ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 20, 2016

Ofisi ya Kamishna Mkuu TRA yavunjwa, kompyuta zaibwa



Dk Philip Mpango
By Peter Elias, Mwananchi

Dar es Salaam. Watu wasiojulikana, wamevamia na kuvunja Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuiba kompyuta na vifaa vingine.

Habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam zinasema miongoni mwa kompyuta zilizoibwa ni ile iliyokuwa inatumiwa na Dk Philip Mpango alipokaimu nafasi ya Kamishna Mkuu wa TRA, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, huenda kompyuta hiyo ikawa na taarifa muhimu kuhusu ukwepaji kodi na sakata la makontena bandarini.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema tayari jeshi hilo linawashikilia watu wanne kwa uchunguzi zaidi.

Sirro alitaja vitu vilivyoibwa katika ofisi hiyo kuwa ni kompyuta mbili, televisheni moja na king’amuzi.

Alisema wanaoshikiliwa ni walinzi wawili kutoka kampuni ya Suma – JKT ambao walikuwa zamu usiku huo, katibu muhtasi pamoja na karani wa ofisi hiyo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alikanusha kutokea kwa wizi huo akisisitiza kwamba lilikuwa ni jaribio la wezi kutaka kuvunja ofisi hiyo.

Kayombo alisema hakuna wizi wowote uliotokea katika jaribio hilo kwa sababu hawakufanikiwa kuingia ndani. Alisema mali zote ziko salama na suala hilo tayari tukio hilo limeripotiwa polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amefanya mabadiliko katika mamlaka hiyo kwa kumwondoa aliyekuwa Kamishna Mkuu, Rished Bade na kumteua Dk Mpango kukaimu nafasi hiyo, kabla ya kumteua kuwa Waziri wa Fedha na nafasi hiyo kuchukuliwa na Alphayo Kidata.

Katika kipindi hicho, baadhi ya wafanyakazi wamewajibishwa kwa kusimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ama kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato au kushirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi na kulisababishia hasara Taifa.

No comments: