Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius Likwelile (katikati) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu Serikali ilivyojipanga kuboresha na kuhudumia sekta mbalimbali nchini ikiwemo elimu, umeme, maji na miundombinu. Kulia ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alfayo Kidata na kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu akisistiza wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu mapato na matumizi ya Serikali yalivyoboreshwa na uchumi wa nchi kuimarika na kutengemaa.
Serikali imetoa jumla ya Sh. Bilioni 318.406 kwa mwezi wa Januari mwaka 2016, kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini na Sh. Bilioni 538.5 kwa mishahara ya watumishi wa Umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Servacius Likwelile alisema kuwa Serikali inajivunia kufanikiwa kutumia fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo hadi sasa Serikali imetumia kiasi cha Sh. Bilioni 71.2 tu kutoka fedha za nje.
Dkt. Likwelile alisema mapato yanayokusanywa nchini yamewezesha kutekeleza sera ya elimu bure ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali ilitoa kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya ruzuku, ada na chakula kwa shule za bweni pamoja na mahitaji mengine ambapo mwezi wa Januari 2016 Serikali imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa ajili ya kutekeleza Sera hiyo.
Aliongeza kuwa katika ulipaji wa madeni ya wakandarasi nchini , Serikali imetoa Sh. Bilioni 130 kwa mwezi Januari mwaka 2016 ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 ilitoa Sh. Bilioni 193.
Kwa upande wa Mfuko wa Barabara, Katibu Likwelile alifafanua mradi huo umetengewa kiasi cha Sh. Bilioni 47.89 na kuongeza kuwa Benki kuu ina fungu la mfuko huo ambapo nayo imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 76.3.
Dkt. Likwelile alisema kuwa Halmashauri zitapelekewa kiasi cha Sh. Bilioni 20.52 kwa ajili ya kuboresha barabara na jumla mfuko huo kufikia kiasi cha Sh. Bilioni 274.71.
Akifafanua kuhusu miradi ya umeme, Dkt. Likwelile alisema kuwa mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali ililipa deni la TANESCO kiasi cha Sh. Bilioni 80 za mradi wa Kinyerezi II na kwa mwezi Januari mwaka 2016 kiasi cha Sh. Bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo.
Hali hii imefikisha kiasi cha Sh. Bilioni 120 kwa ajili ya kulipa madeni na kuendeleza uzalishaji wa umeme nchini.
Alisema kiasi cha Sh. Bilioni 21.959 kimetengwa kwa ajili ya mradi wa umeme vijijini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina mfuko wa mradi huo ambao kwa sasa una kiasi cha Sh. Bilioni 21.9 na kuongeza kuwa huduma ya umeme kwa wananchi itaimarika.
Alifafanua kuwa Serikali imeanzisha mfuko wa maji Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo mpaka sasa mfuko huo una jumla ya kiasi cha Sh. Bilioni 46.3.
Aidha, BoT imetoa Sh. Bilioni 12.5 kuendeleza miradi ya maji ambapo kwa Januari mwaka 2016 Serikali imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 7.7.
Serikali imetenga kiasi cha Sh Bilioni 82.2 kwa mwezi wa Januari ili kuweza kulipa pensheni za wastaafu, na kwa wale wastaafu walio katika daftari la kudumu ambapo wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 33.3 kwa ajili ya malipo yao.
Wabunge wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 35.5 kwa ajili ya mkopo wa magari ambapo kila mbunge atapata kiasi cha Sh. Milioni 90, kiasi cha Sh. Milioni. 45 ni ruzuku na Sh. Mil. 45 ni mkopo ambao utalipwa ndani ya miaka 5.
Aidha, Serikali imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 784.3 kwa ajili ya kulipa deni la taifa.
Naye Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alibainisha kuwa hali ya makusanyo ya mapato nchini iko vizuri ambapo kwa mwezi Januari 2016, makadirio yalikuwa Sh. Trilioni 1 na Bilioni 45 na hadi kufikia sasa kiasi cha Sh. Trilioni 1 na Bilioni 31 zimeshakusanywa.
Matarajio ya TRA ni kukamilisha kukusanya kiasi cha Sh. Billioni 14 zilizosalia.
Aidha, Kidata alibainisha kuwa uingizaji wa bidhaa kupitia bandarini bado uko vizuri licha ya minong’ono kuwa uzuiaji wa mianya ya ukwepaji kodi imepunguza uingizaji bidhaa ambapo kwa mwezi Januari Bilioni 111 zimekusanywa kutokana na ushuru wa forodha.
Kidata alitoa wito kwa kila mtanzania kulipa kodi na kutoa taarifa za wakwepa kodi ili kuweza kukuza mapato ya nchi.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu amepongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.
Alisema kuwa uchumi umekua na unazidi kuimarika licha ya changamoto za kiuchumi duniani ambapo uchumi wa nchi umekua kwa asilimia 7 na unategemewa kukua miezi ijayo kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji nchini.
Mfumuko wa bei unaendelea kubaki ndani ya kiwango cha tarakimu moja, licha ya ongezeko dogo katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kupanda kwa bei za vyakula.
Alisema kuwa mfumuko wa bei ulikuwa asilimi 6.8 mwaka 2015, ukilinganishwa na asilimia 6.1 kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2015.
Wakati huo huo mfumuko wa bei usiojumuisha chakula na nishati uliendelea kubaki katika viwango vya chini ya asilimia 2.5 kutokana na hatua mbalimbali za kisera zilizochukuliwa na BoT.
Prof. Ndulu alifafanua mapato ya fedha za kigeni yanaendelea vizuri ingawa bei ya dhahabu imeshuka kutoka Bilioni 2.5 hadi Bilioni1.3.
Sekta ya utalii imesaidia kuimarisha fedha za kigeni kwani mapato yameongezeka kutoka Bilioni 1.5 hadi Bilioni 2.2.
Sekta ya viwanda nayo imeshika nafasi ya pili katika kuongeza fedha za kigeni nchini ambapo mwaka 2015 mapato yalikuwa Bilioni 1 na kwa sasa yamefikia Bilioni1.5.
Aidha, Prof. Ndulu aliongeza kuwa sekta ya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi imesaidia kuimarisha fedha za kigeni ambapo mapato yamefikia Dola Bilioni11 kwa mwaka.
Hadi kufikia sasa Tanzania imenufaika kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika uingizaji bidhaa hiyo kwa asilimia 44.
Serikali inatarajia kuendelea kuimarisha uchumi ili kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati hadi ifikapo 2025.
Imetolewa na Wizara ya Fedha na Mipango
Kitengo cha Mawasiliano
1 comment:
Asante. ni jambo zuri na mawazo mipango mizuri. Je swala linalohusu wazee na wastaafu ambao wamelitumikia taifa kwa muda mrefu wengi wakiendelea kukosa huduma muhimu linatafakariwaje. Mbona kuna dalili za kutokuwajali na wabunge wetu wameendelea kuwa kichekesho huko bungeni kila kunapokucha. Tatizo kubwa lililopo ni pale wapinzani ambao ndio chachu ya maendeleo na mabadiliko wanapoleta hoja manufaa viongozi wa juu ndio wnaoonekana kuyapinga. TUmewaweka mle ndanii kuleta maendeleo serikali iwe na uchambuzi zaidi.
Post a Comment