ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 23, 2016

Taasisi mpya ya kukabiliana na Vifo vya Wajawazito na Watoto Zanzibar ( KANGA) yazinduliwa

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 23/01/2016

Katika kukabiliana na Vifo vya Wajawazito na Watoto Zanzibar Taasisi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kama KANGA imezinduliwa rasmi ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo nchini.
Mwenyekiti wa Taasisi ya KANGA Dkt.Mohamed Hafidh akitoa maelezo ya Taasisi hiyo ambayo itahusika katika kukusanya michango mbalimbali kutoka kwa wadau kwa lengo la kupambana na Vifo vya Wajawazito na Watoto nchini.Uzinduzi wa Taasisi ya KANGA ulifanyika katika Viwanja vya Hospitali ya Mnazi mmoja na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar

Uzinduzi wa Taasisi hiyo umefanyika katika Viwanja vya Hospitali ya Mnazi mmoja na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya Zanzibar.

Akitoa ufafanuzi wa kuanzishwa kwake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Dkt.Mohamed Hafidh amesema Serikali na Taasisi binafsi zinawajibu wa kuzidisha mikakati ya kukabiliana na Vifo kwa akinamama na watoto ili kuwa na taifa endelevu.

Amebainisha kuwa wapo baadhi ya watu wenye uwezo wa kuchangia lakini wanashindwa kujua wapi watapeleka Misaada yao ili kuokoa maisha ya watoto na akinamama.

Dkt. Mohamed ameongeza kuwa hata Serikali kupitia Wizara ya Afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali za matibabu nakwamba uwepo wa Taasisi ya KANGA kutasaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali kukabiliana na tatizo hilo nchini.

“Ukweli nikwamba wapo wasamaria wema wanaguswa na hali ya vifo vya Wajawazito na Watoto lakini wanashindwa wapi kwa kupeleka misaada yao lakini kupitia Taasisi hii ya KANGA basi itakuwa ni sehemu muafaka ya kupeleka misaada yao na bila shaka lengo litafikiwa”Alisema Dkt. Mohammed Hafidh

Dkt Mohamed amesema hali ya Vifo nchini bado inatisha na kufafanua kwamba kati ya Kinamama Wajawazito Laki moja,wastani wa 460 hupoteza maisha yao nchini ambapo kwa nchi za Ulaya Idadi kama hiyo ni wastani wa watu sita wanaopoteza maisha.

Ameongeza kuwa Wastani wa Watoto 29 kati ya Elfu moja wanaozaliwa hufariki dunia nchini Tanzania ambapo kwa nchi za Ulaya ni Wastani wa watoto watatu wanaopoteza maisha miongoni mwa watoto Elfu moja.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Shekh Abdallah Talib amewaomba Viongozi na wananchi kwa ujumla kuiunga mkono Taasisi hiyo kwa kuchangia jitihada zake za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wazazi na Watoto katika kipindi cha ujauzito na kujifungua.

Amesema kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe ameahidi kukwata kiasi Fulani cha Mshahara wake kila mwezi ili kuchangia harakati za Taasisi ya KANGA.

“Kwa namna ambavyo nimeguswa na Malengo ya Taasisi ya KANGA na kwa namna ambavyo Tatizo la Vifo kwa Wajawazito na watoto linavyoendelea naahidi kukatwa Mshahara wangu kila mwezi kusapoti Taasisi hii”Alisema Shekh Talib

Taasisi ya KANGA ambayo imezinduliwa imejikita katika kujitolea kupambana na tatizo la Vifo kwa watoto na akinamama wakati wa ujauzito ambapo pia malengo ya baadae itaratibu uwepo wa Madaktari Wanawake wa kutosha ili taratibu za Uzazi zote Hospitalini zifanywe na Wanawake wenyewe badala ya Wanaume kama ilivyo sasa.

Katika uzinduzi huo Taasisi mbalimbali zilihudhuria na kutoa michango yao ikiwemo Mfuko wa Huduma za jamii Zanzibar ZSSF, Bank ya Watu wa Zanzibar, Taasisi ya Daraja Faoundation.
Baadhi ya wageni waliohudhuria katika uzinduzi wa Taasisi ya KANGA ambayo itahusika katika kukusanya michango mbalimbali kutoka kwa wadau kwa lengo la kupambana na Vifo vya Wajawazito na Watoto nchini.Uzinduzi wa Taasisi ya KANGA ulifanyika katika Viwanja vya Hospitali ya Mnazi mmoja na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Shekh Abdallah Talib kushoto na Mwenyekiti wa Taasisi ya KANGA Dkt.Mohamed Hafidh kulia kwa pamoja wakiwakabidhi Viongozi kutoka Taasisi ya “DARAJA Foundation” KEKI waliyoinunua katika harambee ya kuichangia Taasisi ya Kanga kama njia ya kuiunga Mkono Taasisi hiyo. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Shekh Abdallah Talib akitoa hutuba yake kabla ya kuizindua Taasisi ya KANGA ambayo itahusikana ukusanyaji wa michango mbalimbali kutoka kwa wadau kwa lengo la kupambana na Vifo vya Wajawazito na Watoto nchini.Uzinduzi wa Taasisi ya KANGA ulifanyika katika Viwanja vya Hospitali ya Mnazi mmoja na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya Zanzibar.

No comments: