ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 14, 2016

Magufuli ampa zawadi ya kiwanja Samatta.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imetoa zawadi ya kiwanja kwa Mbwana Samatta kutokana na mshambuliaji huyo wa TP Mazembe na Taifa Stars kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, jana alimkabidhi Samatta hati ya kiwanja hicho kilicho Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Hii ndiyo hati yenyewe. Ila ukiwa tayari karibu ofisini kwangu ili nikukabidhi hati na vijana wakakuonyeshe kiwanja. Kitakuwa ni kiwanja katika sehemu nzuri kabisa, si zile sehemu watu wamefanya eneo liwe skwata,” alisema Lukuvi.

Mbali na kiwanja, Lukuvi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kumuaga Samatta kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa zawadi ya fedha taslimu kwa straika huyo matata ambazo hata hivyo, hazikuelezwa ni kiasi gani.

“Nimekupa hizi, huu mzigo ni wako kwa niaba ya serikali. Wewe mwenyewe ukiamua kuzionyesha, basi fanya hivyo,” alisema.

Baadaye Samatta alimkabidhi jezi yake TP Mazembe Lukuvi ambaye alisema ataiwasilisha kwa Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha katika hafla hiyo.

Baadaye Samatta pia alitoa jezi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ambaye amekuwa karibu yake kwa kipindi kirefu kabla hajaenda Nigeria alikoshinda tuzo ya Mwanasoka Bora na baada ya kurejea.

Nyota huyo wa zamani wa African Lyon na Simba, ametwaa tuzo ya Mwasoka Bora wa Afrika Anayecheza barani baada ya kuiwezesha TP Mazembe kutwaa taji la tano la Klabu Bingwa Afrika mwaka jana huku akiibuka Mfungaji Bora wa michuano hiyo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

This is very interesting, wabongo tunapenda sana lelemama. What about the other sectore like music, I thought Diamond has done a lot to promote the country (though am not a fan of his music).

Does he really need that? The plot and monies could have been used to assist many kids in need.

Look at Messi - 5 times Footballer of the year, not sure if he has received 5 houses from his country - nothing!

Our priorities - zinachekesha!