Dar es Salaam. Rais mstaafu Benjamin Mkapa amesema yuko tayari kufanya kazi yoyote na kutoa ushirikiano wake kwa serikali ya Rais John Magufuli endapo atahitajika.
Mkapa aliyeambatana na Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Warioba ametoa kauli hiyo leo punde baada ya kukutana na Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.
“Rais Mstaafu Mkapa pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo,” taarifa iliyotolewa na Ikulu leo mchana imeeleza.
Kwa mujibu wa Ikulu, malengo ya mkuu huyo wa zamani wa nchi kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi, kuunda serikali na kumtakia heri ya Mwaka Mpya.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amempongeza katika juhudi zake katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi yakiwemo afya na maji.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Jaji Warioba amewataka Watanzania wote kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi anazofanya ikiwemo kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali ya umma.
"Lazima kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuachia, pale ulipo kama ni mambo ya rushwa uanzie hapo hapo, kama ni mambo ya matumizi mabaya ya madaraka anzia hapohapo, tusije tukamuachia Rais pekee yake, yeye awe kiongozi wetu, lakini Watanzania wote tushughulike na matatizo hayo," amesisitiza Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake