuwa waliamua kufanya hivyo baada ya Manispaa ya Temeke ambako madiwani wawili Ukawa waliipigia kura CCM.

“Ukiumwa na nyoka lazima ukiona jani ushtuke, hiki ndiyo tulichokifanya baada ya madiwani wetu wawili kutusaliti,” alisema Mdee.

Alisema walishanusa harafu ya rushwa kwa baadhi ya madiwani wao kuhongwa fedha kupitia kwa mmoja wa maofisa wa Chadema makao makuu.

Alisema baada kusikia taarifa hizo, walikaa chini na kutafakari na kuja na mbinu hiyo ambayo imekuwa mwarobani wa kuhakikisha Ukawa wanapata kura sahihi za wajumbe wake.

“Wanakinondoni wangetushangaa kama tungekosa umeya kwa idadi ya madiwani waliotupatia,” alisema Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).

“Kuna wajumbe mnakubaliana vizuri, lakini wakifika kwenye sanduku la kura wanabadilika. Kalamu imetusadia sana kwani tulikuwa 38, CCM 20, kura zilivyopigwa tulizipata zote kama tulivyotarajia,” alisema.

Alifafanua kuwa walimweka mtu maalumu wa kufuatilia mwenendo wa kila mjumbe wa Ukawa wakati wa kupiga kura.

“Kama nilivyosema juzi zile kalamu ukifungua tu ina kamera. Ukianza kuitumia kuna mtu maalumu aliyetarishwa kwa ajili ya kuangalia wajumbe wote wa Ukawa wanaopiga kura,” alisema.

Hata hivyo, alisema licha ya baadhi ya wajumbe wa Ukawa kuchukua fedha, lakini wametimiza wajibu wao wa kuhakikisha meya anakuwa chini ya umoja huo na iwe fundisho siku nyingine kwa wajumbe wao wengine.

Akizungumzia umeya wa Dar es Salaam, Mdee alisema wanajipanga vyema ili kuhakikisha jiji hilo linakuwa chini ya Ukawa kwa kuwa wana hazina kubwa ya madiwani wakataowawezesha kuibuka kidedea.

“Kwenye umeya wa Jiji tutakuja na staili tofauti, hizi tulizozitumia katika manispaa za Ilala na Kinondoni, tunaziboresha na tuna uhakika wa kunyakua umeya wa Dar es Salaam,” alisema Mdee.

No comments: