Miongoni mwa watuhumiwa hao ni waliohusika katika kashfa ya kifisadi ya malipo tata ya dola milioni sita (Sh. bilioni 12.6) kwenda kwa Kampuni ya EGMA.
Uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo umeshakamilika na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuombewa kibali cha kuwafikisha mahakamani.
Kadhalika, Takukuru imekamilisha uchuguzi wa sakata la ununuzi wa mabehewa feki ya kubebea kokoto ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kuomba kibali cha DPP kuwafikisha mahakamani watuhumiwa waliobainika kujihusisha na rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na Sheria ya Ununuzi wa Umma katika mabehewa hayo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi kubwa 36 za rushwa na ufisadi zinazowahusu vigogo wa serikali na wafanyabiashara, ambapo kati ya hizo nne wameshazikamilisha.
Mlowola alisema miongoni mwa kesi hizo ni ya hati fungani, inayoihusiha Kampuni ya EGMA na Benki ya Stanbic, ambapo katika uchunguzi wamebaini kwamba fedha hizo zilitakatishwa na watumishi wa umma wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi ya watu kutoka sekta binafsi huku wakifahamu fedha hizo wamezipata kwa njia haramu.
EGMA ni kampuni iliyopewa kazi ya ushauri elekezi katika mauzo ya hati fungani za dola milioni 600 (Sh. trilioni 1.3) ambazo Serikali ya Tanzania iliziuza kwa Benki ya Standard ya Uingereza, wamiliki wake wakiwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, Gasper Njuu na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Mitaji ya Umma Tanzania, Dk. Fratern Mboya, ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Tuko kwenye hatua nzuri kukamilisha uchunguzi huu na watuhumiwa wote bila kujali hadhi au nafasi ya mtu pamoja na taasisi zilizohusika watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema Mlowola.
Fedha hizo, dola milioni sita (Sh. bilioni 12.6), ziliingizwa kweye akaunti ya EGMA na ndani ya siku 10, zilitolewa kupita Benki ya Stanbic kinyume cha taratibu za kibenki.
Baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya ukaguzi katika Benki ya Stanbic, ilitoa taarifa kwa Serikali ya Uingereza kupitia Taaasisi ya Kupambana na Rushwa Kubwa Uingereza (SFO) ambayo ilianzisha uchunguzi uliosababisha kesi kufunguliwa.
Mahakama hiyo iliamuru Serikali ya Tanzania irejeshewe dola za Marekani milioni saba (Sh. Bilioni 15.03) baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu huo.
Baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama hiyo na SFO, ilibainika kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni dola milioni sita (Sh. bilioni 12.6) zililipwa kwa EGMA.
Hadi sasa BoT imeitoza Benki ya Stanbic faini ya Sh. bilioni tatu kwa kosa la kukiuka taratibu za kibenki.
Kuhusu kesi ya mabehewa ya kokoto ya TRL, shauri hilo limeshakamilika uchunguzi wake na jalada limeshapelekwa kwa DPP kuomba kibali cha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa.
Mabehewa hayo 274 yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engeneering and Industrial Ltd ya India yaliyokuwa na thamani ya dola 28,487,500 (Sh. bilioni 61.2).
Kadhalika, Mlowola alisema wameshakamilisha uchunguzi wa kesi ya Shirika Hodhi la Reli nchini (RAHCO), inayomhusu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake, Mhandisi Benhadard Tito, kuhusu ukiukwaji wa sheria na taratibu za kuwapata wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa.
Alisema watuhumiwa kwenye kesi hiyo wameshamatwa na kuhojiwa akiwamo Raia wa Kenya, Kanji Muhando, ambaye alikuwa wakala wa kumpata mzabuni.
Alisema Takukuru wako kwenye hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi huo na watawafikisha mahakamani wote watakaobainika kujihusisha na rushwa bila kujali hadhi zao.
Kwa mujibu wa mtandao wa World Transport Africa, umbali wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma ni kilometa 2,561 ambayo ujenzi wake unatarajia kumalizika mwaka 2020 kuanzia Mpiji (Dar es Salaam) hadi Kigoma.
Vilevile kwa mujibu wa mtandao wa (a4architect.com) Kampuni ya Ujenzi ya China Communiucations Construction Limited (CCC LTD), imetoa makadirio ya gharama za kujenga reli ya kiwango cha 'standard gauge' kutoka Kenya, Uganda hadi Rwanda kuwa kilomita moja ni Shilingi za Kenya milioni 413, sawa na Sh. bilioni 8.6 za Tanzania.
Hivyo, kwa umbali wa kilomita 2,561 wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, Tanzania itahitaji kutumia Sh. trilioni 22 hadi kukamilika kwake.
Mbali na kesi hizo, alisema Takukuru pia imeshakamilisha uchunguzi wa ukwepaji kodi wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil, ambayo inahusu udanganyifu na ukwepaji kodi kwa kuuza kwenye soko la ndani mafuta ya petroli lita 17,461,111.
Kampuni hiyo inadaiwa kudanganya kuwa zimesafirishwa kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kupitia Zambia. Mlowola alisema kitendo hicho cha udanganyifu kimeisababishia serikali hasara ya takribani Sh. bilioni 8.5.
Alisema baada ya uchunguzi kukamilika, Takukuru imeamuru mtuhumiwa na washirika wake kuzirejesha fedha hizo serikalini ndani ya miezi miwili.
ATOA ONYO
Mlowola aliwaonya maofisa wa umma na watendaji, ambao wameshafanya rushwa na ufisadi kuwa sehemu ya kazi zao na miradi ya kuwaingizia kipato kuwa wajitafakari kabla hawajaamua kujihusisha na vitendo hivyo.
Alisema kwa maofisa maduhuli na watekelezaji wa ukusanyaji kodi, kwa atakayekamatwa kwa kujihusisha na ubadhirifu wa fedha na mali za umma, Takukuru haitamwonea haya ofisa yoyote.
Mkurugenzi huyo alisema kwa wale wote watakaohusika kwenye matumizi ya fedha za umma wafuate sheria, kwa kuwa wale watakaokiuka taratibu za ununuzi wa umma, hawatavumiliwa.
“Rais anaposema amejipa kazi ya kutumbua majipu, tambueni kwamba Takukuru ndiyo vidole vya Rais katika kuyatumbua majipu hayo, na mimi ndiyo dole gumba la kutumbulia majipu hayo, na muelewe kwamba mwenye vidole akishaamua kutumbua jipu, kazi ya vidole ni utekelezaji tu,” alisema Mlowola.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment