ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 20, 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUSITISHWA (KUSIMAMISHWA) KWA LESENI ZA WATOA HUDUMA ZA MAUDHUI YA UTANGAZAJI KWA KUSHINDWA KULIPIA ADA ZA LESENI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
 

TAARIFA KWA UMMA

KUSITISHWA (KUSIMAMISHWA) KWA LESENI ZA WATOA HUDUMA ZA MAUDHUI YA UTANGAZAJI KWA KUSHINDWA KULIPIA ADA ZA LESENI

Mnamo tarehe 15 Januari 2016 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa taarifa kwa umma kuhusu kufungia Watoa Huduma za Maudhui ya Utangazaji (Redio na Televisheni) 27 waliokuwa wanadaiwa ada na tozo mbalimbali zinazotokana na leseni zao. Aidha,tarehe 18 Januari 2016 ilichapichwa taarifa ya makampuni ambayo yatafungiwa kwa muda ikiwa watashindwa kulipa ada na tozo hizo katika magazeti mbalimbali. Nia ilikuwa kuwakumbusha kwa mara ya mwisho utekelezaji wa wajibu wao kwa mujibu wa sheria na masharti ya leseni.

Baada ya taarifa hizo katika magazeti Mamlaka ilipokea maombi kutoka katika vituo vingi vikiomba kutokufungiwa vituo vyao na kwamba waruhusiwe kufanya malipo siku hiyo ya tarehe 18 Januari 2016 na kuwasilisha stakabadhi katika ofisi za TCRA kuthibitisha kuwa malipo yamekamilika. Mamlaka ilikubali maombi hayo na hadi kufikia mwisho wa saa za kazi tarehe 18 Januari 2016, redio 12 kati ya 20 na kituo kimoja kati ya vituo vya television 6 vimelipa ada na tozo zote au kubakiza kiasi kidogo cha deni ambalo walikuwa wanadaiwa na hivyo kuviruhusu kuendelea kutoa huduma ya utangazaji kama kawaida. Kwa wale ambo hawajamaliza malipo yote Mamlaka inaingia nao mkataba maalumu wa lini bakaa la deni litalipwa, na kwamba wasipofanya hivyo kwa muda uliokubalika hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa.


Hadi kufikia tarehe 19 Januari 2016 ni vituo 13 ambavyo havijaweza kulipa deni wanalodaiwa na wala hawajawasiliana na Mamlaka. Hivyo basi Mamlaka imeendelea na utekelezaji wa sheria wa kusitisha utoaji wa huduma za utangazaji kwa vituo vya redio na television vilivyoorozeshwa hapa chini, hadi hapo watakapotekeleza wajibu wao wa kulipa ada na tozo wanazodaiwa. Hii inamaanisha ya kuwa vituo hivi vitafunguliwa pindi watakapolipa ada na tozo husika. Ikiwa watashindwa kufanya hivyo kwa muda wa miezi mitatu kuanzia tarehe 19 Januari 2016 hatua zaidi za kisheria kwa mujibu wa Kifungu 22(a) cha Sheria ya EPOCA ya Mwaka 2010 zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufuta leseni zao za kutoa huduma ya utangazaji.

Vituo vilivyofungiwa ni;

1.   Breeze FM ya Tanga
2.   Country FM Radio ya Iringa
3.   Generation FM Radio ya Mbeya
4.   Hot FM Radio ya Mbeya
5.   Impact FM ya Dodoma
6.   Kifimbo FM Radio ya Dodoma
7.   Rock FM Radio ya Mbeya
8. Iringa Municipal TV
9. Sumbawanga Municipal TV
10. Tanga City TV
11. Mbeya City Municipal TV

Mamlaka inapenda kuwakumbusha makampuni yote yaliyopewa leseni ya kutoa huduma za utangazaji wa redio na televisheni na huduma zingine zote zinazosimamiwa na Mamlaka kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao wa kisheria na masharti ya leseni ili kuondoa usumbufu usio wa lazima kwao na kwa watumiaji.

Inawezekana ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake.

IMETOLEWA NA
  
Dr. Ally Y. Simba
MKURUGENZI MKUU


20 Januari, 2016

No comments: