Letisia Ghamayu akionyesha daraja ambalo limeelezwa kuwa chanzo cha mafuriko yaliyosababisha vifo vya Watu nane, Msaidizi wa IGP, Ernest Mangu na familia yake . PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Siku moja baada ya Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Inspekta Gerald Ryoba na familia yake kufariki dunia kutokana na gari waliyokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika eneo la Kongwa mkoani Dodoma, mashuhuda wa tukio hilo wamesimulia mwanzo mwisho namna maafa yalivyowakuta.
Aidha, wakazi wa eneo hilo wameingiwa na hofu na kudai kuwa huenda kuna mzimu uliosababisha maafa hayo.
Maafa hayo yalitokea Jumapili Januari 3, 2016 majira ya saa tatu usiku katika eneo hilo ambalo Inspekta Ryoba na familia yake akiwamo mkewe Fidea John Kiondo, watoto wawili Gabriel Gerald Ryoba na Godwin Gerald Ryoba, msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sara na dereva wa gari hilo, F.3243 Koplo Ramadhan, wote walipoteza maisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalum na Nipashe, wakazi hao walisema kila mwaka eneo hilo limekuwa likijaa maji kutokana na uwapo wa mkondo wa maji unaotoka katika Kijiji cha Hembahemba lakini hakujawahi kutokea maafa makubwa kiasi hicho yaliyosababishwa na maji.
Inspekta Ryoba alipata ajali hiyo katika mtaa wa Majengo, Kibaigwa wilayani hapa maarufu kwa jina la Bwawani alipokuwa akitokea Geita kuelekea Dar es Salaam.
Akisimulia kuhusu maafa hayo, mmoja wa mashuhuda waliokuwapo katika eneo hilo, ambaye ni mlinzi wa Kituo cha Mafuta (Sheli) cha Olympic iliyopo jirani na eneo la tukio, Kinango Maganza, alisema hali hiyo imewatia hofu kubwa kutokana na mvua iliyonyesha ilikuwa ni ndogo lakini imesababisha maafa makubwa.
Alisema siku ya tukio mvua ilianza kunyesha majira ya saa 11:00 jioni na kukatika baada ya saa moja, lakini alishangazwa na kutokea kwa wimbi kubwa la maji ambayo yalikuwa yakiingia katika barabara ya lami kwa kasi na kufanya eneo hilo kujaa maji na magari kushindwa kupita.
Hata hivyo, alisema baadhi ya magari makubwa yaliendelea kupita kwa mwendo mdogo lakini maji yalizidi kujaa na magari mengine ilibidi yasimame.
“Mimi baada ya kuona magari yamesimama, niliingia ndani na kuendelea na shughuli zangu, baadaye alikuja dereva wa Noah kugonga na nilipofungua alikuwa akiomba hifadhi ya gari lake kutokana na kushindwa kuvuka eneo hilo baada ya maji kuingia katika gari hilo na kulifanya lizime na kushindwa kuwaka tena, hivyo walilifikisha sheli wakiwa wanalisukuma," alisema na kuongeza:
“Huyu dereva sina jina lake wala namba ya simu, yeye ndiye aliyenisimulia hali halisi hadi hilo gari la huyo polisi liliposombwa na maji kwa sababu alikuwa mbele yake wakiwa wanatazamana. Yeye alikuwa akitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma na gari lililosombwa na maji lilikuwa likitokea upande wa pili njia ya Dodoma kuelekea Dar es Salaam,”alisema Maganza.
Maganza alisema kwa mujibu wa dereva huyo wa Noah gari hilo wakati linavuka kulitokea wimbi kubwa la maji kutoka kushoto ambalo lilipiga kioo cha mbele hali iliyomfanya dereva wa gari la Inspekta Ryoba kushindwa kulimudu.
“Anasema wakati alipoona wimbi hilo yeye alizima gari na akabaki pale pale alipo, sasa huyu aliyepata ajali yeye alianza kupita na akakutana na hilo wimbi la maji na gari likateleza huku matairi mawili yakiwa juu. Dereva huyo ndiye aliyetuambia ameliona gari limetumbukia upande wa kushoto wa barabara,”alisema mlinzi huyo.
Alifafanua dereva wa Noah alikuwa akitokea barabara ya Dar es Salaam-Dodoma na gari ya Inspekta Ryoba ilikuwa ikitokea barabara ya Dodoma kwenda Dar es Salaam, na kwamba walikuwa mbele ya magari yote yaliyokuwa yamesimama.
“Polisi walipata taarifa baada ya madereva wa mabasi yaliyosimama kupiga simu na kuwajulisha kuwa kuna gari limesombwa na maji, hata polisi wao walivyokuja ilibidi waje hapa kwenye kituo cha mafuta kukaa hadi maji yalipopungua ndipo wakaanza jitihada za kulitafuta hilo gari, huku wakizuia magari mengine yasipite,”alisema Maganza.
Alisema kwa upande wake, alishuhudia polisi wakitafuta gari hilo na kutokana na wingi wa maji na tope zito ilifanya shughuli ya kulitoa iwe ngumu na walipofanikiwa walikuta kuna maiti ndani ya gari hilo.
“Mimi nina miaka mitatu hapa, lakini sijawahi kushuhudia vifo vya watu wengi kiasi hichi katika eneo hili ambalo kila mwaka maji hujaa hasa msimu wa mvua na huwa hata siku moja hayavuki lami kuja upande mwingine, hapa lazima kutakuwa na mizimu au jini,” alisema Maganza.
WAKAZI WA ENEO WASIMULIA
Naye mkazi wa eneo hilo, Leticia Ghamayu, alisema tangu aanze kuishi katika eneo hilo hajawahi kusikia maafa makubwa kiasi hicho ingawa baadhi husombwa lakini akadai huwa wanatoka hai.
“Haya maji huwa yanajaa hapa wakati wa msimu wa mvua lakini haya ya juzi yaliyojaa hadi mawimbi makubwa kwa kweli kuna kitu jamani, hata gari lenyewe sehemu iliyodondokea ni hatua tatu tu kutoka kwenye lami lakini maiti zingine zimekutwa ng’ambo ya pili ya barabara,”alisema mkazi huyo.
Alisema wakazi wa eneo hilo hukabiliana na hali hiyo kwa kutopita hadi maji yapungue na magari husimama hadi maji yanapopungua ndipo huendelea na safari.
“Hii barabara ya Dodoma- Dar es Salaam katika eneo hili la Kibaigwa, mtanana na Pandambili sio bure kuna kitu maana licha ya haya maafa hata ajali tu haziiishi ni mara kwa mara sasa sijui kuna jini au mizimu,”alisema Ghamayu.
Alibainisha kuwa kwa sasa wananchi wameingiwa na hofu na hali hiyo imekuwa gumzo kijijini hapo hivyo watakapoona hali hiyo wataacha kupita hadi maji yaishe.
Hata hivyo, mkazi mwingine wa eneo hilo, Selemani Hamisi, alisema tukio la kusombwa gari katika eneo hilo sio la kwanza kwani mwaka juzi kuna gari ya wanajeshi ilisombwa lakini hakuna mtu aliyefariki.
“Mimi naona tatizo sio mizimu tu, itakuwa ni hili daraja ni dogo, linashindwa kumudu maji hayo mengi yanayopita kutoka mkondo wa maji wa Hembahemba hadi huko Kijiji cha Ndurugumi, yaani inabidi lijengwe daraja kubwa ili roho zetu zisiwe juu juu,”alisema Hamisi.
Kwa upande wake, Helena Simba ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo, alisema si mara ya kwanza eneo hilo kujaa maji, kwani zamani hali ilikuwa mbaya zaidi na waliomba wawekewe daraja, lakini lilowekwa ni dogo na halilingani na maji yanayopita katika eneo hilo.
“Kwa kweli hili eneo ni korofi, lakini halijawahi kuleta maafa kiasi hichi, matukio ya watu kusombwa maji yapo lakini hakuna aliyefariki, huwa wanaokolewa wakiwa hai, sasa hili la juzi limekuwa gumzo mpaka watu wanahisi kuna jambo si bure,”alisema mkazi huyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kibaigwa, Fotina Wimbe, alisema vifo hivyo vya kusombwa na maji ni vya mara ya kwanza kutokea katika eneo hilo ingawa kumekuwa na matukio ya watu kusombwa na maji ila wakiokolewa wanakutwa hawajafa.
“Msongamano wa maji hapa ni wa muda mrefu, tatizo ni daraja dogo maana hata mwaka juzi gari lilisombwa sijui lilikuwa la wanajeshi, lakini hakuna aliyekufa ila safari hii hata hatuelewi hiki kitu gani maana ni maafa makubwa...vifo vya watu nane,”alisema mjumbe huyo.
Aliongeza kuwa wamekuwa wakitambikia mizimu wakati wanapokosa mvua, lakini kwa ajali mbalimbali zinazotokea katika eneo hilo hawajawahi kutambika.
Alibainisha kwa tukio la ajali ya Inspekta huyo, wananchi wamekuwa wakizungumza sana huku wakihusisha huenda eneo hilo kuna jini.
Mwili wa marehemu Inspekta Ryoba na familia yake ilisafirishwa jana na kufika Kijijini kwao Kasamwa mkoani Geita majira ya mchana na maziko yanatarajiwa kufanyika kijijini hapo leo.
CHANZO: NIPASHE
2 comments:
TUNASHINDWA KUENDELEA KWA SABABU AKILI ZA MWAFRIKA HATA AKISOMA VIPI BADO ANAAMINI KINACHOTOKEA KINA SABABU HATA MAJANGA HAYO YANAYOTOKANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA. ETI "HAYO MAFURIKO HAYAJAWAHI KUTOKEA AU SIJAWAHI KUONA". SI NDIYO YAMETOKEA MWAKA HUU??? ETI "HAPO SI BURE KUNA JINI NA MIZIMU" HAO JINI NA MIZIMU MUMEWAONA WAPI???? KWELI UJINGA NA MARADHI NA UMASKINI ALIOSEMA NYERERE TUUPIGE VITA, HATUUWEZI TENA KAMA TUNA JAMII YA NAMNA HII INAYOFIKIRIA KILA KITU UCHAWI TU, MTU AKIUGUA UENDAWAZIMU, MALARIA, TUMBO, KICHWA ETC...ETC UTASIKIA SI BURE KALOGWA WAKATI MAZINGIRA WANAYOISHI INAZALISHA MBU KWA KWENDA MBELE!! NI AIBU KWA JAMII NA KWA NCHI YETU BADALA YA KWENDA MBELE TUNAENDELEA KURUDI NYUMA......WATU WAZIMA NA AKILI ZAO WENGINE NI VIONGOZI WAMESHAKATIKA MISHIPA YA AIBU WANAUA WENYE ULEMAVU WA NGOZI WAKIJUA WATAPATA VYEO NA NAFASI KUBWA SERIKALINI NA KWENYE BIASHARA ZAO. JUZI MAMA MMOJA MWENYE SHULE ALIPOTEZA SHILINGI MILLIONI 600 KUMPA MGANGA WA KIENYEJI ILI AMTENGENEZEE DAWA ILI SHULE YAKE IVUTIE WANAFUNZI WENGI BAADA YA KUKATAA SHARTI LA KUUA MWANAFUNZI MMOJA ALIYEPO HAPO SHULENI KIMAZINGARA, NDIYO MAANA NASEMA NCHI YETU HATA WASOMI WAMESHAPOTEZA USOMI KWA KUFUATA MAMBO YA KIPUUZI YA KIMAZINGAOMBWE. SISHANGAI SANA KUTOKANA NA PEW RESEARCH WATANZANIA TUNAONGOZA KWA ASILIMIA 93 KWA WALE WANAOAMINI UCHAWI, SASA NADHANI IMESHAPITA HATA HIYO ASILIMIA 93....TUNAKWENDA MBELE KUYATUKUZA MAJINI NA MIZIMU!!!
Daraja hili kajenga mhandisi gani
Magufuli ulikuwa ujenzi hukuona daraja hili
Hata Mimi kipofu daraja ni zirooooooooooo
Design yake shittttt
Huwezi kupokea maji mengi kwenye design hii ya daraja
Post a Comment